Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kardinali Nichols afichua kilichojiri uchaguzi wa Papa mpya

Muktasari:

  • Kardinali wa Uingereza afichua maelezo kuhusu mchakato na hisia za uchaguzi wa Papa mpya, akizungumzia hatua zilizochukuliwa na majukumu ya viongozi wa Kanisa Katoliki.

London. Wakati Ibada ya kwanza ya Papa mpya inatarajiwa kufanyika Mei 18, Kardinali mmoja kutoka Uingereza amefichua jinsi Papa Leo XIV alivyoiitikia kwa utulivu alipoulizwa kama anakubali kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

Alisema baada ya kuchaguliwa, akionyesha kuwa ‘hatawaogopa watawala wa kiimla,’ kufuatia kikao cha siri cha uchaguzi wa Papa. Jina halisi la Papa Leo XIV ni Kardinali Robert Francis Prevost.

Kardinali Vincent Nichols (79), ambaye ni kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Uingereza na Wales, alikuwa miongoni mwa makardinali 133 walioshiriki katika kikao cha kumchagua Papa mpya, alisema kuwa kila hatua ya mchakato huo ilifuatwa kwa umakini na uangalifu mkubwa.

Kardinali Vincent Nichols kutoka Uingereza.

Kwa Kardinali Nichols, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Westminster, huu ulikuwa mkutano wake wa kwanza wa ‘conclave’, na alifanikiwa kushiriki kwa kuwa bado hajafikisha umri wa miaka 80  ambao ndiyo ukomo wa kushiriki katika mchakato huo.

Kardinali Nichols aliiambia gazeti la mtandaoni la MailOnline kutoka Uingereza jinsi aliyekuwa Kardinali Robert Francis Prevost (sasa Papa Leo XIV) alivyopokea kwa utulivu jukumu lake jipya la kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, alipoulizwa kama anakubali wadhifa huo.

"Kulikuwa na hali ya furaha ya dhati alipokubali wadhifa wa Papa. Nilikuwa nimesimama umbali wa futi chache tu alipokuwa akizungumza, na alikuwa mtulivu wa hali ya juu.

"Aliupokea kwa utulivu na mtazamo wa kawaida kabisa, bila kuonyesha hisia nyingi. Alikubali jukumu hilo kwa utulivu mkubwa," alisema Kardinali Nichols.

Kardinali Nichols pia alieleza kuwa Papa Leo XIV "hatawaogopa watawala wa kiimla" baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki.


Sifa ya Papa Leo XIV

"Ningesema Papa Leo ni raia wa dunia na baada ya kutafakari, ilikuwa wazi kwamba huyu ni mtu mwenye kina cha kiroho kinachohitajika na uzoefu wa kuongoza kanisa."

"Kwa kweli kulikuwa na sehemu yangu ambayo haikutaka kuondoka kwa sababu ilikuwa hali ya kiroho ya kipekee sana na nitaithamini sana."

"Yeye ni mtulivu sana, ana mawazo ya wazi, ni mwenye maamuzi, na nimemwona akitatua matatizo bila kuacha maadui nyuma  ana uwezo wa kuwaleta watu pamoja.

Kisha akitoa hisia zake za kwanza kuhusu Liverpool timu yake ya kipenzi kushinda Ligi Kuu ya England, Kardinali Nichols aliambia MailOnline: "Ilikuwa furaha kiwango kikubwa kabisa pia."


Kuhusu Papa wa zamani aliyeitwa Leo

Katika kauli ya kuvutia kuhusu Papa wa zamani aliyeitwa Leo, alisema: "Mwaka 452 BK, Papa Leo alimzuia Attila wa Hun kuingia Jiji la Roma jambo linaloonyesha kwamba hataogopa watawala wa kiimla."

Papa Leo XIII, alikuwa Papa maarufu kwa juhudi zake katika kukuza haki za wafanyakazi na kutoa mafundisho kuhusu haki za kijamii.

Alipoulizwa kama alikuwa akimzungumzia Rais Donald Trump wa Marekani, Kardinali Nichols alijibu: "Huenda ukasikia hivyo, lakini mimi sikusema hivyo."

Kardinali Nichols, mzaliwa wa Liverpool, alifafanua pia sababu ya kuchelewa kwa moshi mweusi, ambao huashiria kuwa hakuna Papa aliyechaguliwa baada ya kura ya kwanza Jumatano, kwa zaidi ya saa mbili.

Alimlaumu padre wa Kipapa, Raniero Cantalamessa, mwenye umri wa miaka 91, kwa kuongea kwa karibu saa nzima zaidi ya ilivyotarajiwa, jambo ambalo liliwaacha watu 45,000 waliokusanyika nje ya Vatican wakiwa katika hali ya kusubiri kwa hamu.

Alisema: "Nadhani inafahamika kuwa Padri Cantalamessa alitoa hotuba ndefu sana... ilikadiriwa kuwa ya saa moja au zaidi. Mtu mmoja alisema ilikuwa hotuba yake ya kuaga, na kweli ilikuwa nzuri sana."

 “Ilipendekezwa kuwa ingetumia nusu saa tu, lakini iliendelea kwa muda mrefu zaidi. Subira ni fadhila nzuri, na haiwezi kuonyeshwa kirahisi isipokuwa unapoitenda.”

Akifichua undani wa jinsi conclave ilivyofanyika, Kardinali Nichols alisema: “Kulikuwa na hali ya undugu wa kipekee, watu kutoka kila pembe ya dunia.”

“Hakukuwa na usumbufu kutoka kwa simu za mkononi na kulikuwa na roho ya mshikamano miongoni mwa sisi.”

“Ilikuwa ni kipindi cha subira kuu kwa sababu tulifuata kila hatua kwa umakini mkubwa, na hilo lilihitaji muda, hata zoezi lenyewe la upigaji kura lilichukua muda mrefu.”

Aliongeza: "Ilikuwa uamuzi wa haraka sana, kura nne tu, na nadhani hiyo ni kwa sababu Papa Francis aliacha kundi la makardinali waliokuwa na maono na roho kama yake ya kuwa Kanisa la kimisionari."


Kuhusu Attila wa Hun

Attila, alikuwa kiongozi wa Wahunni kutoka mwaka 434 hadi alipofariki mnamo 453.

Alisimamia himaya iliyounganisha makabila mbalimbali kama vile Waostrogoti, Waalani, Wabulgari na wengineo katika Ulaya ya Kati na ya Mashariki. Attila alipigana katika vita nyingi na majirani.


Kuhusu idadi ya Wakatoliki

Kwa sasa (makadirio ya 2024), yanaonyesha idadi ya Wakatoliki duniani inakadiriwa kuwa takribani watu  bilioni 1.38  hadi  bilioni 1.4 na hiyo inawafanya kuwa kundi kubwa zaidi la Wakristo duniani. Hii ni karibu asilimia 17 hadi 18 ya watu wote duniani.

Mgawanyo wa Wakatoliki duniani (kwa ufupi):

Amerika ya Kusini – Karibu asilimia 40 ya Wakatoliki wote duniani, Brazil ikiwa nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi (zaidi ya milioni 120).

Ulaya – Takribani asilimia 24, ingawa idadi inashuka polepole.

Afrika – Inakua kwa kasi, inachukua karibu asilimia 18 ya Wakatoliki wote duniani.

Asia – Takribani asilimia 12, pamoja na idadi kubwa nchini Ufilipino (takriban milioni 85).

Amerika Kaskazini na Oceania – Idadi ndogo zaidi kwa pamoja (chini ya asilimia 10).


Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao