Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngoma bado ngumu kumpata Papa mpya, moshi mweusi wafuka

Muktasari:

  • Moshi huo umefuka usiku Jumatano kuamkia Alhamisi Mei 8, 2025, kuashiria kuwa hakuna papa aliyechaguliwa wakati makardinali 133 walipoanza mchakato wa siri wa karne nyingi wa kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani.

Vatican. Mchakato wa kumpata Papa mpya umeanza rasmi huku moshi mweusi ukifuka juu ya Kikanisa cha Sistine saa 3:00 usiku wa Jumatano, Mei 7, 2025, kuashiria kuwa kura ya kwanza imepigwa bila kumpatikana mshindi.

Moshi huo, unaoashiria kuwa hakuna Papa mpya aliyechaguliwa, ulifuatiwa na hali ya kimya na matumaini miongoni mwa maelfu ya waumini waliokuwa wamekusanyika nje ya Kanisa hilo takatifu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya Vatican, watu takriban 45,000 wamejitokeza katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kushuhudia tukio hilo muhimu la kihistoria, wakifuatilia kwa makini kupitia TV kubwa zilizowekwa kwa ajili hiyo.

Miongoni mwa waliokuwepo ni Shemasi Nicholas Nkoronko kutoka Tanzania, ambaye amesema wito wao mkubwa kwa sasa ni sala.

“Jukumu letu hapa ni kusali na kuungana na Wakristo wengine, Wakatoliki wengine, kumwomba Roho Mtakatifu aongoze mchakato mzima,” amesema wakati wa mahojiano na Vatican News.

Muonekano wa moshi mweusi ukiwa unafuka kutoka kwenye bomba nje ya Kanisa la Sistine

Shemasi Nkoronko amesisitiza kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki anayesubiriwa na mamilioni ya waumini duniani hapaswi kuangaliwa kwa kigezo cha anatoka wapi, bali sifa ya kiroho.

“Popote anapotoka Papa mpya iwe ni Afrika, Asia, Amerika tunachohitaji ni Papa Mtakatifu. Tunahitaji Papa ambaye ataliongoza Kanisa na atakuwa mchungaji wa Kanisa,” amesema kwa msisitizo.

Mchakato wa uchaguzi huo umeanza mchana kwa ibada maalum na kuendelea kwa upigaji kura wa awamu ya kwanza jioni, ambapo makardinali 133 kutoka mataifa 70 walishiriki.

Makardinali wanatarajiwa kurejea tena ndani ya Kanisa la Sistine leo Alhamisi kwa awamu nyingine ya upigaji kura hadi pale mmoja wao atakapopata theluthi mbili ya kura zinazohitajika kuiongoza imani ya Katoliki yenye waumini bilioni 1.4 duniani.


Hali ya nje na ndani ya Sistine

Nje ya Kanisa la Sistine, Uwanja wa Mtakatifu Petro ulijaa umati wa waumini waliokusanyika kushuhudia tukio hilo la kihistoria kupitia skrini kubwa, huku wakishangilia kila hatua ya mchakato, zikiwamo milango kufungwa na moshi kuanza kufuka.

Ndani ya Sistine, hali ilikuwa ya utulivu na uzito wa kiimani, makardinali wakiwa wamevalia mavazi mekundu, wakiimba nyimbo za Kilatini na kutoa kiapo cha usiri mbele ya picha ya Michelangelo ya “Hukumu ya Mwisho”.

Makardinali wakiwa ndani ya Kanisa la Sistine katika mchakato wa kumchagua Papa mpya wa Kanisa Katoliki.

Askofu Mkuu Diego Ravelli, msimamizi wa ibada za kipapa, aliamuru “extra omnes” – yaani, watu wote wasiostahili wakae nje kabla ya lango kufungwa na mchakato kuanza rasmi.


Matarajio ya waumini

“Natumaini makardinali watachagua mtu ambaye ni mpatanishi na ataunganisha Kanisa tena,” alisema Gabriel Capry (27), kijana kutoka London aliyekuwepo kwenye uwanja huo.

Mtalii Lisette Herrera kutoka Jamhuri ya Dominika alisema: “Ninamsihi Roho Mtakatifu atupe papa kijana atakayekaa nasi kwa muda mrefu.”


Shinikizo na changamoto

Ingawa makardinali wanapaswa kuepuka ushawishi wa kidunia, mikakati mbalimbali ya kushawishi ilionekana Roma kabla ya mkutano. Vijana Wakatoliki waliandika barua ya wazi, vyombo vya habari vya kihafidhina vikatoa tathmini za wagombea, na watetezi wa upadrisho wa wanawake walirusha moshi wa rangi ya waridi kutuma ujumbe wao.

Muonekano wa moshi mweusi ukiwa unafuka kutoka kwenye bomba nje ya Kanisa la Sistine

Rais wa Marekani, Donald Trump, naye alivutia hisia alipopigwa picha akiwa amevaa kama Papa kitendo kilicholaaniwa na wanasiasa wakongwe wa Ulaya kama kuingilia imani isivyofaa.

Kwa upande wa changamoto, Papa mpya anatarajiwa kukabiliana na masuala nyeti kama nafasi ya wanawake katika Kanisa, haki za watu wa LGBTQ+, wakimbizi, na kashfa ya unyanyasaji wa kingono. Swali kubwa kwa makardinali ni kama wataendeleza urithi wa mageuzi wa Francis au kuirejesha hali ya kihafidhina ili kuleta umoja katika Kanisa.


Majina yanayojitokeza

Wagombea wanaopewa nafasi kubwa ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin (Italia), ambaye ni Katibu wa Vatican, Kardinali Luis Tagle (Ufilipino), anayesifiwa kwa uongozi wake wa kiuinjilishaji barani Asia, na Kardinali Peter Erdo (Hungary), anayewakilisha msimamo wa kihafidhina.

Kwa mujibu wa historia, uchaguzi wa papa huwa unachukua kati ya awamu tatu hadi 14 za kupiga kura. Papa Francis mwenyewe alichaguliwa katika awamu ya tano mwaka 2013.

Makardinali wanatarajiwa kurejea Sistine Alhamisi asubuhi kuendelea na upigaji kura hadi pale watakapompata papa wa 267 wa Kanisa Katoliki duniani.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.