Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawasiliano ya simu yazimwa Vatican uchaguzi wa Papa mpya

Muktasari:

  • Mchakato wa kumchagua Papa mpya umeanza kwa misa leo Mei 7, 2025.

Vatican. Mchakato wa kumpata Papa mpya ukianza leo Jumatano Mei 7, 2025 kwa misa, mawasiliano yote kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii yatazimwa mjini Vatican.

Uchaguzi unafanyika kufuatia kifo cha Papa Francis kilichotokea Aprili 21 akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta, Vatican.

Kwa mujibu wa andiko la Padri Richard Mjigwa kupitia mtandao wa Vatican News, kuanzia leo Mei 7, saa 9:00 alasiri kwa saa za Ulaya (sawa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati) mawasiliano yote kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii yatazimwa mjini Vatican na yatarudishwa wakati wa kumtangaza Papa mpya wa 267.

Baraza la Makardinali, katika mkutano wa tano uliofanyika 28 Aprili 28, liliamua mchakato wa uchaguzi kumpata Papa mpya uanze rasmi leo Mei 7, 2025.

Kuna jumla ya makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura lakini wanaoshiriki ni 133, wakiwamo kutoka nchi 15 wanaoshiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Papa.

Padri Mjigwa ameandika kwa kadiri ya Katiba ya Kitume ya “Universi Dominici Gregis” iliyotungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II Februari 22, 1996 idadi ya makardinali wanaopaswa kupiga au kupigiwa kura ni 120 lakini imekuwa ikizidi mara zote.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ameongoza misa kwa ajili ya uchaguzi huo.

Katika mahubiri amesisitiza imani, matumaini na mapendo thabiti ili kuomba nguvu za Roho Mtakatifu kwa makardinali kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu, ustawi, maendeleo na mafao ya kanisa na binadamu katika ujumla wake.

Waamini katika sala ya kuombea uchaguzi wamesali kumuomba Mungu alilinde Kanisa katika ukweli, umoja na amani; awajalie makardinali roho wa akili, shauri, heshima na mang’amuzi, haki, mshikamano na maridhiano.

Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi limewaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho na kusikiliza mapenzi ya Mungu.

Padri Mjigwa ameandika: “Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati, tayari kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu wa Mungu.”

Kanisa linamhitaji Papa atakayeamsha dhamiri za watu wa Mungu: Kimaadili, kiroho na kijamii katika ulimwengu mamboleo ambao una maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini unaotaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vyake.

Ameandika Papa ajaye awe daraja na mwongozo katika mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya watu wa Mungu.

“Ni kiongozi anayepaswa kuwa shuhuda wa imani, atakayesimama kidete kulinda na kutetea: haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, tayari kuchochea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, miito mitakatifu ndani ya kanisa, elimu, malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya.”

Makardinali wako kwenye kanisa dogo la Sistine, tayari kuanza mkutano wa uchaguzi wa Papa mpya, huku waamini wakialikwa kufunga na kusali kuombea ufanisi katika uchaguzi huo.

Taarifa ya Vatican ilisema makardinali wote watakuwa katika nyumba ya Mtakatifu Marta na nyingine ya zamani ya Mtakatifu Marta mjini Vatican.

Makardinali wapigakura watasafiri kutoka nyumba ya Mtakatifu Marta kwenda kwenye kanisa dogo la Sistine kama wanavyotaka, hata kwa miguu, lakini kwa njia inayolindwa.

Kanisa dogo la Sistine ndiko makardinali watajifungia kwa ajili ya kumchagua Papa mpya. Tayari kumewekwa ulinzi eneo hilo.