Prime
NIKWAMBIE MAMA: Hivi wote tunakijua tunacho kichagua?

Watanzania ni watu wanaohitaji elimu kila sekunde. Huwa wanafurahishwa bila kujua kinachowafurahisha, na wakati mwingine wanachukizwa bila kulijua chukizo lao.
Wanaweza kuingia taabuni kutokana na watu wabaya wanaowazunguka, lakini wakawa tayari kuwalinda watu hao wawe ni ndugu au wahamiaji haramu. Inawezekana maisha ya kidugu waliyozoeshwa ndiyo sababu ya tabu zao.
Ni watu wasiopenda kujifunza kutokana na makosa. Tunaona mara nyingi nyakati za chaguzi wakiingia kwenye mitego ya viongozi waongo na wabovu.
Hawana muda wa kutathmini kazi za viongozi wao, bali husikiliza na kunukuu nyimbo za kampeni. Baada ya hapo wanageuka watani wa jadi kama wale wa Jangwani na Msimbazi: “Mwaka huu hatuwaachii hata jimbo moja!” Hivi chaguo lao ni chama, mgombea au sera?
Nauliza hivi kwa sababu nina uhakika asilimia kubwa ya wapigakura hawajui wanachokitaka. Ukiwauliza watu walio karibu yako, kila mmoja wao atakupa jibu litakalokushangaza.
Wapo wanaochagua kutokana na mapenzi, na wapo wasiochagua kwa sababu ya chuki.
Huu sasa ndio mtindo wa watani wa jadi.
Hata kama chama chake hakina sera, atakipigia kura kwa lengo la kuwakoga tu pale kitakapotangazwa kuwa mshindi.
Wenzetu ambao leo tunawaona wana maendeleo walikuwa kama sisi. Lakini wakagundua kuwa kazi haihusiani na mapenzi wala chuki.
Unaweza kufanya kazi na mtu usiye na mapenzi naye, matokeo yakawa bora zaidi kuliko kufanya kazi na umpendaye.
Hawa wanatufundisha jinsi ya kutokutazamana usoni wakati wa kazi, bali wanatazamana kwenye bidii na uwajibikaji. Kwenye mafaili na miradi.
Bosi mmoja alikwenda kujipigia kura jimboni. Aliongozana mkewe na watoto wawili. Njiani hakuacha kuwakumbusha kuwa kuchukua kwake jimbo ndio kutengeneza maisha yao.
Kila mtu atawaheshimu kama familia ya Mheshimiwa, kwa maana hiyo watapata fursa hadi za kuuza kwa wenzao.
Kipato chao pia kitaongezeka kwa sababu bosi atakuwa anazichanga hata kama atakuwa anasinzia tu mjengoni.
Wakapiga kura kwa amani na utulivu mkubwa. Matokeo yalipotangazwa, yalimshangaza bosi huyu hadi kumtia shinikizo la damu.
Alizinduka akiwa wodini akiwaza kwa sauti juu ya matokeo yale: “Hivi inakuwaje nipate kura moja wakati tumeenda wanne; mimi, mke wangu na watoto wawili.
Wote tumepiga kura na wamesema hakuna kura iliyoharibika. Ina maana nimejipigia kura peke yangu au nimeibiwa?”
Kweli siasa ni kiboko. Bosi huyohuyo angetangaza upinzani dhidi ya rushwa, si ajabu asingepata hata kura yake mwenyewe.
Kila mtu angemguna na kusema kuwa hayo ni maneno ya mtu mwenye njaa. Hii ndiyo sababu ya kwa nini kiongozi akisimama kwenye mstari ulionyooka watu humchukia. Akifunga mianya ya rushwa hela inapotea huku mtaani. Maana yake hela inaondoka mifukoni na kurudi kwenye mifumo.
Miradi itaendelezwa, huduma za jamii zitaboreshwa na miundombinu itarekebishwa. Hakutakuwa na sababu ya kupeana rushwa iwapo mifumo yote itakwenda kama ilivyokusudiwa. Matajiri wenye viwanda na wafanyabiashara wakubwa wanapodaiwa matrilioni ya fedha za kodi, wanaikwepa mifumo na wanaishia kuwahonga wasimamizi wasio waaminifu. Fedha zinazagaa mtaani na Serikali inakosa fedha za miradi.
Pamoja na Watanzania kujinadi kuwa wana umoja usio na mfano, bado utaona kuwa Watanzania hawa ni wabinafsi kupindukia.
Mbadhirifu mmoja anakuwa tayari kuwaharibia daima mamilioni ya wenzake, ilimradi yeye pekee apate kutesa japo kwa siku mbili.
Yupo tayari kufilisi shirika la umma lililoajiri na kuhudumia mamilioni ya wananchi kwa faida ya mchepuko mmoja tu wa uswahilini.
Wapigakura ni lazima watambue kwa nini wanatimiza haki yao ya kidemokrasia. Wasibwetezwe kwa ahadi zisizotekelezeka na maneno matupu kutoka kwa wagombea wasiojitambua.
Hata kama mgombea hana sura nzuri na maneno ya kumtoa nyoka pangoni, kitu cha msingi anachoweza kuwavutia nacho ni sera. Kwamba atatumia njia zipi kuwavusha kutoka kwenye korongo waliloshindwa wenzake. Na yamtoke mtimani, siyo mdomoni.
Mpango wa kusikiliza ahadi zilezile kwenye kila uchaguzi umepitwa na wakati. Tena wapigakura tulio makini tunaanza kuwauliza wanasheria njia za kuwaadabisha wagombea waongo.
Yeyote atakayeahidi bila kutekeleza achukuliwe kuwa amewadanganya wananchi, na itafutwe namna ya kumdai.
Haiwezekani kiongozi anatoa ahadi katika miongo miwili mizima, kila anaporudi anadai muda haukutosha.
Haya yote si kwamba Watanzania hawayaoni. Wanawaacha viongozi wa ukweli kwa makusudi kama ya watani wa jadi. Maisha hayataki utani hata kidogo. Ndiyo maana wakati mwingine taifa linaingia vitani kwa ajili ya kulinda watu pamoja na rasilimali zake.
Pengine mpaka sasa wapo wasiojua wanataka fedha au maendeleo. Wengine wanatamani kuishi kama waliopo Brunei; kumiliki majumba na magari ya kifahari kisha kula bata masaa yote siku zote. Kwani Serikali ingekuwa na fedha za kuboresha miradi, Tanzania si ingelikuwa zaidi ya Oman?
Kila kanda ingekuwa na SGR si tungeliishi vijijini mwetu na kupiga kazi mijini? Lakini ajabu mtu anataka hela ziwe mfukoni mwake tu!