CAG: Asilimia 95 fedha za miundombinu hazikupelekwa Tanapa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini Sh21.97 bilioni, sawa na asilimia 95 hazikutolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji bajeti ya miundombinu ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) kwa mwaka 2023/2024.
Mbali na Tanapa, lakini Sh28.61 bilioni zilizoidhinishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), hazikutolewa kabisa na Serikali, licha ya Tanapa na NCAA kuiingizia Serikali mapato ya kigeni.
CAG anaonya kuwa endapo hali hiyo ikiendelea hivyo, itasababisha kuzorota kwa miundombinu inayosaidia huduma za utalii, itaathiri ukuaji wa utalii, itatatiza utoaji wa huduma, na hatimaye kupunguza mapato kwa Serikali.
Hayo yapo katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, iliyowasilishwa bungeni Aprili 16, 2025 ambapo CAG katika ukaguzi huo, alifanya mapitio ya kina katika sekta ya utalii nchini.
CAG katika taarifa hiyo, anaeleza kuwa katika ukaguzi wa usimamizi na uendelezaji wa miundombinu ya Tanapa, mamlaka hiyo ilipokea Sh1.06 bilioni tu kati ya Sh23.03 bilioni zilizoidhinishwa kwa ajili ya kazi hiyo mwaka 2023/2024.
Kiasi cha Sh21.97 bilioni hakikutolewa na Serikali kwa Tanapa, ikiwa ni asilimia 95 ya bajeti iliyoidhinishwa, licha ya juhudi za Mamlaka kufuatilia kwa Serikali.
Ukosefu wa fedha za maendeleo ulisababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maendeleo 15 yenye thamani ya Sh14.12 bilioni inayotekelezwa na Hifadhi za Taifa 10 na ucheleweshwaji huo ulianzia miezi 10 hadi 33.
Katika mapitio ya Mpango wa Mwaka wa Matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2023/24, CAG amebaini kuwa Hifadhi za Taifa 12 zina mtandao wa barabara wa kilomita 25,683.9.
Hifadhi hizo ni Serengeti, Katavi, Ziwa Manyara, Mikumi, Nyerere, Ruaha, Burigi, Arusha, Tarangire, Mkomazi, Saadani na Kilimanjaro.
“Tanapa ilipanga kufanya matengenezo ya kilomita 6,712.2 kati ya kilomita 25,683.9, lakini iliweza kutengeneza kilomita 4,022, sawa na asilimia 60 ya lengo, huku kilomita 2,690.2 hazikutengenezwa kutokana na kutopata fedha.”
CAG anasema pamoja na kutotolewa kwa fedha za maendeleo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Sh637.60 bilioni katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa niaba ya Tanapa na NCAA.
Kati ya fedha hizo, Sh410.90 bilioni zilikusanywa kutoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa na 226.70 bilioni kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
Katika NCAA, CAG alibaini Sh28.61 bilioni ziliidhinishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ambayo ilijumuisha miradi nane, ikiwamo barabara, maji, vibanda vya walinzi na mageti ya kuingilia na kutoka, lakini kiasi hicho hakikutolewa na Serikali.
CAG anapendekeza Serikali izipe kipaumbele Hifadhi za Taifa na maeneo ya hifadhi kwa kuzipa fedha za kutosha zinazohitajika kusaidia shughuli za ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya ndani ya Hifadhi za Taifa.
Haya yanajitokeza kipindi ambacho Serikali inatekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 hadi 2025/2026) ambao umelenga kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni 5 kutoka watalii milioni 1.5, ongezeko ambalo wanatarajiwa kuiingizia nchi Dola za Marekani bilioni sita.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Takwimu ya Maliasili ya Desemba 31, 2024, watalii wa kimataifa walioingia nchini mwaka 2024 walikuwa 2,141,895, sawa na ongezeko la watalii 333,690 ikilinganishwa na watalii wa kimataifa1, 808,205 walioingia 2023.
Sekta ya utalii iliingiza Dola za Marekani bilioni 3.37 mwaka 2023 na Dola za Marekani bilioni 3.9 kwa mwaka 2024 kutoka kwa watalii wa kimataifa, ikiwa ni ongezeko la Dola za Marekani bilioni 0.53, sawa na asilimia 16.
Ufinyu bajeti ya kutangaza utalii
Katika ukaguzi wake wa bajeti ya kukuza soko la utalii inayofanywa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), CAG alibaini kuwa mwaka wa fedha 2023/24 bajeti ya Bodi ilikuwa Sh4.95 bilioni kwa ajili ya kukuza masoko ya ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, Serikali ilitoa Sh3.40 bilioni, sawa na asilimia 69, huku Sh1.55 bilioni hazikutolewa, sawa na asilimia 31.
Halikadhalika CAG amebaini TTB ilipanga kushiriki katika maonesho yapatayo 212 kwa ajili ya kutangaza utalii wa kimataifa na wa ndani kama sehemu ya mkakati wake wa masoko kwa vivutio vya utalii.
Hata hivyo, kutokupatikana kwa fedha zote zilizoidhinishwa kwa lengo hilo kulipelekea Bodi ya Utalii kushiriki katika maonesho 103, sawa na asilimia 48.
CAG anasema matumizi bora ya maonesho ya utalii wa kimataifa na ule wa ndani yana mchango mkubwa katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania na matokeo yake yanaweza kuongeza mapato ya Serikali na kuongeza watalii.
Anapendekeza kuwa Bodi ya Utalii, kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, ifuatilie mara kwa mara Wizara ya Fedha ili kuhakikisha inatoa kwa wakati fedha zilizoidhinishwa za utangazaji wa utalii kwa maonesho yaliyopangwa.