Wito kwa waamini kusali kuelekea uchaguzi wa Papa mpya

Muktasari:
- Chumba kilichokuwa kinatumiwa na hayati Papa Francis kitafunguliwa baada ya uchaguzi wa Papa mpya.
Vatican. Baraza la Makardinali katika mikutano elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Papa mpya linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho na kusikiliza mapenzi ya Mungu.
Uchaguzi wa Papa mpya unafanyika kesho Mei 7, 2025 kufuatia kifo cha Papa Francis kilichotokea Aprili 21.
Katika andiko lililochapishwa kwenye mtandao wa Vatican News, makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini.
Amesema makardinali wenyewe wanapenda kujinyenyekesha ili waweze kuwa vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo.
Baada ya maadhimisho ya misa kwa ajili ya uchaguzi wa Papa mpya, Mei 7, Padri Mjigwa amesema makardinali watatakiwa kuhamia kwenye nyumba ya Mtakatifu Martha ambako watalala.
Katika nyumba hiyo, amesema chumba kilichokuwa kinatumiwa na hayati Papa Francis kitafunguliwa baada ya uchaguzi wa Papa mpya.
Kwa mujibu wa utaratibu wa kanisa, baada ya kifo cha Papa Francis chumba hicho kilifungwa.
Amesema mchakato wa upigaji kura utakuwa mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni.
Andiko hilo linaeleza kuwa Kardinali John Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi na Kardinali Antonio Cañizares, ambaye ni Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Valencia, Hispania ni kati ya makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao hawatashiriki uchaguzi wa Papa mpya.
Taarifa ya Vatican imesema makardinali katika mkutano wao wa 10 uliofanyika Mei 5, 2025 walikuwa na mijadala iliyohusu hali ya kanisa na matumaini yao ya siku zijazo.
Msemaji mkuu wa ofisi ya waandishi wa habari ya Vatican, Dk Matteo Bruni aliwaeleza wanahabari Jumatatu Mei 5 kwamba makardinali 179, wakiwamo 132 wapigakura walishiriki mkutano huo.
Katika taarifa alibainisha makardinali wote 133 ambao ni wapigakura wapo mjini Roma.
Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, aliliambia Baraza la Makardinali kwamba, Kardinali Camerlengo, Kevin Farrell, walipiga kura Jumamosi Mei 3, kwa ajili ya shughuli za vyumba vya makardinali ambako watalala ikielezwa wanaweza kuanza kuingia vyumbani kuanzia asubuhi ya leo Jumanne Mei 6.
“Wote watakuwa katika nyumba ya Mtakatifu Marta na ile ya zamani ya Mtakatifu Marta mjini Vatican,” imeeleza taarifa hiyo.
Makardinali wapigakura wataweza kusafiri kutoka nyumba ya Mtakatifu Marta kwenda kwenye kanisa dogo la Sistine kama wanavyotaka, hata kwa miguu, lakini kwa njia inayolindwa.
Kanisa dogo la Sistine ndiko makardinali watajifungia kwa ajili ya kumchagua Papa mpya. Tayari kumewekwa ulinzi eneo hilo.
Taarifa hiyo imeeleza maadhimisho yote wakati wa uchaguzi wa Papa mpya yatafanyika kwa lugha ya Kilatini. Baraza la Makardinali katika mikutano yake, limesema linatambua mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu ya kiroho na kimwili.
Wamegusia kashfa ya manyanyaso kijinsia ndani ya kanisa na masuala ya vitega uchumi vya Vatican kuwa ni madonda yanayohitaji uponyaji wa haraka.
Imeeleza liturujia ya kanisa, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi la Kimisionari na utekelezaji wa sheria za kanisa ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na vipaumbele vya kanisa katika mapambazuko ya milenia ya tatu ya Ukristo.
Baraza la Makardinali katika kikao cha Aprili 30, 2025 pamoja na mambo mengine, kilijadili kuhusu hali ya uchumi ilivyo mjini Vatican na changamoto zake ili kuendelea kuimarisha mfumo wa uchumi utakaoenzi utume wa Papa sehemu mbalimbali za dunia.
Pia sera na mikakati ya vitega uchumi vya Vatican, hali ya kifedha ya Benki Kuu ya Vatican (IOR) iliyoanzishwa mwaka 1942 na Papa Pio XII.
Benki hiyo inajihusisha na huduma kwa mashirika ya kitawa, kazi za kitume na shughuli za uinjilishaji unaofanywa na kanisa duniani.