Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bunge lagomea utaratibu ajira JWTZ, Spika Tulia atoa maagizo

Muktasari:

  • Kwa mara nyingine hoja ya kigezo cha ajira ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa wamepita Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeibua tena bungeni na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutoa maagizo serikalini.

Dodoma. Tangazo la nafasi za ajira kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limezua mvutano bungeni ikitajwa kuwa chombo hicho kimekiuka maagizo ya Bunge kwa kuweka kigezo cha waombaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kutokana na hilo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameagiza Serikali kupeleka majibu bungeni ni kwa nini wameweka tangazo ambalo linakwenda kinyume na maazimio yaliyotolewa na Bunge.

Spika wa Bunge, Tulia Ackson

April 30, 2025, JWTZ kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano, Kanali Gaudentius Ilonda walitangaza nafasi za ajira kwa vijana wenye taaluma mbalimbali lakini katika kipengele ‘f’ waliweka kigezo cha ulazima wa muhusika kuwa amepitia JKT kwa kujitolea au kwa mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti.

Ajira hizo kwa vijana wenye elimu ya sekondari hadi elimu ya juu ni kwa vijana wataalamu wa tiba ikiwemo madaktari waliobobea katika fani za daktari wa upasuaji,  daktari wa upasuaji wa mifupa na viungo, wa magonjwa ya kibofu na njia ya mkojo, mtaalamu wa kusoma picha za magonjwa kama za X-ray, MRI, CT,  wa masikio, pua na koo, daktari wa usingizi, wa magonjwa ya ndani, wa macho,  wa saratani.

Wengine ni madaktari wa uchunguzi wa sampuli za mwili kwa ajili ya upimaji  wa magonjwa, wa magonjwa ya akili, wa huduma za dharura, wa magonjwa ya damu, wa tiba za wanyama, mhandisi wa tiba na vifaatiba,  taalamu wa maabara ya meno na daktari wa afya za abiria na wahudumu wa anga. 

Kanali Ilonda ametaja taratibu za kutuma maombi kuwa yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe makao makuu ya jeshi hilo jijini Dodoma kuanzia Mei Mosi hadi Mei 14,2025.

Leo Mei 8, 2025 Mbunge wa Mbozi (CCM), George Mwenisongole ameomba mwongozo wa Spika akitaka kujua ni namna gani JWTZ wamekiuka Azimio la Bunge kwenye nafasi hizo wakiweka kigezo cha JKT tena.

“Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilisimama hapa na kuomba mwongozo wa Spika kuhusu kigezo cha kutaka watu wanaotaka kuajiriwa kwenye vyombo vya ulinzi lazima wawe wamepita mafunzo ya JKT, leo tena JWTZ wamerudia kwenye mambo hayo, naomba mwongozo wako,” amesema Mwenisongole.

Mbunge wa mbozi George Mwenisongole

Spika amemsimamisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Uratibu, William Lukuvi huku akimpa nakala ya tangazo hilo ambapo Waziri Lukuvi amekiri Bunge lilipitisha Azimio hilo lakini halikulenga moja kwa moja kwenye ajira za JWTZ.

“Hili linaleta ukakasi, mbunge ameomba mwongozo lakini tulishalipitisha hapa na Serikali ilikuwepo, leo inapotolewa kigezo hiki kinakwenda kinyume na Azimio la Bunge, kama chombo kinataka waajiriwa wake wapitie JKT si wawaajiri halafu wawapeleke wenyewe JKT,” amesema Dk Tulia.


Hoja ilikoanzia

Februari 16, 2024 Mbunge George Mwanisongole aliibua hoja ambapo wakati huko kulikuwa na tangazo la nafasi za ajira kwa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama ambao baadhi waliweka kigezo cha wasailiwa kuwa wamepitia JKT na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Katika hoja hiyo kuliibua mjadala mkali wa wabunge na mawaziri uliohitimishwa kwa Bunge kupitisha azimio la kuondoa kigezo cha kupitia mafunzo ya JKT na JKU.

Mwanisongole katika mwongozo huo alisema wako maelfu ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne na sita nchini ambao wanataka kupata nafasi za ajira kwenye vyombo hivyo, lakini hawakuwa na sifa za kujiunga na JKT kwa hiyo wanakosa nafasi.

“Wanaopata nafasi ni wachache na hao ndiyo ambao wanapata nafasi ya kuomba ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, naomba kutoa hoja kigezo hiki kiondolewe na mchakato wa ajira unaoendelea usimame,” alisema Mwenesongole.

Wabunge waliochangia hoja hiyo na kuunda Azimio walikuwa ni Rashid Shangazi (Mlalo), Hamisi Tabasamu (Sengerema), Luhaga Mpina (Kisesa), Husna Sekiboko, Dk Christian Mzava na Agnes Marwa.

Mawaziri waliochangia walikuwa Jumanne Sagini (Naibu Waziri mambo ya Ndani wakati huo sasa ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria), Innocent Bashungwa (Waziri wa Ujenzi sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Dk Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi.

Mwisho wa mjadala Bunge limeazimia vijana wote wapewe fursa sawa za ajira pale wanapokuwa wametimiza masharti mengine yote yanayohusika na nafasi ya ajira husika isipokuwa cheti cha JKT na JKU.

Dk Tulia amesema Serikali ifanye hivyo hadi pale  itakapokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwapa mafunzo ya JKT na JKU vijana wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.

Ametaja sababu tatu ambazo zimewafanya kufikia maamuzi hayo kuwa ni JKT na JKU kutokuwa na uwezo wa kuwapokea na kuwafundisha vijana wote wanaohitimu kidato cha nne na cha sita.

Sababu nyingine ni uwepo wa uwezekano wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwapeleka katika mafunzo hayo watakaokuwa wameajiriwa kwa kuzingatia masharti ya msingi ya ajira husika.

Ametaja sababu nyingine ni uwepo wa vijana wenye uwezo wa kutimiza masharti ya ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama isipokuwa sharti la kupitia mafunzo hayo.