Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utekelezaji wa bajeti unavyoongeza hatari ya ukuaji wa deni la taifa

Utekelezwaji wa bajeti ya serikali ni ule utaratibu unaotumika kuhakikisha bajeti iliyoidhinishwa na Bunge inatekelezwa kwa usahihi na ufanisi katika jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo stahiki.

Utaratibu huu unahuisha namna Serikali inavyokusanya mapato (kama vile kodi, misaada, mikopo n.k) na kuyatumia mapato hayo katika kugharamia huduma kama elimu, afya, miundombinu, n.k., kwa kufuata makadirio na mipango iliyoidhinishwa na Bunge.

Kama utekelezaji wa bajeti unakuwa mzuri, maana yake Serikali inakusanya mapato na kuyatumia kama ilivyopangwa na kuidhinishwa na Bunge katika kufanikisha malengo ya maendeleo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wake wa Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imeonyesha kumekuwa na utekelezaji mzuri wa bajeti kwenye makusanyo ya mapato kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Katika mwaka wa fedha 2021/22, Bunge liliidhinisha bajeti ya Sh37.99 trilioni 37.99, lakini Serikali ilikusanya jumla ya Sh38.30 trilioni, hivyo kuvuka lengo la makusanyo.

Hali hii iliendelea kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo bajeti ya Sh41.48 trilioni iliidhinishwa na Bunge, na Serikali ikakusanya Sh41.88 trilioni 41.88.

Vilevile, kwa mwaka wa fedha 2023/24, bajeti iliyoidhinishwa ilikuwa Sh44.39 trilioni, lakini makusanyo yalifikia Sh46.50 trilioni ikiashiria nyongeza ya asilimia 5 ya mapato yaliyokuwa yamepangwa kukusanywa.

Kwa ujumla, utekelezaji wa bajeti umekua kwa zaidi ya asilimia 100 kwa miaka yote mitatu mfululizo. Ripoti ya CAG inaeleza kuwa mafanikio haya yametokana, kwa kiasi kikubwa, na Serikali kukopa zaidi ya ilivyopangwa awali.

Katika mwaka 2021/22, Serikali ilipanga kukopa shilingi trilioni 11.162, lakini ilikopa Sh12.44 trilioni. Mwaka uliofuata wa 2022/23, lengo la kukopa lilikuwa Sh12.36 trilioni, lakini utekelezaji ukafikia Sh14.60 trilioni.

Kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali ilikadiria kukopa Sh11.89 trilioni, lakini ilikopa Sh15.92 trilioni ikiwa ni kiasi kikubwa zaidi ya makadirio na sawa na ongezeko la asilimia 34 ya mikopo iliyokuwa imepangwa kuchukuliwa.

Hali hii inaonyesha kuwa, kwa sehemu kubwa, utekelezaji wa bajeti kwa asilimia kubwa umetegemea mikopo ambayo imezidi mipango ya awali. Ingawa makusanyo ya mapato yamevuka malengo ya bajeti, inaibua hoja kuhusu uendelevu wa utegemezi wa mikopo katika kufanikisha bajeti ya Serikali.

Kukopa zaidi kunaweza kuashiria uwepo wa changamoto katika mapato ya ndani au mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, lakini pia kunaweza kuongeza mzigo wa deni la taifa kwa siku za usoni.

Ingawa kumekuwa na ufanisi mkubwa katika makusanyo ya mapato, hususan kupitia mikopo, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha kuwa bado kuna changamoto katika makusanyo ya mapato ya ndani.

Endapo changamoto hizi zitatatuliwa kwa ufanisi, Serikali itaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa mikopo inayochukuliwa mwaka hadi mwaka..

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24, kulikuwepo na kiasi kikubwa cha mapato ya ndani ambacho hakikukusanywa kwa sababu moja au nyingine aidha na serikali kuu, serikali za mitaa au na mashirika ya umma.

Uchambuzi uliofanywa na taasisi ya WAJIBU (Institute of Public Accountability) kwa kushirikiana na Policy Forum umebainisha kuwa Serikali haikukusanya mapato yasiyotokana na kodi yenye thamani ya shilingi trilioni 1.34.

Aidha, kulikuwapo na ulipaji mdogo wa ushuru kutoka kwa watengenezaji watatu wa vinywaji baridi vya kaboni, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 609.77 hakikulipwa ipasavyo.

Uchambuzi huu, ambao uliangazia kwa kina hoja zenye umuhimu mkubwa kwa jamii zilizoibuliwa na CAG, uliwasilishwa Mkurugenzi Mtendaji wa WAJIBU, Ludovick Utouh, ambaye pia ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mstaafu).

Katika uwasilishaji wake, Utouh anaeleza kuwa kulikuwapo na mashauri ya kikodi yenye thamani ya Sh9.83 trilioni ambayo yalikuwa hayajatatuliwa hadi wakati wa ukaguzi. Aliongeza kuwa, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilishindwa kukusanya mapato yenye thamani ya Sh110.6 bilioni kutoka vyanzo mbalimbali.

Zaidi ya hayo, uchambuzi huo ulionesha kuwa baadhi ya taasisi za Serikali zilipokea fedha zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge bila kutumia utaratibu unaokubalika wa kutoa fedha zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.

Kwa jumla, kiasi cha shilingi bilioni 389.04 kilitolewa ziada katika Wizara ya Kazi, Wizara ya Nishati, pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

“Kutokukusanya mapato ya ndani kikamilifu kunasababisha Serikali kuendelea kutegemea mikopo ili kufidia mapungufu ya mapato ya ndani, hali hii inachochea kuongezeka kwa deni la Taifa.

Ingawaje deni la Taifa hadi sasa ni himilivu kwa vigezo vya Benki ya Dunia, kwa kasi ya ongezeko ya deni hilo, haitaichukua nchi miaka mingi kabla ya kufikia ukomo wa ukopaji, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa serikali kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Mathalani, mashauri ya kikodi yasiyotatuliwa kwa kipindi kirefu yenye thamani kubwa ya Sh9.83 trilioni yanakwamisha upatikanaji wa mapato ya ndani ambayo yangeweza kutumika kuimarisha huduma za jamii na hivyo kupunguza umuhimu wa kukopa.

Aidha, utoaji wa fedha zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge bila kuzingatia utaratibu ulioanishwa kisheria unadhoofisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, na unaweza kusababisha matumizi yasiyo na tija au yasiyozingatia vipaumbele vya kitaifa.

“Endapo changamoto hizi hazitatatuliwa, zinaweza kuhatarisha uthibiti wa bajeti, kuathiri huduma za kijamii, na kuongeza mzigo wa madeni kwa vizazi vijavyo.”

Utouh, ambaye alikuwa CAG kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2014 anashauri ni vyema bajeti itumike kama nyenzo muhimu ya udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili kuleta ufanisi katika utekelezwaji wake.

Anasema kutokufuata bajeti ilivyoidhinishwa na Bunge wakati wa utekelezaji, kunasababisha uwepo wa viashiria vya ubadhirifu wa fedha za umma.