Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche aibua mapya mnyukano Chadema

Muktasari:

  • Amesema wenye kinyongo ndani ya chama hicho ni wachache ambao mirija yao imekatwa baada ya uongozi mpya kuingia madarakani.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema wenye kinyongo ndani ya chama hicho ni wachache ambao mirija yao imekatwa baada ya uongozi mpya kuingia madarakani.

Hata hivyo, amesema chama hicho hakitavumilia mambo hayo, kwa kuwa lengo lake ni kurudi kuzungumza ajenda zinazowalenga wananchi.

Kauli ya Heche, inakuja katikati ya nyakati ambazo, kumekuwa na mitazamo tofauti ndani ya Chadema, kutokana na makundi yaliyotokana na uchaguzi wa ndani.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Januari 21 na 22, mwaka huu, Tundu Lissu alimshinda Freeman Mbowe, huku Heche akimshinda Ezekia Wenje katika wadhifa wa makamu mwenyekiti bara.

Makundi katika uchaguzi huo, yalikuwa kati ya wanaomuunga mkono Mbowe na wale wa Lissu. Hata hivyo, baada ya matokeo, wagombea wote walikubaliana kujenga umoja ndani ya chama hicho, huku kaulimbiu ikiwa ni ‘Stronger Together.’

Heche ameyasema hayo leo, Ijumaa Februari 21, 2025 alipokutana na kuzungumza na wanachama wa chama hicho katika Kanda ya Kaskazini.

Ameijenga hoja hiyo kwa kurejea kikao cha Kamati Kuu alichodai kiliyazungumza mambo yote kuhusu uchaguzi mbele ya viongozi wakuu, hivyo hawana muda wa kupoteza sasa.

Kwa mujibu wa Heche, waliobaki na kinyongo ni wanachama wachache ambao mirija yao imekatwa baada ya uongozi mpya kuingia madarakani.

“Hao ndio wana kinyongo, wanataka watuletee mgogoro na nataka nitumie nafasi hii kuwaambia hatuko dhaifu, kwa mnaonifahamu mimi sio dhaifu,” amesema.

Amesema chama hicho hakitavumilia mambo hayo, kwa kuwa lengo lake ni kurudi kwenye ajenda za wananchi.

Heche amewasihi wanachama waachane na yanayoendelea katika vyombo vya habari alivyodai vinataka kusababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

Amesisitiza hata kwa wale wasiomuunga mkono katika uchaguzi wa chama hicho, hakuwahi kuwa na kinyongo nao na asingependa yeyote amuombe msamaha kwa kutomuunga mkono.

Amesema historia yake ndani ya chama hicho ni kuwa na vijana ambao baada ya kuhamia CCM waliteuliwa kuwa viongozi ndani ya Serikali, lakini yeye alibaki.

“Sio kwa sababu sikushawishiwa, nimeshawishiwa sana. Leo nikichukia kile tunachokipigania ninapokiona nitakuwa mtu wa ajabu sana,” amesema.

Sambamba na hayo, Heche amesema baada ya uchaguzi uteuzi katika nafasi yoyote ndani ya chama hicho utazingatia uwezo wa mtu na sio kwa sababu aliuunga mkono uongozi uliopo madarakani.

“Hatutakuwa na upendeleo, kama unastahili kupata viti maalumu na tunavyo, utapata wewe unayestahili. Hatutafanya hivi kwamba watu fulani wana viti maalumu vya kudumu, mbele yangu na mbele ya Lissu ondoa kabisa,” amesema.

Amesema kama kuna wanaodhani wamejenga mzinga wa asali, chama hicho kinaushusha chini na mambo yote yatakwenda inavyotakiwa.

Amejengea hoja kauli ya ‘No reform no election’, akisema chama hicho kilibainisha mapungufu 16 kwenye sheria ya uchaguzi, ambayo ni kikwazo kwa mpinzani kushinda.

Amesema wamepeleka ripoti hiyo kwa viongozi wa dini na kuwaeleza nini wanataka, ili waende kwenye uchaguzi huru na haki.

Amesema kwa sasa wanaendelea kuyaona mashirika yasiyo ya kiserikali kisha jumuiya za kimataifa na baadaye watatoa msimamo.

Heche amesisitiza uamuzi wa chama hicho kupigania mageuzi ya mifumo ya uchaguzi, wanalenga kurudisha nguvu ya kura ya wananchi.

Amesema yaliyoshuhudiwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa yanatosha kwa upinzani kudai uchaguzi huru na haki, ndiyo maana chama hicho kimetoka na msimamo wake.

“Halafu leo kuna mwana-Chadema anasema twende kwenye uchaguzi, huyo ni mwenzetu? Wendawazimu ni kufanya jambo lilelile kwa njia zilezile na utarajie matokeo tofauti,” amesema.

Kuhusu kujiandaa

Akijibu hoja ya CCM  kwamba hawajajiandaa, Heche amesema ushindi wa uchaguzi hautokani na fedha, badala yake ni kuwa na wagombea bora, jambo ambalo Chadema wamesheheni.

Jambo lingine, amesema chama hicho kina ajenda ambazo pia ni nyenzo muhimu ya ushindi katika uchaguzi wowote.

“Sisi tunahitaji haki na uhuru tu, puliza kipenga hata kesho Chadema iwashughulikie muone. Hatuhitaji hata miezi mitatu kupuliza kipenga, tuna mtandao mkubwa nchi hii, tunachohitaji ni tume huru na ya haki tu,” amesema.

Heche amesema hawatakubali kwenda kufanya uchaguzi wa kuisindikiza CCM.