Prime
Mawaziri watatu kubanwa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa ratiba, bajeti ya Wizara ya Ujenzi itajadiliwa kesho Jumatatu na Jumanne, kisha itafuata Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Jumatano ya Mei 7, 2025 kisha Alhamisi na Ijumaa itakuwa ni Bajeti ya Wizara ya Maji.
Dodoma. Mawaziri watatu wataingia katika mjadala wa wabunge kuhusu bajeti za wizara zao kwa mwaka 2025/26 huku hoja kubwa zikitarajiwa kujitokeza zikiwa ni madeni ya makandarasi kwenye miradi ya barabara na utekelezaji wa ahadi za viongozi.
Wizara zitakazokutana na kiu ya wananchi kutaka majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili ni ya Ujenzi inayoongozwa na Abdallah Ulega, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, (Profesa Palamagamba Kabudi) na Wizara ya Maji, Jumaa Aweso.

Kwa mujibu wa ratiba, bajeti ya Wizara ya Ujenzi itajadiliwa kwa siku mbili kesho Jumatatu na Jumanne, kisha itafuata Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Jumatano ya Mei 7, 2025 ambayo itajadiliwa kwa siku moja.
Kuanzia Alhamisi na Ijumaa itakuwa ni Bajeti ya Wizara ya Maji.
Hoja zingine zinatotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa uwasilishaji wa bajeti za wizara hizo kwa wiki inayoanza wa maji katika maeneo kesho Jumatatu, Mei 5, 2025 ni upatikanaji mbalimbali ya mijini na vijijini, hali mbaya ya uchumi wa vyombo vya habari, masilahi ya wanahabari na uwepo wa sheria zinazolalamikiwa na vyombo vya habari.
Bunge hilo lililoanza vikao vyake Aprili 8, 2025 limeshajadili na kupitisha bajeti ya sita ambazo ni za Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Zingine ni Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Nishati, Wizara ya Madini na Wizara ya Katiba na Sheria.
Mkutano huu wa 19 wa Bunge ni wa mwisho kwa uhai wa Bunge ambalo Juni 27, 2025 litahutubiwa na kuvunjwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kwenda katika michakato ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wa madiwani, wabunge na Urais.
Kwa muda sasa kumekuwa na vilio vya wabunge kuhusu utekelezaji wa ahadi za viongozi wakuu wakiwamo marais waliopita kuhusiana na ujenzi wa barabara.
Miundombinu ya barabara ni miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wabunge. Kwa barabara zilizopo chini ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) chini ya Tamisemi, wabunge walishupalia ukarabati wa barabara zao.
Sasa itakuwa zamu ya Waziri Ulega ambaye atajibu hoja ambazo wabunge wataziibua zikiwamo za barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Katika bajeti za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2021/2022, 2023/24 wabunge walionesha hofu yao kuhusu utekelezaji wa ahadi za marais waliopita Benjamin Mkapa (marehemu), Jakaya Kikwete na John Magufuli (marehemu).
Hoja hiyo iliibuka kwa mara nyingine katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Februari 4, 2025 ambako Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka alihoji Serikali inatumia utaratibu gani kuhakikisha utekelezaji wa ahadi za viongozi ili zisionekane kama ni ahadi zisizotekelezeka.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi(Ofisi ya Waziri Mkuu) Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga alisema ili kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa ahadi za viongozi zinakua na uhalisia, Ofisi ya Waziri Mkuu ilibuni na kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki wa uratibu na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali (Dashboard).
Madeni ya makandarasi bado ni hoja itakayojikita katika mjadala wa bajeti ya Waziri Ulega.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu shughuli zilizofanyika mwaka 2023, inabainisha miongoni mwa changamoto zinazoikabili Tanroads ikiwamo ucheleweshaji wa ulipaji wa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri hali inayosababisha ongezeko la gharama.
Kwa mfano taarifa hiyo ilibainisha miradi iliyokamilika ilikuwa 94 na makandarasi washauri walikuwa wanaidai Serikali Sh386.36 bilioni huku miradi ya barabara inayoendelea kujengwa ikiwa ni 69, yenye deni la makandarasi la Sh392.6 bilioni, hivyo kufanya jumla ya deni lote kuwa ni Sh778.96 bilioni.
Kwa mwaka 2024/25, Bunge lilipitishia Wizara ya Ujenzi bajeti ya Sh1.77 trilioni huku Sh1.6 trilioni zikielekezwa katika miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, mwaka 2024, Serikali iliweka mkakati rasmi wa kulipa madeni ya makandarasi kwa kiwango cha Sh70 bilioni kila mwezi ambapo Sh50 bilioni zinawalenga makandarasi wazawa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee amesema bado hoja ya kushindwa kwa mfumo wa utekezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara kwa mfumo wa EPC+F (Procurement, Construction and Finacing) itaendelea kuzungumziwa bungeni kwenye mjadala huo.
“Madeni ya makandarasi na wataalamu washauri bado ni tatizo sugu. Miradi mingi iko kwenye mkwamo. Wizara ya Fedha pia haipeleki fedha kama inavyotakiwa hata zile ambazo zina ulinzi wa kisheria (ring fancing),” amesema.
Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), amezitaja baadhi ya tozo hizo ni zile wananchi wanazotozwa kwenye mafuta lakini haziendi kulikokusudiwa kwenye ujenzi wa barabara.
Hali mbaya ya vyombo vya habari
Kwa upande wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, hoja ya maandalizi ya viwanja vya michezo kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON2027) nayo inatarajiwa kuzungumzwa na wabunge.
Pia, wadau wa habari wanatarajia kusikia suala la masilahi ya waandishi wa habari na hali ya uchumi ya vyombo vya habari inashughulikiwa kwa namna gani na Serikali.
Machi 2023, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliunda timu ya watu waliofanyia tathimini hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini iliyowasilisha ripoti kwake.
Ripoti hiyo tayari imekwisha kabidhiwa serikalini. Huenda ikawa sehemu ya mijadala ya wabunge.
Akizungumzia kuhusu matarajio yake kwa bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta), Mussa Juma amesema wanashukuru waziri amewaalika kwenda kusikiliza hotuba na mjadala wa bajeti hiyo bungeni, lakini matarajio yao ni kusikia jinsi Serikali ilivyoshughilika na changamoto za sekta ya habari.
Amesema bado Serikali inatakiwa kuboresha sheria zinazosimamia sekta hiyo ili kutoa uwanja mpana kwa uwekezaji.
Juma ametaja miongoni mwa sheria hizo ni ile inayotaka hisa zaidi ya asilimia 50 kwenye vyombo vya habari ziwe zinamilikiwa na wazawa (Watanzania).
Amesema sheria hiyo inawanyima fursa wawekezaji ambao wangeweza kuwekeza vya kutosha katika sekta hiyo, hivyo kuinua masilahi ya waandishi wa habari nchini ambayo bado ni duni.
"Tunatarajia kusikia suala la masilahi ya waandishi wa habari limeshughulikiwaje maana bado waandishi wengi hawana mikataba, masilahi yao ni duni," amesema.

Amesema pia sheria inataka kuanzishwa kwa mfuko wa kuendeleza waandishi wa habari, hivyo wanatarajia uanzishwaji wake umefikia wapi pamoja na suala la kuanza kwa bodi ya ithibati ya waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema ukiangalia taarifa ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, tatizo kubwa ni uchumi na uhuru wa vyombo vya habari hautishiwi na Serikali, mtu mmoja mmoja au kampuni bali ni uchumi.
Balile amesema hata vyombo vikubwa vya habari duniani vinafunga matawi yake, wamepunguza bidhaa nyingi za lugha kwa sababu ya uchumi.
“Sasa ajenda inayopaswa kusukumwa ni uchumi wa vyombo vya habari. Hata mwaka 2008 ilitokea mdororo wa uchumi na Serikali kutoa fedha kuokoa, basi ni wakati sasa kwa Serikali duniani ikiwamo Tanzania kutoa fedha kuviokoa kwa sababu ni muhimu jana, leo na kesho,” amesema Balile.
Kusuasua kwa upatikani wa maji
Lakini katika Wizara ya Maji, bado wananchi wanakabiliwa na uhaba wa maji, upatikanaji wa maji umekuwa wa kusuasua katika maeneo mengi, hali ambayo imewafanya waliounganishiwa maji kuyatazama kumiliki mabomba yasiyo na faida kwao.
Suala la maji limekuwa likipigiwa kelele mara kadhaa na wabunge na wengine wamekuwa wakisikika wakisema linaweza kuwapa wakati mgumu kwa wananchi wao hasa kipindi hiki, hivyo watambana waziri kuhakikisha wanampatia majibu sawia ya miradi iliyopo kwenye maeneo yao.
Malalamiko ya mgawo usiofuatwa wa maji, yamesikika katika maeneo ya miji, mamlaka za maji kwenye kukabiliana na upungufu wa maji imepanga siku za mgawo wa maji.
Kwenye maeneo hayo, bado wananchi wamelazimika kutumia vipato vyao vidogo kununua huduma hiyo kwa gharama kubwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji upatikani wa maji maeneo ya vijijini umefukia asilimia 83 kutoka asilimia 79 ya mwaka 2020 huku mijini ikifikia asilimia 91.6 kutoka asilimia 84 mwaka 2020.
Wakati wananchi wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, katika mwaka 2024/25, bajeti Wizara ya Maji ilikuwa ni Sh627.7 bilioni pungufu ya asilimia 17 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2023/24.
Kupungua kwa bajeti hiyo, kulilalamikiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ikisema kupungua huko kunaonesha sekta hiyo haikuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali katika mwaka huo wa fedha.
Hata hivyo, mkazi wa Nkhungu jijini Dodoma, Raheli Mbwana amesema bado changamoto ya upatikanaji wa maji ni kubwa katika jiji hilo, hali inayowafanya kutumia gharama kubwa katika maisha.

"Kwa kuunganisha mabomba Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini nyakati za sasa kuunganishiwa maji ni hatua moja na upatikanaji wa maji ni hatua nyingine," amesema.
Amesema mamlaka za maji zimejaribu kuwa na mgawo ili kuwezesha maeneo yote kupata maji angalau mara tatu au mbili kwa wiki lakini bado hakuna utekelezaji wa ratiba hizo walizoweka.
Amesema wakati mwingine baadhi ya maeneo yameshindwa kupata maji hata mara moja kwa wiki kama ratiba ya mgawo inavyotaka, hivyo kufanya kutokuwepo kwa uhakika wa kupata huduma hiyo.
Raheli amesema ni mategemeo yake Serikali itaongeza bajeti ya Wizara ya Maji katika mwaka 2025/26 ili kuboresha hali ya upatikanaji wa maji baada ya kusambaza miundombinu na kuunganisha huduma hiyo kwa watu wengi.