Prime
Mapya mafuta yanayodaiwa kuwababua ngozi wakazi Yombo Dovya

Muktasari:
- Wananchi walidai walipata athari za kiafya baada ya kutumia chakula kilichoandaliwa kwa kutumia mafuta hayo.
Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania(TBS), limetoa ripoti ya mafuta yanayodaiwa kuwadhuru wakazi wa Yombo Dovya zaidi ya 200 na kueleza kuwa yalikuwa na kemikali.
Tukio hilo liliripotiwa kwa mara ya mwanzoni mwa Januari, 2025 ambapo wananchi walisema walipata athari za kiafya baada ya kutumia chakula kilichoandaliwa kwa kutumia mafuta hayo, waliyodai wameyanunua kwa mfanyabiashara wa duka mtaani kwao.
Walisema athari walizozipata ni pamoja na kuumwa tumbo, kuharisha, kuvimba uso, macho kuwasha na kuwa mekundu, kutokwa na vipele, na ngozi kubabuka.

Januari 17, 2025, TBS ilieleza kufanya ukaguzi ambapo shehena ya madumu ya mafuta yaliyokutwa kwa msambazaji wa bidhaa husika maeneo ya Tandika, iliondolewa na sampuli kuchukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa kimaabara.
Mei 2, 2025 Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora, Lazaro Msasalaga alitoa mrejesho wa ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari akieleza kuwa walibaini mafuta kutoka kwa muuzaji wa jumla mtaani yalifunguliwa na hivyo kusababisha madhara hayo.
Amesema hilo lilithibitika baada ya kuchukua sampuli katika moja ya kaya zilizoathiriwa na mafuta hayo.
Hata hivyo Msasalaga ameeleza sababu ya kuchelewa kutoa majibu hayo, kuwa imetokana na kusubiri kuthibitisha majibu yanayotokana na uthibitisho wa kimaabara na kisayansi.
“Tunajua waandishi wa habari au wananchi wanapenda jambo linapotokea kupewa mrejesho ndani ya muda mfupi, lakini kuna mazingira wakati mwingine yanasasabisha ucheleweshaji
“Mfano katika sampuli tuliyochukua mara ya kwanza yalionyesha hakuna tatizo, na tukajiuliza kama hakuna tatizo wananchi wameathirika na nini ikabidi tupime kwa mara ya pili na katika upimaji huu ilibidi tupime sampuli za madumu yote 99,” amesema.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
Mkurugenzi huyo amesema katika uchunguzi huo, walifanya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu na Jeshi la Polisi na kueleza kuwa maelezo anayoyatoa yamezingatia nini taasisi hizo zilifanya kwa upande wao.
Hata hivyo amesema waligundua kuwa muuzaji anayeagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi hayakuwa na tatizo bali kwa muuzaji anayeuza kwa jumla hapa nchini.
“Kwa mlolongo huo hatuwezi kuwa na mashaka kwa mafuta yaliyoingizwa hapa nchini.Lakini baada ya hapo tulifuatilia mnyororo wa mauzo, ambapo yupo muuzaji anaitwa Ally Fadhil Ally.
“Huyu mpaka tukio hili linatokea alikuwa amebakiwa na madumu 99 ambayo tulipochunguza yalionekana kufunguliwa nakili yake na kama imefanywa hivyo kisayansi yakiingia mwanga yanakuwa yameharibika na kuwa na athari kiafya.
Akieleza hatua zainazofuata baada ya ripoti hiyo, Msasalaga amesema TBS kupitia Idara yake ya sheria itamwandikia muhusika barua na endapo muhusika atakiri kosa, kwa mujibu wa sheria ya viwango atapigwa faini isyopungua Sh20 milioni.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
Amesema endapo mfanyabiashara huyo atakataa wakienda mahakamani na mahakama ikajidhirisha atafungwa miaka isiyopungua miwili au fani ya Sh100 milioni hadi Sh150 milioni au adhabu ya vyote kwa pamoja.
Wakati TBS ikisema hivyo,Mwananchi imezungumza Ally ambaye ni mfanyabiashara anayetuhumiwa kuhusika na tukio hilo na kueleza kuwa bado hajapata barua kuhusiana na majibu ya ripoti hiyo,.
Pia amesema amesema sampuli ya mafuta waliochukua ilikuwa madumu 65 na sio 99 kama ilivyoelezwa na TBS na kueleza kuwa hayakuwa yakihusiana na waliouziwa wananchi kwa kuwa hayo aliyauza tangu Desemba mwaka 2024 na aliyamaliza ndani ya siku moja.
Walichosema wananchi
Wakizungumzia hatua hiyo, wananchi walioathirika akiwemo Razaki Shafii (20), ametaka walipwe haki inayostahili kutokana na athari walizozipata.

Alivyokuwa mmoja wa waathirika waliokula mafuta mwezi Januari, mwaka huu baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo. Picha na Nasra Abdallah
Shafii amesema kutokana na kula mafuta hayo hadi sasa macho yake hayaoni vizuri na wala hajapata msaada wowote jambo linalomfanya kushindwa kwenda kwenye shughuli zake za ujenzi.
Naye Mama Edi amesema yeye anasubiri maamuzi yatakayoamuliwa na waathirika wenzake endapo kama watafanya kikao, kwa kuwa mwenyewe hawezi kulisemea hilo kwa sasa.