Mfahamu Papa mpya kutoka Marekani

Muktasari:
- Ni Papa anayetajwa kufanana kimatendo na Papa Francis.
Papa Leo XIV alikuwa mwanachama wa Shirika la Mtakatifu Augustine, ambaye anaelezwa kufanana kimatendo na Papa Francis katika kujitolea kwa maskini na wahamiaji, pamoja na juhudi za kuwafikia watu mahali walipo.
Kabla ya kifo cha Papa Francis, Papa Leo XIV (Kardinali Prevost) alishika mojawapo ya nyadhifa zenye ushawishi mkubwa ndani ya Vatican, akiiongoza ofisi inayohusika na uteuzi na usimamizi wa maaskofu duniani kote.
Ni Papa ambaye aliwahi kutoa kauli maarufu akisema: “Askofu hastahili kuwa kama mfalme mdogo anayejitenga katika himaya yake, bali awe mchungaji aliye karibu na watu wake.”
Mwaka jana, aliliambia tovuti rasmi ya habari ya Vatican kuwa “askofu hastahili kuwa kama mfalme mdogo anayeketi kwenye ufalme wake.”
Licha ya kuwa na asili ya Marekani, Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 69 aliyezaliwa Chicago nchini Marekani na anayezungumza lugha kadhaa, anaonekana kama kiongozi wa Kanisa anayevuka mipaka ya kitaifa.
Alitumikia kwa miongo miwili nchini Peru, ambako alihudumu kama mmisionari, padri, mwalimu na baadaye askofu.
Huko pia alipata uraia wa nchi hiyo. Baadaye, alipanda cheo na kuongoza shirika lake la kidini katika ngazi ya kimataifa. Maisha yake mengi ameyatumia nje ya Marekani.
Alipadirishwa mwaka 1982 akiwa na umri wa miaka 27, na baadaye alipata shahada ya uzamivu katika sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas, Roma.
Akiwa kiongozi wa Waaugustino, alitembelea mashirika ya shirika hilo duniani kote, na anazungumza kwa ufasaha Kihispania na Kiitaliano.
Wengi humwelezea kama mtu mnyenyekevu, wa heshima na asiye na makelele.
Wafuasi wake wanaamini kwamba ataendeleza mchakato wa mazungumzo na ushauriano ulioanzishwa na Francis, ambao unawashirikisha waumini wa kawaida katika majadiliano na maaskofu.
Hata hivyo, haijafahamika wazi ikiwa atakuwa wazi kwa Wakatoliki wenye kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wenye mwelekeo wa jinsia mbili, na waliobadili jinsia kama alivyokuwa Papa Francis.
Ingawa hajazungumza kwa mapana juu ya suala hili hivi karibuni, katika hotuba yake kwa maaskofu mwaka 2012, alikosoa namna vyombo vya habari vya Magharibi na utamaduni wa kisasa vinavyokuza “huruma kwa imani na vitendo vinavyokinzana na Injili.”
Kama ilivyo kwa makardinali wengine wengi, naye pia amekosolewa kwa namna alivyoshughulikia madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mapadre.