Samia: Msiozeshe watoto, wapelekeni shule

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan ametaka wazazi wilayani Liwale wawapeleke watoto shuleni badala ya kuwaozesha.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi wilayani Liwale katika Mkoa wa Mtwara, kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wa kike badala ya kuwapeleka shuleni.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Septemba 17, 2023 alipohutubia katika mikutano wa hadhara wilayani Liwale mkoani Lindi, ikiwa ni muendelezo wa ziara zake katika mikoa ya Kusini.
Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi wilani humo, wanaamua kuwapangia watoto shughuli nyingine na kuacha kuwapeleka shule.
“Watoto mnawaficha hawaendi kuripoti shuleni, mnawapangia kazi nyingine, mnawaozesha sasa hii haitatufikisha popote,” amesema.
Ameeleza msingi wa mabadiliko ya wilaya hiyo ni uwepo wa wasomi wa kutosha na kwamba kupatikana kwao kutatokana na kupelekwa shuleni.
Rais Samia ameeleza kusikitishwa na kitendo hicho, akifafanua Serikali imekuwa ikifanya kila namna kuboresha miundombinu ya elimu lakini baadhi ya wazazi wanaamua kutowapeleka watoto kusoma.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa nchi ameahidi kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme wilayani humo.
“Tumepanga kuunganisha huduma za umeme katika mikoa hii kutoka Gridi ya Mkoa wa Ruvuma,” amesema.
Changamoto nyingine aliyoahidi kuishughulikia ni wanyama waharibifu, akisema kwa kuwa ngazi ya Wilaya na Mkoa wameshindwa, litachukuliwa kitaifa na kutatuliwa haraka.