Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaja na mwarobaini kuporomoka majengo

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Kufuatia kuporomoka kwa jengo la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 29, Serikali imekuja na mwarobaini wa changamoto zilizopo hususan katika masuala ya uratibu, usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo hapa nchini.

Dodoma. Wizara ya Ujenzi imewasilisha bajeti yake kwa mwaka 2025/26 huku ikisema kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne Kariakoo jijini Dar es Salaam inatunga sheria ya majengo kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya majengo nchini.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 5, 2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26.

Katika mwaka wa fedha 2025/26 Wizara ya Ujenzi inaomba kuidhinishiwa Jumla ya Sh2.28 trilioni kati ya hizo, Sh2.18 trilioni zinakwenda katika shughuli za miradi ya maendeleo huku Sh90.46 bilioni zikienda katika matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake.

Wakati kukiwa na ongezeko la bajeti, mwaka 2024/25, Bunge liliidhinishia wizara hiyo, Sh1.77 trilioni huku Sh1.68 trilioni zikienda katika shughuli za miradi ya maendeleo.

Akiwasilisha bajeti hiyo yenye vipaumbele 10, Waziri Ulega amewapa pole kwa wote walioathirika na maafa hayo na kuomba marehemu wote wapumzike kwa amani.

“Wizara yangu, ikiwa ni msimamizi wa shughuli za majenzi nchini, inaendelea na taratibu za kutunga sheria ya majengo kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya majengo nchini,” amesema.

Amesema sheria hiyo itakapoanza kutumika itakuwa mwarobaini wa changamoto zilizopo hususan katika masuala ya uratibu, usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo hapa nchini.

Jengo hilo la ghorofa nne katika mtaa wa Congo na Mchikichi, eneo la Kariakoo liliporomoka Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo vya watu 29, majeruhi 88 na hasara ya mali.

Mbali na jengo hilo, majengo mengine yaliyowahi kuporomoka na kusababisha athari na lililoporomoka mwaka 2006 eneo la Chang’ombe, Dar es Salaam na kuua watu wanne. Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa alitoa maagizo watu wawajibishwe kwa uzembe uliojitokeza.

Juni 21, 2008 ghorofa jipya lililokuwa linajengwa mitaa ya Mtendeni na Kisutu lilianguka na kuangukia jengo dogo walimokuwa wakiishi watu.

Machi 29, 2013 jengo la ghorofa 16 katika makutano ya barabara za Zanaki na Indira Ghandi lilianguka na kusababisha vifo vya watu 36, sababu ya kuporomoka ikitajwa kuwa ujenzi usiozingatia utaalamu.

Vipaumbele 10

Ulega amevitaja vipaumbe vya wizara hiyo ni kuendelea na ujenzi wa barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi, kuimarisha shughuli za kijamii pamoja na zile zinazounganisha barabara na njia nyingine za usafiri.

Nyingine ni kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, nchi jirani pamoja na barabara za ulinzi kwa kiwango cha lami na kuendelea na ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano katika miji inayokua kwa kasi na majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Morogoro.

“Kuendelea na ukarabati na matengenezo ya barabara kuu na mikoa ili kuhakikisha zinapitika katika majira yote ya mwaka pamoja na matengenezo makubwa ili kuhakikisha kuwa barabara haziendelei kuharibika na kupoteza thamani,” amesema.

Nyingine amesema kuendelea kuimarisha usafiri na miundombinu ya vivuko ili kuunganisha maeneo ya nchi kavu ambayo yametenganishwa na maji katika maeneo ya bahari, maziwa na mito na kuendelea na miradi ya usalama barabarani ikiwemo kujenga mizani pamoja na kusanifu na kujenga barabara za michepuo na zile zinazozingatia mahitaji ya watumiaji wote wa barabara.

Ametaja vipaumbele vingine kuendelea kujenga nyumba za watumishi wa umma na majengo ya Serikali kwa kuupa kipaumbele utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kwa lengo la kuwaongeza wabobezi wa ndani, pamoja na kutoa kipaumbele kwa kampuni za ndani zinazohusika na masuala ya ujenzi.

Ulega ametaja vipaumbele vingine ni kuendelea na mapitio ya sera, miongozo na mifumo inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi ili iendane na wakati ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya teknolojia na maendeleo endelevu.

Kipaumbe kingine ni kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vilivyokasimiwa Wizara ya Ujenzi, ikiwemo Msalato.

Aidha, Ulega amesema hadi Aprili 2025 jumla ya magari 8,344,978 yalikuwa yamepimwa katika mizani 79 iliyopo nchini ambapo kati ya hayo, magari 22,585 sawa na asilimia 0.27 yalikuwa yamezidisha uzito zaidi ya asilimia tano ya unaoruhusiwa kisheria.

Amesema wasafirishaji waliozidisha uzito walichukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu udhibiti wa ajali, Ulega amesema katika kuboresha usalama barabarani, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imefanya ukaguzi wa usalama barabarani (Road Safety Audit), ili kutambua maeneo hatarishi na kuyafanyia maboresho.

Amesema wizara kupitia Tanroads imeweka alama na michoro muhimu ya barabarani na kufunga taa za kuongoza watumiaji wa barabara (traffic signals) katika makutano ya barabara pamoja na taa za barabarani (street lights) katika maeneo mbalimbali ya miji.

Ulega amesema katika kupambana na ajali zinazosababishwa na uchovu wa madereva, Wizara kupitia Tanroads inafanya usanifu wa kujenga maeneo ya kupumzika.

“Vituo vilivyopangwa kujengwa kwa upande wa Ushoroba wa Kati ni Muhalala (Manyoni) na Nyakanazi (Kagera) na ushoroba wa Dar es Salaam-TANZAM vitakuwa maeneo ya Vigwaza (Pwani), Ruhaha Mbuyuni (Morogoro), Idofi (Makambako) na Iboya (Songwe),” amesema.

Amesema kwa upande wa ushoroba wa Kaskazini vituo hivyo vitajengwa maeneo ya Segera (Tanga) na Himo (Kilimanjaro),”amesema Ulega.


Miundombinu iliyoharibiwa na mvua

Ulega amesema kupitia programu ya Crisis and Emergency Response Component (CERC) jumla ya mikataba 81 yenye thamani ya Sh556.92 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya dharura imesainiwa na makandarasi wanaendelea na kazi.

Amesema kati ya hiyo, miradi mitano inatekelezwa katika mradi wa Msimbazi Basin Development Project, miradi sita inatekelezwa katika mradi wa RISE na miradi 70 inatekelezwa chini ya TanTIP.

Amesema kati ya mikataba hiyo, miradi 72 inatekelezwa na makandarasi wazawa na kuwa katika mwaka 2025/26, kipaumbele kitakuwa kufanya matengenezo makubwa ya barabara ili zisiendelee kuharibika.

Amesema barabara zilizopangwa kufanyiwa matengenezo ni pamoja na Dar es Salaam – Kibiti - Lindi – Mingoyo (km 463) ambayo ilijifunga kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni na barabara hiyo itajengwa kwa awamu.

“Niwahakikishie watumiaji wa barabara hii kuwa, matengenezo haya makubwa yatakapokamilika itakua ni suluhisho la changamoto ya kujifunga mara kwa mara,” amesema.