Prime
KESI YA LISSU: Hakimu atoa onyo, Lissu agomea tena mtandao

Muktasari:
- Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini, tukio analodaiwa kulitenda Aprili 3, 2025 ndani ya Tanzania.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelekeza upande wa mashitaka kukamilisha haraka upelelezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Pia imeelekeza tarehe ijayo, upande wa mashitaka uje uieleze Mahakama hiyo upelelezi wa kesi hiyo umefikia hatua gani.
Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga ametoa maelekezo hayo, leo Jumanne Mei 6, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa njia ya video.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.
Hakimu Kiswaga amefikia hatua hiyo, baada ya upande wa mashitaka kuieleza mahakama hiyo upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Awali, jopo la mawakili wanne wa Serikali wakiongozwa na Tawab Issa, Job Mrema, Cathbert Mbiling'i na Harrson Lukosi, umedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na wanaomba kujua iwapo mshtakiwa amefikishwa mahakamani kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao.
Wakili Tawab baada ya kuuliza swali hilo, Kamishna Msaidizi wa Magereza (CPA), Juma Mwaibako ambaye pia ni Mkuu wa Gereza la Ukonga, ameieleza Mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa amejulishwa aende katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kusikiliza kesi yake kwa njia mtandao, lakini amesema hawezi kwenda kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao
"Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa tumemjulisha anatakiwa kwenda sehemu ambayo imetengwa kwa ajili ya kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao, lakini amesema hawezi kwenda kusikiliza kesi yake kwa njia ya mtandao," amedai CPA Mwaibako.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akiwa ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Mtandao
Hakimu Kiswaga baada ya kupewa taarifa hiyo, aliuliza upande wa mashitaka hatua ya kesi hiyo, ambapo upande wa mashitaka umedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
"Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika mheshimiwa hakimu, hivyo tunaomba Mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Tawab.
Tawab baada ya kutoa taarifa, Wakili wa upande wa mashitaka, Mpare Mpoki amehoji upelelezi kutokukamilika huku kesi hiyo ikiwa imefikisha siku 27.
"Mheshimiwa hakimu, tunashangaa kwa nini upelelezi wa kesi hii unachukua muda mrefu kukamilika," amedai Mpoki.
"Mteja wetu ana haki ya kusikilizwa kesi yake kwa haraka ili haki iweze kutendeka, sasa ni kitu gani kinakwamisha upelelezi kutokukamilika kwa wakati? Tunaomba wenzetu watuambie upelelezi umefikia hatua gani,” amehoji Mpoki.
Mpoki amedai shitaka aliloshtakiwa mteja wake adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa, hivyo kama upande wa mashitaka hawana karatasi za kuandikia maelezo ya mashahidi na vielelezo waseme ili wapewe.
Akijibu hoja hizo, wakili Tawab amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na ukikamilika wataambiwa na wataandaa nyaraka na kuzipandisha mtandaoni.
Tawab baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Kiswaga amemkumbusha kuwa upande wa utetezi wanataka kujua upelelezi umefikia hatua gani.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.
Tawab amedai bado wanaendelea na upelelezi kwa sababu kesi hiyo ni kubwa na hawawezi kueleza upelelezi wao wanafanya katika eneo gani.
"Upelelezi wa kesi hii haujakamilika na hakuna sheria yoyote tuliyokiuka, hivyo tukikamilisha tutawapa taarifa, lakini sheria haitulazimishi kuseme upelelezi umefikia hatua gani," amedai Tawab.
Baada ya majibu hayo ya Serikali, Mpoki amehoji upelelezi huo utakamilika lini kwa sababu wao wanashughulika na maisha ya mtu (Lissu) kwa sababu hati ya mashitaka wana maneno yaliyosemwa na Lissu, hivyo haoni sababu ya upelelezi kuchelewa kukamilika.
Akijibu swali hilo, Tawab ameomba upande wa utetezi kutumia lugha nzuri.
"Mheshimiwa hakimu, sisi tunasema upelelezi wa kesi hiyo na taarifa za kujua upelelezi umefikia wapi hatuwezi kuzisema, pia lugha waliyotumia kuwa hatuna karatasi za kuandaa nyaraka sio lugha nzuri, wasilete ushabiki hapa mahakamani, hivyo watumie lugha nzuri," amesema Tawab.
Hata hivyo, hakimu Kiswaga ameingilia kati malumbano hayo na kueleza mawakili watumie lugha nzuri kwa kuwa kesi hiyo inasikilizwa na watu wengi.
"Pande zote mbili nyinyi ni maofisa wa mahakama, hakikisheni mnatumia lugha nzuri kwa sababu watu wanatufuatilia kwenye mtandao," ameelekeza hakimu Kiswaga.
Kiswaga baada ya kutoa onyo hilo, mwakili wa pande zote mbili walikubaliana kutumia lugha nzuri.
Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alitoa maelekezo mawili ambayo ni: "Natoa wito kwa upande wa mashitaka kuhakikisha mnakamilisha upelelezi kwa haraka na pia tarehe ijayo, mje mtuambie upelelezi wa kesi hii umefikia hatua gani."
Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 19, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya mtandao ambapo luninga mbili zilizofungwa kwenye ukumbi huo zilionesha mawakili wa Serikali wakiwa ofisini kwao, mawakili wa utetezi walikuwepo ukumbi wa video uliopo Mahakama ya Kisutu pamoja na hakimu naye alikuwepo katika ukumbi huo, huku luninga nyingine ukionesha eneo maalumu lililotengwa gerezani kwa ajili mahabusu kusikiliza kesi zao.
Kwa mara ya kwanza, Lissu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, 2025 akikabiliwa na shitaka moja la uhaini.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuandika maeneo yafuatayo
"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko..., kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."