Wananchi Ruangwa wamzawadia Rais Samia ng’ombe, ufuta

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kilimahewa Ruangwa mkoani Lindi leo Septemba 18, 2023.
Dar es Salaam. Wananchi wa Ruangwa mkoani Lindi wamempatia Rais Samia Suluhu Hassan zawadi mbalimbali wakati wa ziara yake katika jimbo hilo ikiwa ni shukrani yao kwake kwa kuwatembelea.
Rais Samia amepewa zawadi hizo leo Septemba 18, 2023 wakati akiendelea na ziara yake katika Kijiji cha Nandagala ambako ndiko alikozaliwa Waziri Mkuu, Kassimu majaliwa ambaye ndiyo mbunge wa Jimbo la Ruangwa.
Zawadi walizozitoa kwa Rais Samia ni pamoja na kilo 25 za ufuta, mbuzi wawili na ng’ombe mmoja.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Waziri Mkuu Majaliwa amesema zawadi hizo ni shukrani yao kwa kuwatembelea katika kijiji chao.
“Wananchi hawa wanakupa kilo chache za ufuta, kilo 25 ambazo wakati mwingine zinafaa kutafuna na mkate, unapata lishe.
“Mbili, wanakupa mbuzi wawili ili ukitaka kufuga sisi tutawapeleka mpaka Kizimkazi, hakuna shida. Lakini tatu, wametoa ngombe mmoja ili tumpeleke Kizimkazi na sisi tuko tayari kumpeleka Kizimkazi. Naomba uzipokee zawadi zetu hizo kwa niaba ya wananchi hawa,” amesema.
Akizungumza baada ya kupewa zawadi hizo, Rais Samia amewashukuru wananchi wa Ruangwa kwa zawadi walizompa na kuahidi kwamba atarudi tena Ruangwa.
“Waziri Mkuu amesema ufuta nitapaka kwenye mkate lakini sisi Wazanzibari tuna kitu kinaitwa kashata. Kwa hiyo ufuta huu nakwenda kutengeneza kashata. Watoto wanazipenda sana lakini pamoja na mimi mwenyewe, nawashukuru.
“Sisi Wazanzibari kwa ufugaji siyo wazuri, lakini tunashukuru kwa mifugo hii, nawahakikishia nakwenda kuifuga vizuri, maana yake nitatafuta wataalamu waiangalie, nawashukuru sana kwa zawadi hizi,” amesema Rais Samia.