Rais Samia amteua Twange kuwa bosi mpya wa Tanesco

Muktasari:
- Mbali na uteuzi huo Rais Samia amemteua Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kufanya mabadiliko ya vituo vya kazi vya baadhi ya wakuu wa Wilaya.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemteua Lazaro Twange kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Twange aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo amechukua nafasi ya Gissima Nyamo-Hanga ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 13, 2025 katika ajali ya gari iliyotolea wilayani Bunda, mkoani Mara.
Bosi huyo mpya ana anachukua nafasi ya kuliongoza shirika hilo linalojishughulisha uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme.
Uteuzi wa wake umetangazwa leo Jumanne Mei 6, 2025, kupitia taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, iliyosainiwa na Mkurugenzi wake, Sharifa Nyanga.
Mbali na uteuzi huo kwa mujibu wa taarifa hiyo Rais Samia pia amemteua Andrew William Massawe kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), akichukua nafasi ya Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman aliyemaliza muda wake.
Kadhalika taarifa Lameck Nganga ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, akichukua nafasi ya Kolimba aliyehamishiwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Tanga
Bahati Mfungo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu, akitoka Wilaya ya Arumeru alikokuwa Afisa Tarafa.
Pia Rais samia amefanya mabadiliko kadhaa ya wakuu wa wilaya akimhamisha Mkuu wa Wilaya Handeni, Albert Msando kwenda Wilaya ya Ubungo akichukua nafasi ya Twange anayeteuliwa kuwa bosi wa Tanesco.
Japhari Kubecha yeye amepelekwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni akitokea Wilaya ya Tanga. Dadi Horace Kolimba amehamishiwa kutoka Karatu kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga.