Prime
Usiyoyajua kuhusu Papa Leo XIV, kutembelea Tanzania

Muktasari:
- Papa Leo XIV, Mmarekani wa kwanza kushika wadhifa huo, aliwahi kutembelea Tanzania aliwahi kuzuru Tanzania mwaka 2003na ana historia tajiri ya huduma ya Kanisa na mwezi Septemba umebeba siri katika maisha yake.
Dar es Salaam. Robert Prevost (69), sasa Papa Leo XIV akiwa wa kwanza kuchaguliwa kutoka Marekani na historia ya kipekee huku mwezi Septemba ukibeba siri nzito katika maisha yake.
Septemba ndio mwezi aliozaliwa Leo XIV akiwa Papa wa 267, alioteuliwa kuwa kiongozi wa shirika la Mt Augustine, alioteuliwa kuwa askofu na ndio mwezi alisimikwa kuwa kardinali.
Alizaliwa Chicago, Marekani. Baba yeke akiwa Mfaransa, Louis Prevost na mama yake Muitaliano, Mildred Martinez.

Amefanya utume wake nchini Peru kwa miaka minane akiwa askofu na miaka 20 akiwa mmisionari. Anazungumza Kiingereza, Kihispania, Kiitaliano, Kifaransa na Kireno. Anasoma Kilatini na Kijerumani.
Historia jina la kipapa Leo
Amechagua jina la kipapa, Leo, linalotokana na Kilatini likiwa na maana ya simba likiashiria nguvu na ujasiri. Ni Papa wa 14 kati ya waliochagua kutumia jina hilo.
Leo ni jina la nne kuchaguliwa na mapapa wengi, sambamba na Clement. Jina lililochaguliwa zaidi ni John likiwa la kwanza likifuata Gregory na Benedict.
Kwa zaidi ya karne moja hakujawahi kuwa na Papa aliyechagua jina la Leo, wa mwisho kuchagua jina hilo alikuwa Leo XIII, aliyezaliwa Roma wakati wa ukoloni wa Wafaransa mwaka 1810.
Alihudumu kuanzia mwaka 1878 hadi kifo chake mwaka 1903.
Katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi Mei 8, 2025 baada ya Papa kuchaguliwa, Matteo Bruni, msemaji mkuu wa ofisi ya waandishi wa habari Vatican, alizungumzia jina la Papa Leo XIV akisema: "Ni kumbukumbu ya wazi kwa mtangulizi wake Leo XIII, ambaye Mei 1891 alichapisha Waraka wa Rerum novarum, ambao mafundisho ya kijamii ya kisasa ya kanisa yanatoka humo.”

Bruni alisema jina Leo limechaguliwa kama rejea kwa wanaume na wanawake, kwa kazi zao, hata wakati wa akili mnemba, akilinganisha kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia ya sasa na ile ya karne ya 19.
Papa Leo I anayejulikana pia kama Papa Leo Mkuu alihudumu kwenye karne ya tano.
Alijulikana kwa hekima, ujasiri na mchango mkubwa katika kuimarisha mamlaka ya Kipapa katika kanisa na hata kisiasa katika Dola ya Kirumi.
Alionyesha ujasiri wakati wa uvamizi wa Mfalme wa Attila wa Hun kwa kumshawishi kusitisha uvamizi wake na kuiepusha miliki ya Roma na uharibifu.
Alikutana naye ana kwa ana na kumshawishi asivamie Mji wa Roma.
Kikao chao kilichorwa katika picha ya mwaka 1514 na Raphael. Kazi hiyo ya enzi ya Renaissance (Kipindi katika historia ya Ulaya kilichojulikana kwa kufufuliwa kwa elimu na hekima za enzi za Kale), sasa inaonyeshwa katika Jumba la Kitume la Vatican ambako makardinali 133 waliopiga kura akiwemo Kardinali Robert Prevost, sasa Leo XIV, walipita kuelekea kwenye Kanisa dogo la Sistine, Mei 7, 2025 kuanza kikao cha uchaguzi wa Papa mpya.
Katika picha hiyo, Papa Leo I asiye na silaha, akiwa chini ya uangalizi wa Mtakatifu Petro na Mtakatifu Paulo anakabiliana kwa utulivu na Attila na jeshi lake. Kikao hicho ni ishara kuwa makubaliano ya amani yanaweza kufikiwa bila kutumia vurugu.
Papa Leo I aliandika kuhusu mafundisho ya kanisa, pia alihimiza mamlaka ya Papa kama kiongozi wa kanisa lote. Aliimarisha nafasi ya Roma kama kitovu cha Ukristo, hasa nyakati ambazo udhaifu wa kifalme ulifanya kanisa kuwa nguzo ya utawala na mshikamano wa jamii.
Baada ya kifo chake, alitangazwa kuwa Mtakatifu na baadaye akapewa heshima ya kuwa mmoja wa walimu wa kanisa kwa mchango wake wa kiimani na kiutawala na baadaye viongozi 13 wa kanisa hilo wamechagua jina lake kuishi kwa kufuata nyayo zake.
Safari Tanzania
Akiwa Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino, alitembelea Vikarieti ya Tanzania ya shirika hilo.

Padri Chesco Msaga, naibu katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) akizungumza na Mwananchi leo Mei 9, 2025 amethibitisha kuhusu ziara hiyo nchini.
Askofu Robert Prevost sasa Papa Leo XIV, alitembelea nyumba za shirika hilo zilizopo Mahanje mkoani Ruvuma, Morogoro na Dar es Salaam.
Taarifa ilimbatana na picha ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza alizuru mwaka 1993 Mahanje (Ruvuma) na mwaka 2002 Morogoro, lakini Padri Msaga amesema alifanya ziara hiyo Agosti, 2003.
Wasifu wa Papa Leo XIV
Papa Leo wa XIV alizaliwa Septemba 14, 1955 katika Jimbo Kuu la Chicago, Illinois, nchini Marekani.
Alihitimu elimu ya sekondari katika seminari ndogo ya Shirika la Mtakatifu Augustino mwaka 1973. Alipata Shahada ya Sayansi ya Hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Villanova mwaka 1977.
Pia ni mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Theolojia kutoka Chuo cha Theolojia cha Kikatoliki Chicago. Alipata Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kanisa mwaka 1984 na Shahada ya Uzamivu ya Sheria za Kanisa mwaka 1987 kutoka Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas huko Roma.
Agosti 29, 1981 aliweka nadhiri za maisha kwenye Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A.
Juni 19, 1982 alipewa Daraja la Upadri na Septemba 14, 2001 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino hadi Septemba 4, 2013.
Septemba 26, 2015 hayati Papa Francis alimteua kuwa Askofu wa Jimbo la Chiclayo, nchini Peru.
Januari 30, 2023 Papa Francis alimteua kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kumpandisha cheo kuwa Askofu Mkuu na kusimikwa Aprili 12, 2023, akichukua nafasi ya Kardinali Marc Armand Ouellet, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.
Septemba 30, 2023 alisimikwa kuwa Kardinali hadi Juzi alipochaguliwa kuwa Papa.