Prime
Mahakama ya kijeshi yaagiza kesi mauaji ya askari JWTZ isikilizwe upya

Muktasari:
- Yabaini dosari hukumu mahakama ya kijeshi. Risasi nne za SMG zilifyatuka na kuua. Ni kutoka kwenye bunduki ya marehemu
Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani ya Mahakama ya Kijeshi (Court Martial Appeal Court) imeamuru kusikilizwa upya kwa shauri la kuua bila kukusudia linalomkabili Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mahakama hiyo inayoundwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa shauri hilo, zilizofanywa na Mahakama Kuu ya Kijeshi (GCM), iliyoketi katika kamandi ya Jeshi la nchi Kavu, Kibaha mkoani Pwani 2023.
Wainng’ari alitiwa hatiani kwa kosa la kusababisha kwa uzembe, kifo cha askari mwenzake wa JWTZ, Daud Mbwana, wakiwa Beni Mavivi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Machi 23 mwaka 2021.
Ilidaiwa siku ya tukio, mrufani akiwa katika majukumu ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa (UN), yeye na Private Daud Mbwana, alikuwa anajaribu kuiweka vizuri silaha ya Private Daud iliyokuwa imewekwa vibaya kiusalama.
Pasi na kukusudia, alisababisha kufyatuka kwa risasi nne za silaha aina ya Sub Machine Gun (SMG) ambapo kati ya risasi hizo, mbili zilimpiga eneo la mgongoni na moja ilimpiga eneo la kichwani na kusababisha kifo cha Private Mbwana.
Aliposomewa mashitaka hayo mrufani alikanusha, ambapo kesi ilikwenda katika hatua ya usikilizwaji kamili ambapo Jenerali wakili wa Mahakama wa Jamhuri katika mahakama ya kijeshi aliita mashahidi 11 na kutoa vielelezo 15.
Mei 12, 2023 upande wa utetezi uliwasilisha hoja za mwisho na kueleza mteja wake alikuwa hana kesi ya kujibu, lakini baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande zote mbili, Mahakama iliona ana kesi ya kujibu hivyo kutakiwa kujitetea.
Hata hivyo, kabla upande wa utetezi haujaanza uwasilishaji, upande wa Jamhuri uliwasilisha ombi la kutaka kufanya marekebisho katika hati ya mashitaka kwa kuingiza neno “kwa uzembe” ili kosa liwe la kusababisha kifo kwa uzembe.
Baada ya kusikiliza pande mbili, Juni 19, 2023 Mahakama hiyo ilieleza ombi hilo ni moja ya kasoro ya kiufundi na kwa kuzingatia sheria ya nidhamu jeshini, haitaathiri haki ya mshtakiwa hivyo kuamuru maneno hayo yaingizwe.
Hii ni baada ya kufyatuka kwa risasi nne katika bunduki aliyokuwa na kusababisha kifo cha Mbwana na baada ya Mahakama ya Kijeshi kusikiliza pande mbili za shauri hilo, ilimtia hatiani ofisa huyo na kuamuru afukuzwe kazi jeshini.
Hata hivyo hakuridhishwa na uamuzi huo, hivyo akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ya Kijeshi dhidi ya Mashauri wa Mahakama Kuu ya Kijeshi (Judge Advocate General -JAG) akipinga uamuzi huo.
Mahakama ya Rufani ya Kijeshi katika hukumu yake iliyoitoa Machi 28, 2025, imekubaliana na rufaa hiyo na kuamuru kesi isikilizwe upya.
Hoja za kisheria kortini
Katika rufaa hiyo, mrufani aliwakilishwa na wakili kanali mstaafu wa Jeshi, Godwin Banda wakati mjibu rufaa, JAG, akiwakilishwa na Kanali Kasamawe na Luteni Deogratius Mwakapimbila.
Akijenga hoja za rufaa, wakili Banda alisema kutiwa hatiani na adhabu aliyopewa mteja wake iliegemea katika hati ya mashitaka iliyokuwa na dosari za kisheria na hiyo inatokana na marekebisho ya hati ya mashitaka yaliyofanyika Juni 19, 2023.
Alieleza kuwa marekebisho hayo yalifanyika pasipokuwepo mamlaka au nguvu yoyote ya kisheria kwani ilitakiwa kuwepo na suala jipya, kupitishwa kwa hati mpya ikiwa na majina na saini ya mtu au mamlaka iliyorekebisha.
Mbali na hoja hiyo, alieleza kuwa GCM ilishindwa kufahamu kuwa taarifa za kosa hilo zilizokuwepo kwenye hati halisi ya mashitaka, haikuwa imebainishwa kosa la mauaji ya bila kukusudia kwa uzembe chini ya kifungu 195(1) na (2) sura ya 16.
Kwa mujibu wa wakili Banda, ushahidi wa Jamhuri uliopokelewa katika Mahakama hiyo ya Kijeshi ulikuwa unajaribu kuthibitisha tuhuma dhidi ya mrufani zilizopo katika hati ya mashitaka, kabla kurekebishwa baada ya Jamhuri kufunga kesi yake.
Wakili huyo alisema marekebisho hayo ya hati ya mashitaka yalikuja kama wazo la baada ya wasilisho la mrufani kuwa hati ya mashitaka ilikuwa haibainishi kosa la kuua bila kukusudia kwa mujibu wa sheria za nchi.
Pia akasema GCM iliyosikiliza shauri hilo ilishindwa kubaini kuwa ushahidi wa upande wa Jamhuri haukuthibitisha shitaka la kuua bila kukusudia kwa uzembe.
Alieleza kuwa upande wa Jamhuri haukuwa umewasilisha ushahidi kuonyesha kuwa mrufani alifanya kwa uzembe katika kutenda kosa analoshtakiwa nalo, na uliingiza taarifa ya kosa jipya ambalo silo Jamhuri iliwasilishwa ushahidi wake.
Mbali na dosari hiyo, lakini mrufani hakupewa fursa ya kukiri au kukanusha shitaka hilo jipya na hakuna shahidi wa Jamhuri aliyeitwa tena, ili kudodoswa na mrufani kuhusiana na taarifa hiyo mpya ya mashitaka.
Kwa upande wao, mawakili waliowakilisha upande wa Jamhuri, walisema hati ya mashitaka ilifanyiwa marekebisho kwa kuingiza neno “kwa uzembe” baada ya majadiliano ya pande mbili katika shauri hilo mbele ya Mahakama ya Kijeshi.
Walijenga hoja kuwa mshitakiwa katika kesi hiyo alielewa uasili wa mashitaka yanayomkabili baada ya marekebisho hayo na hayakuathiri mzizi wa shitaka, na inathibitishwa na kauli yake kuwa yuko tayari kujitetea.
Walisema hitimisho la Mahakama ya Kijeshi na adhabu iliyotolewa, haiwezi kuwa batili kwa sababu tu ya kupotoka kwa utaratibu uliowekwa katika udhibiti wa vikosi vya ulinzi, labda tu kama hiyo itakuwa imesababisha haki kutotendeka.
Mawakili wa Jamhuri walipinga hoja ya mrufani kuwa mauaji yaliyotokea hayaangukii katika kosa la kuua bila kudhamiria na kusisitiza kuua bila kukusudia kunatofautishwa na kuua kwa kukusudia kwa kukosekana nia ya kuua au kudhuru.
Walisema pale inapoonekana hati ya mashitaka ina dosari na inaweza kuathiri mwenendo wa kesi, sheria inatoa mwanya wa kuifanyia marekebisho ili kutibu dosari inayoonekana na kusema rais wa Mahakama ya Kijeshi ana mamlaka hayo.
Kwa mujibu wa mawakili hao, ombi la kufanya marekebisho hayo ilitokana na kubainika kukosekana kwa neno “kwa uzembe” kwa vile kosa lilitendeka kwa kumuua Daud Mbwana Ally bila uhalali na pia kutokana na uzembe.
Hukumu ya jopo la majaji
Katika hukumu yao, majaji Obadia Bwegoge, David Ngunyale na Arnold Kirekiano walisema utaratibu wa kurekebisha hati ya mashitaka unataka kama mshtakiwa ataomba ahirisho ili kusomewa hati mpya ya mashitaka, aruhusiwe na mahakama.
Lakini wakasema ni takwa la kisheria kuwa marekebisho hayo ni lazima yaidhinishwe katika hati ya mashitaka na kusainiwa na rais wa Mahakama ya Kijeshi na ikifanyika hivyo itachukuliwa kuwa ni hati halisi ya mashitaka.
Majaji hao walisema katika rufaa iliyo mbele yao, marekebisho ya hati ya mashitaka yalifanywa baada ya upande wa mashitaka kufunga kesi yao na kwa namna ilivyofanyika, mrufani hakupewa nafasi ya kuhoji mashahidi upya.
Kulingana na majaji hao, malalamiko ya mrufani ni kuwa taarifa mpya ya “kwa uzembe,” iliyoingizwa katika hati ya mashitaka ilikuwa ni tuhuma na wao (majaji) wanakubaliana na mrufani kuwa alitakiwa asomewe upya na kukiri au kukana.
Majaji hao walisema marekebisho hayo hayakupaswa kufanywa baada ya upande wa mashitaka kufunga kesi yao na sababu ni kuwa mshtakiwa hawezi kuwasilisha utetezi wake kwa kesi ambayo hati ni tofauti na iliyomuona ana kesi ya kujibu.
“Usikilizwaji wa kesi ulidhoofika kuanzia tarehe ambayo marekebisho yalifanyika kwenye hati ya mashitaka. Marekebisho ya hati ya mashitaka baada ya uamuzi wa mrufani ana kesi ya kujibu, utetezi na hukumu vyote ni badili na vinafutwa”
Majaji hao walisema baada ya kuzingatia namna mwenendo huo wa shauri ulivyopotoka, wameridhika kuwa haki inataka kesi hiyo isikilizwe upya na hivyo wanaagiza isikilizwe upya kuanzia pale ambapo mrufani ana kesi ya kujibu.