Wenje: Nitasimama na Chadema, sina mpango wa kuhama

Muktasari:
- Ametoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuweka wazi msimamo wake wa anabaki au anaondoka.
Geita. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje amesema hawezi kuhama chama hicho akisisitiza bado anaamini katika nguvu ya chama hicho kuleta mabadiliko ya kweli nchini licha ya sintofahamu iliyoibuka baada ya uchaguzi wa ndani wa chama uliofanyika Januari 21, 2025.
Katika uchaguzi huo, Wenje aligombea nafasi ya umakamu mwenyekiti Bara akimuunga mkono, Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea uenyekiti.

Wenje alishindwa na John Heche huku Tundu Lissu akiibua mshindi wa mwenyekiti dhidi ya Mbowe aliyeiongoza kwa Chadema kwa kipindi cha miaka 21.
Wenje ametoa kauli hiyo jana Jumamosi, Mei 10, 2025 mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara wa Kampeni ya No reforms, No election 'Bila mabadiliko hakuna uchaguzi' uliofanyika Manispaa ya Geita.

Katika mkutano huo, umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema na viongozi mbalimbali.
Katika mkutano huo, Mnyika alimsimamisha Wenje akitaka aeleze ukweli umma wa wananchi kuhusy hatima yake.
Mnyika amedai yapo maeneno yanayosemwa Wenye amepanga kuondoka na kumtaka athibitishe mbele ya umma kama ataendelea kuwa sehemu ya harakati za chama hicho.
“Wenje walikuwa wanasema unaondoka sauti ya watu ni sauti ya Mungu nataka useme hapa umesimama jukwaani umeona matumaini ya Watanzania nataka utoe kauli mbele yao wewe hutakuwa sehemu ya wanaoondoka useme kutoka ndani ya nafsi na mwenyezi Mungu anakusikia," amesema Mnyika.
Akijibu wito huo, Wenje amesema ataendelea kusimama na Chadema kwa kuwa bado anaona matumaini kwa Watanzania kupitia chama hicho.

“Watu wa Kanda ya Victoria hiki chama kimebeba matumaini ya watu wengi, mimi mwenyewe kaka yangu aliuawa kwa sababu ya Chadema, familia yangu imeumizwa kwa ajili ya chama, tuna kovu na tuna matumaini tunasonga mbele kwa kuwa tunajua tuna matumaini katika safari hii, aluta continual,” amesema Wenje.
Mnyika amesema zipo tetesi kuna mpasuko ndani ya Chadema baina ya waliokuwa timu Freeman Mbowe na timu Tundu Lissu baada ya uchaguzi kumalizika na kusisitiza tofauti hizo zimekwisha na kuwataka kuwa timu Chadema inayopambana na CCM.
“Baada ya uchaguzi wa tarehe 21 timu Mbowe na timu Lissu ziliishia pale Mlimani. Wenje alikuwa timu Mbowe, Lema alikuwa timu Lissu na mimi nilikuwa msimamizi wa uchaguzi sasa wote tumebaki wanaChadema,” amesema Mnyika.
Akizungumzia wanaodai kubaguliwa ndani ya Chama, Mnyika amesema hakuna anayebaguliwa: “Nawaomba wana Chadema na wapenzi wa Chadema kama kuna mtu ulikuwa na timu sasa aiache tuendelee kuwa timu moja ya Chadema tupambane na CCM tukisimamia No referms, No election,” amesema Mnyika
Kauli ya kubaguliwa imetolewa na makada mbalimbali ambao kwa simu wametangaza kukihama chama hicho wakiwemo waliokuwa wajumbe wa sekretarieti wakati wa utawala wa Mbowe.
Baadhi ya vigogo wa chama hicho na wanachama wameondoka wakikituhumu Chadema kuwabagua na kutokuendeshwa kwa kufuata katiba ya chama. Hawajasema wanakwenda chama gani lakini tetesi zilizopo wanajiandaa kwenda Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Wajumbe hao wa sekretarieti ni manaibu katibu wakuu, Benson Kigaila (Bara), Salumu Mwalimu (Zanzibar), katibu wa sekretarieti, Julius Mwita, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema na Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Catherine Ruge.
Pia, viongozi wa kanda, mikoa na wilaya nao wametangaza kukihama. Kuna taarifa wengine pia wataendelea kuondoka ndani ya chama hicho.
Alichokisema Lema
Akizungumza kwenye mkutano huo, Lema amesema wana makusudi na chama hicho na makusudi hayo ni mabadiliko na uhuru wa kweli na ambaye hataishi kwenye azma hiyo habaguliwi bali anajibagua.

“Kwenye chama hiki sina timu, uchaguzi umeisha na mimi moyo wangu ukichagua timu ukimalizana nao tunaendelea na kazi ya siasa, sina timu ila namchukia kwa dhati kabisa mtu anayetaka kusaliti mapambano haya," amesema Lema.