Prime
Mbinu mpya ya Polisi Kisutu

Muktasari:
- Kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa hatua tofautitofauti.
Dar es Salaam. Wakati kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu zikiendelea leo Jumanne, Mei 6, 2025, askari wa Jeshi la Polisi wametanda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na maeneo ya jirani.
Kwa siku ya leo kwenye viunga vya Mahakama hiyo kunaonekana hakuna hekaheka ikilinganishwa na Aprili 24 na Aprili 28, 2025, Jeshi la Polisi limekuja na mtindo mpya ambapo magari ni machache ikilinganishwa na siku nyingine lakini idadi ya askari wanaofanya doria kwa farasi na miguu kuzunguka karibu na mahakama hiyo ni kubwa zaidi.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.
Wakimkuta raia amesimama kwa muda awe anaongea na simu anaulizwa maswali kujua anataka kwenda wapi? wakijua au akishindwa kujieleza kwa ufasaha basi anaamriwa kuondoka katika eneo hilo mara moja.
Lissu anakabiliwa na kesi mbili tofauti ya jinai ambapo shitaka moja ni la uhai na nyingine akikabiliwa na mashitaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Ikumbukwe baada ya viongozi wa Chadema kuwahamasisha wananchi kuhudhuria mahakamani hapo Aprili 24, 2025 kusikiliza kesi ya mwenyekiti wao, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilipiga marufuku kusanyiko lolote karibu na eneo la Mahakama.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.
Upigaji marufuku huo ulijengwa na hoja kuwa Mahakama hiyo inahitaji utulivu kwani, kuna kesi nyingi zinazopaswa kusikilizwa zaidi ya ile inayomkabili kiongozi huyo na zinapazwa kupewa uzito uleule.
Majibu ambayo yalikuwa yanapata ukinzani dhidi ya viongozi wa Chadema na mawakili wanaosimamia kesi hiyo kwa hoja tofauti, ikiwemo ile waliyodai Lissu ni kiongozi na ameshika nafasi mbalimbali, hivyo hadhi yake ni tofauti na wengine lakini hata mashitaka yanayomkabili watu lazima wasikilize ili wajue.
Leo Mei 6, 2025 Jeshi la Polisi lipo mahakamani hapo na linaendelea na mbinu ya kutumia farasi kufanya doria kutembea kwa miguu kuzunguka eneo la Mahakama na kuwatimua walioketi jirani na Mahakama hiyo.
Pia wapo askari wengine waliotulia kwenye baadhi ya magari yaliyopo mahakamani hapo katika kila kona ya kufika Kisutu ikiwemo Mnazi Mmoja, mkabala na Hoteli ya Serena, barabara ya kuelekea hoteli ya Holiday Inn pamoja na eneo la Chuo Cha Biashara Dar es Salaam (CBE).
Wakati askari hao wakiwa maeneo hayo hakuna mwananchi anayeruhusiwa kuingia mahakamani hapo kama sio mwandishi wa habari.
Ndani ya Mahakama hiyo yapo magari mawili yenye askari ambao nao wanafanya doria ndani ya mahakama na kuna waliosimama kwenye geti kubwa la kuingia mahakamani hapo.
Mwananchi imezungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema- Bara, Aman Golugwa kutaka kujua kwa nini makada wa chama hicho hawajajitokeza kwa wingi ikilinganishwa na siku zilizopita.
Golugwa amesema wamejitokeza kiasi na wamevaa nguo za kirai lakini wameshindwa kujitokeza kwa wingi kwa kuwa wanasubiri uamuzi utolewe na Mahakama, kama kesi hiyo itasikilizwa kwa njia mtandao au laa.

Askari Polisi wakiimarisha ulinzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam leo Jumane, Mei 6, 2025.
"Wengi wanasubiri uamuzi ndiyo maana hakuna hekaheka kama siku zilizopita. Unajua tuliweka pingamizi sasa leo Mahakama inatoa majibu. Ingawa msimamo wetu tunaungana na mwenyekiti hatutaki mashitaka yake yafanyike kwa njia mtandao," amesema
Amesema iwapo Mahakama hiyo itakuja na msimamo wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwa mtandao, mwenyekiti wao atagomea kula gerezani na wao kama wanachama watamuunga mkono hadi haki itendeke.
Endelea kufuatilia Mwananchi