Serikali yaagiza aliyeandika ‘siku za Kitima zinahesabika’ atafutwe

Muktasari:
- Tamko hilo la Serikali linatokana na tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dr Charles Kitima.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumhoji mtu aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa siku za Kitima zinahesabika.
Pia amelitaka Jeshi hilo kuwatafuta waliotengeneza na kusambaza waraka feki uliodaiwa kutolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), uliolenga kuchochea mgongano kati ya Kanisa na Serikali.
Bashungwa ametoa kauli hiyo baada ya kuwapo tukio la Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima kushambuliwa Aprili 30, 2025 kwenye makazi yake Kurasini jijini Dar es Salaam yalipo makao makuu ya baraza hilo. Padri Kitima amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.
Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo Mei 2, 2025 jijini Dodoma kwenye hafla ya kuwaaga watumishi wa umma waliostaafu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.
Amesema wizara hiyo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao kupitia vyombo vyake vya usalama.
Bashungwa amelaani kilichofanyika na kutaka mtu aliyeandika ujumbe kumuonya Kitima kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X atafutwe.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka, yule mtu aliye-tweet kwenye mitandao ya kijamii kwamba, ‘siku za Kitima zinahesabika’. Mtu huyu atafutwe haraka, ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, kwa watu wote watakaobainika kuhusika katika tukio hili,” amesema.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa viongozi wa dini nchini katika kudumisha amani, mshikamano wa kijamii na maadili ya Taifa.
“Tunalaani vikali shambulio hilo la kinyama dhidi ya kiongozi wa dini na tunamuombea Padri Kitima uponaji wa haraka na urejeaji salama katika majukumu yake muhimu kwa Taifa,” amesema.
Wakati waziri akitoa agizo hilo, kumekuwa na mijadala kutoka kwa watu mbalimbali wakihoji aliyeandika kuhusu Kitima ni hatua gani amechukuliwa hasa baada ya tukio la kushambuliwa Padri Kitima.
Bashungwa pia ameliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta waliotengeneza na kusambaza waraka feki uliodaiwa kutolewa na TEC aliosema ulilenga kuchochea mgongano kati ya Kanisa na Serikali.
“Kumekuwapo waraka feki uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukidaiwa ni waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lakini baraza kupitia taarifa yake kwa umma imekanusha kuwa waraka huo haukutolewa na TEC na kuwataka wananchi, waumini na watu wote wenye mapenzi mema kupuuza kabisa waraka huo hivyo waliosambaza nao watafutwe,” ameagiza.
Waziri amewataka watendaji wote wa wizara na vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wao kwa weledi kwa kuzingatia sheria ili kulinda amani na usalama wa nchi.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya wahalifu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi yetu,” amesema.

Vilevile amekemea vitendo vyote vinavyochafua taswira ya Taifa, vikiwamo vya kudhuru watu au kusambaza taarifa zenye kuchochea uhasama wa madhehebu ya kidini.
“Ni wakati muafaka sasa Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kusimamia sheria zinazohusu mitandao ya kijamii ili kuhakikisha watu wote wanatii sheria bila shuruti, hivyo kuendelea kuwa na jamii yenye ustaarabu na kuheshimu utu wa kila Mtanzania na hata mgeni,” amesema.
Amewahakikishia Watanzania kuwa nchi iko salama, akiwasihi kuendelea kutii sheria bila kushurutishwa ili kudumisha hali ya amani, utulivu na usalama nchini.
Bashungwa ametoa kauli wakati ambao kumekuwa na matamko kadhaa ya kulaani matukio hayo kutoka kwa vyama vya siasa, viongozi wa dini na hata mabalozi.
Wanaopaza sauti wanataka kufanyika uchunguzi wa haraka na wa kina ili hatua za kisheria kwa wote waliohusika zichukuliwe.
Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro limesema mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kwa kushambuliwa Dk Kitima na uchunguzi dhidi ya tukio hilo unaendelea.