Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyu ndiye fundi nguo aliyeshona vazi la Papa Leo XIV

Muktasari:

  • Raniero Mancinelli (86), ameshona mavazi kwa ajili ya mapapa wanne, Yohane Paulo II, Benedick XVI na Francis. Ndiye ameshona vazi la Papa Leo XIV.

Vatican. Katika mtaa tulivu wa Borgo Pio, hatua chache kutoka Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican kuna chumba kidogo chenye meza mbili za mbao, mashine ya kushonea na pasi ya zamani.

Ndani ya chumba hiki ndipo Raniero Mancinelli (86), alikata na kushona vazi kwa ajili ya Papa mpya, lililowekwa ndani ya chumba cha machozi, karibu na Kanisa dogo la Sistine, ulikofanyika uchaguzi kuanzia Mei 7, 2025.

"Ninashona mavazi matatu ya saizi tofauti, 50, 54 na 58," Mancinelli ameeleza alipozungumza na National Catholic Reporter (NCR).

"Nitawapa makardinali kabla ya kuanza kwa mkutano wa uchaguzi. Ni zawadi, kama kawaida," amesema katika mahojiano yaliyochapishwa Mei 4, 2025, siku tatu kabla ya mkutano wa kumchagua papa mpya.

Mavazi hayo matatu meupe (kanzu) yakiendana na mengine ya hariri na dhahabu, yalikuwa tayari wakati moshi mweupe ulipotoa ishara kwamba mrithi wa Papa Francis aliyefariki dunia Aprili 21, 2025 amepatikana, ambaye ni Kardinali Robert Prevost sasa Papa Leo XIV.

Akizungumza kwa kujiamini, Mancinelli amesema amekuwa akishona mavazi ya mapapa kwa zaidi ya nusu karne. Alianza kazi akiwa na miaka 15 akimsaidia baba yake.

"Nahisi kawaida. Hii imekuwa kazi yangu kwa miaka 70, naifanya kwa ari kubwa. Nafanya kazi na binti yangu na mjukuu wangu Lorenzo, mwenye miaka 23. Ni utamaduni unaoendelea," amesema.

Katika kuta za chumba kuna picha zikimwonyesha Mancinelli akiwa na mapapa aliowavisha – Yohane Paulo II, Benedick XVI na Francis.

Pasi yake nzito ya zamani, ni ileile aliyotumia tangu mwaka 1962. Mashine ya kushonea inaonekana kama kifaa cha makumbusho, lakini hutumika kutengeneza mavazi meupe kwa ajili ya tukio lenye msisimko katika maisha ya papa.


Uhusiano na Papa Francis

Alikuwa na uhusiano wa kipekee na Papa Francis tangu kitambo.

"Mkutano wetu wa kwanza siwezi kuusahau kamwe. Alikuwa mchangamfu, mwenye furaha. Tulionekana kama marafiki wa maisha yote. Nilikutana naye takribani mara tano. Alinichagua," amesema.

Ni katika duka la Mancinelli zaidi ya miaka 30 iliyopita Papa Francis alinunua msalaba wa chuma aliouvaa kifuani hadi siku ya kifo chake. Picha ya msalaba huo imechorwa juu ya kaburi lake katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu alikozikwa Aprili 26.

Jorge Mario Bergoglio (Papa Francis) aliyezaliwa Desemba 17, 1936 jijini Buenos Aires nchini Argentina alipochaguliwa kuwa Papa aliomba kuendelea kuvalishwa na Mancinelli lakini kwa ombi maalumu kwamba, mavazi yawe ya kawaida.

"Francis hakupenda vitu vya gharama kubwa. Alitaka vitambaa rahisi na vya kudumu, kama sufu nyepesi iliyochanganywa na terital (jamii ya polyester)" amesema Mancinelli.

Mtindo rahisi wa maisha wa Papa Francis ulifungua njia ya uelewa mpya wa umaridadi kama papa. Alikataa kuvaa mozzetta (vazi jekundu fupi linaloishia mabegani) usiku wa uchaguzi wake. Jioni ya Machi 13, 2013 alipochaguliwa alionekana akiwa amevaa vazi refu jeupe pekee.

Mancinelli amesema katika maandalizi ya vazi la Papa mpya alitengeneza mozzetta iwapo atataka kuvaa.

Mancinelli ameieleza NCR kwamba amewaona makardinali wawili katika siku za hivi karibuni, mmoja wa Marekani na mwingine kutoka Ulaya Mashariki, wakiwa wamevaa kanzu mpya nyekundu.

"Niliwaambia, waheshimiwa vipi kama ukawa papa? Nao walisema, 'Hapana, hakuna shida," amesema ingawa hakumbuki walikuwa nani lakini huenda kama fundi mzuri wa kazi, anabaki kuwa mtunza siri.

Katika siku za hivi karibuni, duka lake limekuwa likitembelewa na makardinali kutoka duniani kote wakitaka mavazi na vitu vingine.

Hata hivyo, Mancinelli anasema aliwakatalia akiwaeleza: "Tusubiri hadi baada ya mkutano wa uchaguzi. Sitaki mmoja wao awe Papa akiwa amevaa kitufe kipya cha dhahabu nilichoshona."

"Natumaini nitaendelea kumvalisha papa ajaye pia, kama bado sijamvalisha," amesema.

Alitabasamu aliposema haya, akionyesha mavazi ya mrithi wa Papa Francis huenda tayari yamepita mikononi mwake ikiwa ni ishara ya heshima aliyoipata kupitia miaka mingi ya huduma yake.

Anasema mmoja wa makardinali aliwahi kumwambia: “Nitakufanya waziri wa mambo ya nje wa Vatican nikichaguliwa kuwa Papa.”

Hata kama haitatimia, Mancinelli tayari ana cheo chake kikuu, fundi nguo mwenye historia.