Ripoti ya CAG yabaini upungufu katika usimamizi wa data za elimujiolojia nchini

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere. Picha na Maktaba.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti hiyo hadi Juni 2024,GST ilikuwa imefanikisha uchoraji wa asilimia 97 ya ramani za jiolojia ,hata hivyo theluthi moja ya taarifa hizo hazikuchapishwa hali inayodhoofisha upatikanaji wa data muhimu kwa wawekezaji na wadau wengine.
Ripoti ya ukaguzi wa utendaji kuhusu usimamizi wa data za kielimujiolojia katika sekta ya madini nchini imebaini mapungufu makubwa katika ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na usambazaji wa taarifa hizo muhimu.
Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha juhudi za Serikali za kuvutia wawekezaji na kufanikisha malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, na kuwasilishwa bungeni wiki iliyopita, imeoyesha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kwa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), bado kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa taarifa hususan kwenye ramani, tafiti za kijiokemia na jiografia ya angani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, GST hadi Juni 2024 ilifanikiwa kufikia asilimia 97 ya uchoraji wa ramani za jiolojia, lakini asilimia 35.09 ambayo ni sawa na theluthi moja ya taarifa hizo hazikuchapishwa.
Kutochapishwa kwa taarifa hizo kunadaiwa kudhoofisha upatikanaji wa data muhimu kwa wawekezaji na wadau wa sekta ya madini.
“Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 36 ya ramani za kijiolojia zilizokusanywa hazikuwasilishwa kwa matumizi ya umma kwa sababu ya ukamilifu mdogo wa taarifa, zikiwemo tafsiri za maabara na uchambuzi wa kiuchumi,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Aidha, katika eneo la tafiti za kijiolojia za kemikali, GST ilifanikiwa kufanya tafiti kwa kiwango cha asilimia 84 kwa msongamano mdogo, lakini kwa tafiti za kina (msongamano mkubwa), ni asilimia 23 pekee ya nchi yote iliyofikiwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa tafiti za msongamano mkubwa ni muhimu kwa kutambua maeneo yenye rasilimali za madini, lakini utekelezaji wake umeathiriwa na utegemezi mkubwa wa ufadhili kutoka kwa washirika wa maendeleo ambapo zaidi ya nusu ya tafiti zilizofanyika kwa kiwango hicho zilitegemea wahisani.
Kifungu cha 27A na 27B cha Sheria ya Madini Na. 123, pamoja na Mpango Mkakati wa GST wa mwaka 2020/21-2024/25, kinaitaka taasisi hiyo kuhakikisha upatikanaji na usambazaji wa taarifa za kijiolojia kwa matumizi ya Serikali, wawekezaji na umma. Hata hivyo, utekelezaji wake umeelezwa kuwa dhaifu.
Wamiliki wa leseni ya madini hawawasilishi taarifa
Ukaguzi wa CAG umebaini licha ya kanuni za benki ya Taifa ya taarifa za rasilimali za madini za mwaka 2021 kutaka wamiliki wa haki za madini (MRH) kuwasilisha taarifa za kielimujiolojia kwa GST lakini wamiliki hao hawatekelezi.
Ripoti hiyo imeeleza katika mwaka wa fedha 2021/22 ni asilimia saba tu ya taarifa ziliwasilishwa, huku mwaka 2022/23 zikiwa 12 na 2023/24 taarifa 11 pekee zikiwasilishwa licha ya kuongezeka kwa idadi ya waliosajiliwa.
“Hali hii inaashiria udhaifu mkubwa katika usimamizi wa taarifa za kielimujiolojia na inakwamisha utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22–2025/26,” imeeleza ripoti hiyo.
Upungufu wa vifaa na mafunzo kwa watendaji
CAG amebaini pia GST ilishindwa kupata vifaa vya kijiolojia vilivyopangwa kununuliwa kwa ajili ya uchambuzi na tafsiri ya data kwa mwaka wa fedha 2020/21, 2022/23 na 2023/24.
Miongoni mwa vifaa vilivyokosekana ni pamoja na vya kutambua mitetemo ardhini (seismic equipment), kompyuta ngumu za kazi ngumu (Tough Books), vifaa vya GPS na magnetometer.
Uhifadhi wa taarifa kwa njia ya Kawaida
Kwa mujibu wa ukaguzi huo wa CAG umebaini kuwa taarifa za kielimujiolojia katika GST huhifadhiwa kwa njia ya kawaida kwenye seva, pasipo mfumo wa kisasa wa kutafuta taarifa kwa vigezo maalumu.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa maofisa wa GST walikiri kutokuwepo kwa mfumo wa kisasa wa kuhifadhi na kutafuta data kwa ufanisi na kwamba mwaka wa fedha 2023/24, ilipanga kununua vifaa na programu ya kompyuta kwa ajili ya kuanzisha benki ya taarifa ya Taifa ya rasilimali za madini, lakini utekelezaji haukufanyika.
“Wakati wa ukaguzi, maofisa wa ukaguzi walishuhudia wateja wawili waliolipa fedha kwa ajili ya kupata data za maeneo ya QDS 45 na QDS 46, lakini baadaye ikagundulika kuwa data za azimio la chini kwa maeneo hayo hazikuwepo, hali iliyoonyesha mpangilio mbovu wa data,”inaeleza ripoti hiyo.
Ukaguzi na uhakiki wa taarifa za wamiliki wa leseni umezorota
Kwa mujibu wa CAG kati ya taarifa 553 zilizowasilishwa na wamiliki wa leseni za madini kwa mwaka 2023/24 ni asilimia 73 pekee zilikaguliwa huku zile za mwaka 2020/21 na 2021/22, kati ya taarifa 308 na 288 hazikufanyiwa mapitio.
Hata hivyo ripoti hiyo imeleza kwa mwaka wa fedha 2022/23, GST ilipitia taarifa zote 243 zilizowasilishwa na wamiliki wa leseni za madini.
Aidha, ukaguzi umebaini kuwa GST haikuwa na programu ya kompyuta ya kuchambua na kuchakata taarifa zilizowasilishwa, jambo lililoathiri uwezo wake wa kutoa ushauri kwa Serikali kwa wakati.
Wizara ya madini yashindwa kufuatilia utendaji wa GST
Ripoti hiyo ya CAG imeonyesha kwa kipindi cha miaka minne 2020/21 hadi 2023/24 Wizara ya Madini imefuatilia utendaji wa GST kwa mwaka mmoja tu na kueleza kuwa mipango ya ufuatiliaji haikujumuisha majukumu ya GST wala viashiria vya utendaji, na bajeti ya utekelezaji haikutolewa kwa miaka yote minne.
Mkaguzi Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa hali hiyo imesababisha wizara kushindwa kutoa mrejesho na mapendekezo ya kuboresha usimamizi wa taarifa hizo, jambo ambalo lingeweza kusaidia kufikia malengo ya Sera ya Madini ya mwaka 2009.
Ili kutatua mapungufu yaliyoonekana CAG amependekeza GST kuandaa mpango wa kitaifa wa kupanua uchoraji wa ramani na tafiti za jiokemia na jiografia ya angani katika maeneo yote nchini.
Pia, imeshauriwa kuanzisha utaratibu wa kupokea na kuhakiki taarifa kutoka kwa wamiliki wa leseni za madini, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wake.
Kwa upande wa uhifadhi wa taarifa, ripoti inapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kisasa wa usimamizi wa data, wenye uwezo wa kuorodhesha, kugawanya na kutafuta taarifa kwa ufanisi.
CAG ameishauri Wizara ya Madini kuweka mpango wa ufuatiliaji wa utendaji wa GST, ikiwemo viashiria vya kupima mafanikio na kuripoti maendeleo kwa wakati.