Rais Samia aacha tabasamu Liwale

Muktasari:
- Wananchi wa Halmashauri ya Liwale mkoani Lindi wamebaki na tabasamu baada ya Rais Samia kuwahakikishia kuwatatulia changamoto zinazowakabili ikiwamo uvamizi wa tembo.
Liwale. Rais Samia Suluhu Hassani amesema kuwa changamoto zote ambazo zinaikabili Halmashauri ya Liwale anakwenda kuzifanyia kazi na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo zinapatikana katika halmashauri hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kuwasili kutoka mkoani Mtwara leo Jumapili Septemba 17, 2023 amesema kuwa anajua changamoto zinazowakabili Wanaliwale ikiwemo wanyama wakali ambapo ngazi ya Mkoa na Wilaya wamsehindwa kutatua huku akiahidi kulichukua na kulifanyia kazi Serikali Kuu.
Rais Samia amesema kuwa changamoto nyingine ni barabara ya Liwale-Nagurukuru ambayo wakati wa mvua haipitiki kwa urahisi na kusema kuwa zitatengwa fedha kwa kwaajili ya barabara hiyo ambayo ina urefu wa kilometa 72.
"Serikali inachukua changamoto zote ikiwemo zile za wanyama wakali aina ya tembo kwakuwa ngazi ya Mkoa na Wilaya wameshindwa kulifanyia kazi nalichukua kama Taifa na nitakaa na viongozi wa Kitaifa ili zifanyiwe kazi kwa haraka.
"Kuhusu kero ya barabara ya Nangurukuru-Liwale yenye urefu wa kilometa 72 itakwenda kutatuliwa na Mkoa wa Lindi na Mtwara unaingia kwenye Grid ya Taifa kutokea Mkoa wa Ruvuma pia amewataka vijana kufuga nyuki na kuwaambia kuwa Serikali itawapatia soko," amesema Rais Samia.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Tellack akitoa salamu za mkoa alisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya wanyama waharibifu aina ya tembo katika Wilaya ya Nachingwea na Liwale pamoja na changamoto ya wakulima na wafugaji.
RC Tellack amesema kuwa mkoa wameunda kamati za ulinzi kwa kusimamiwa na askari, wagambo na wananchi wenyewe na kufanya oparesheni mara kwa mara pia amesema kuwa mkoa wanakesi tano ambazo ni za ubakaji, kuharibiwa mali.
"Mkoa wa Lindi unakabiliwa na changamoto ya mifugo pamoja na wanyama wakali tembo lakini tumeunda kamati mbalimbali ilikuweza kutusaidia ulinzi wa awali pale ambapo kuna mifugo ili wasiingie na kufanya oparesheni mbalimbali pale ambapo kuna changamoto kubwa," amesema.
Naye, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamedi Mchengerwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Liwale asiwe mpole katika kusimamia miradi ya maendeleo hadi kufikia hatua ya watendaji kujinufaisha pesa za Serikali.
Waziri Mchengerwa ameendelea kusema kuwa fedha zinazotolewa ni kwa ajili ya wananchi na sio kujinufaisha watendaji na kuongeza ubadhirifu wa fedha Liwale ni mkubwa na kumtaka mkurugenzi kusimamia ipasavyo fedha za Serikali.
"Ofisa manunuzi aliehama nimuagiza asimamishwe kazi hukohuko alipo na huyu aliyeletwa mpya nae ashushwe cheo na kusimamishwa kazi kwakuwa wanachelewesha maendeleo," amesema Waziri Mchengerwa.
Matumla Issa ni mkazi wa liwale amesema kuwa ujio wa Rais Samia hasa vijana wamepata fursa za kufuga nyuki ambapo awali waliacha ufugaji wake kwakuwa soko lake halikuwa zuri.
Fadhila Bakari amesema kuwa anaamini matatizo ya kuingiliwa na wanyama wakali kama tembo Rais Samia anaenda kuyafanyia kazi kwa haraka.
"Furaha yangu kubwa kwa Rais wetu aliposema kuwa tatizo la tembo atakwenda kulitatua kwa haraka kiukweli nimefarijika sana tembo wanasumbua sana hapa kwetu Liwale, tumeacha mashamba yetu kulima kwa ajili ya kuogopa tembo," amesema Fadhila.