Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais TEC asimulia shambulio la Padri Kitima, awapinga Polisi

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Rais wa TEC, taarifa zinaeleza kabla ya kushambuliwa alikuwa akipata kinywaji ni upotoshaji, badala yake shambulio dhidi yake lilifanywa alipotoka eneo la mgahawa ambalo siku zote hulitumia kwa shughuli zake.

Dar es Salaam. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amesema Padri Charles Kitima ameshambuliwa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kujeruhiwa kidevuni.

Hata hivyo, amesema taarifa zinazoeleza kabla ya kushambuliwa alikuwa akipata kinywaji ni upotoshaji, badala yake shambulio dhidi yake lilifanywa alipotoka eneo la mgahawa ambalo siku zote hulitumia kwa shughuli zake.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa

Hayo yanajiri saa chache baada ya kusambaa kwa taarifa za kushambuliwa kwa Padri Kitima, ambazo kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilifanyika alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini alikokuwa anapata kinywaji kuanzia saa 1 jioni hadi 4 na robo.

Hata hivyo, jeshi hilo linamshikilia, Rauli Mahabi anayeishi Kurasini kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo lililotokea ofisi za TEC Kurasini na uchunguzi wa kina unaendelea kwa ajili ya hatua za haraka na kali kuchukuliwa.

Taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi hilo Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro imesema: “Padri huyo inadaiwa tangu saa tatu asubuhi (jana Jumatano) walikuwa na kikao na viongozi wa dini mbalimbali na baada ya kikao kuisha saa 1 jioni alikwenda kwenye kantini yao ambapo aliendelea kupata kinywaji hadi saa nne na robo alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini hiyo ndipo alidai kushambuliwa kichwani na kitu butu na watu wawili." 


Kauli ya TEC

Akizungumza na Mwananchi leo, Alhamisi Mei 1, 2025, Askofu Pisa amesema Padri Kitima alishambuliwa eneo la karibu na mgahawa uliopo makao makuu ya TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima

Amesema eneo alikoshambuliwa ndilo ambalo siku zote hufanyia kazi zake baada ya shughuli za pamoja na hakuwa anapata kinywaji, wala si sehemu kunakopatikana kinywaji chochote.

"Ile taarifa ya polisi inayosema kuwa alikuwa anapata kinywaji kuanzia saa 1 hadi 4 na robo usiku imepotosha, ukweli hakuwa anapata kinywaji alikaa eneo la mgahawa ambalo ndilo siku zote hufanyia kazi zake," amesema.

Kwa mujibu wa Askofu Pisa, awali Padri Kitima alikuwa na mapadri wenzake kwa kikao cha pamoja na walipomaliza wenziwe waliondoka na akabaki kwenye eneo la mgahawa anakofanyia shughuli zake.

Akiwa katika eneo hilo, amesema ulifika wakati alitoka hapo kwa ajili ya kurudi ndani na kabla ya kufika kuna uchochoro wenye giza na hapo ndipo alipovamiwa na kuanza kushambuliwa.

"Ameshambuliwa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na amejeruhiwa kidevuni, ameumia sana, lakini taarifa ya Aga Khan inaeleza kwamba hali yake inazidi kuimarika hadi sasa," amesema Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi.

Kuhusu taarifa ya polisi, Askofu Pisa amesema kwa namna ilivyo inaonyesha Padri Kitima alikuwa anapata kinywaji kwa saa kadhaa, jambo ambalo kwa tafsiri ya kawaida jamii itadhani ni pombe.

"Kusema alikuwa anapata kinywaji kwa saa zote hizo ni kwamba alikuwa anakunywa pombe na pengine kapigwa na walevi, hili sio kweli tunaandaa taarifa kamili," amesema Askofu Pisa.

Amesisitiza katika eneo hilo, hakuna baa wala kinywaji na kama kuna anayehitaji kupata kilevi hicho kwa kawaida angeenda nje ya eneo hilo.

"Hakuna baa pale na hakuna sehemu ya kupata vinywaji, vinywaji tunaenda kupata kwenye baa pale ni mgahawani. Maana ukisema mtu alikuwa anakunywa kwa saa zote hizo maana yake alikuwa anakunywa pombe si hivyo," amesisitiza.