Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TEC: Shambulio la Padri Kitima linagusa maeneo matatu

Muktasari:

  • Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limesema shambulio dhidi ya Katibu Mkuu wake, Padri Charles Kitima lililolenga uhai wake halikuishia kumuumiza yeye pekee, bali ni uvamizi wa baraza hilo la kiroho na limejeruhi heshima ya Taifa.

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesema shambulio dhidi ya Katibu wa Baraza hilo, Padri Charles Kitima, licha ya kumuumiza yeye, pia baraza hilo limeshambuliwa na heshima ya Taifa imejeruhiwa.

Kauli hiyo imetolewa katika salamu za TEC zilizotolewa na Makamu wa Rais wa Baraza hilo, Askofu Eusebius Nzigilwa leo Jumapili Mei 4, 2024 katika misa ya kumsimika Askofu wa Jimbo Jipya Katoliki la Bagamoyo, Askofu Stephano Musomba.

Hili ni tamko la pili la TEC, baada ya tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wake, Padri Kitima, lililotokea Makao Mkuu ya baraza hilo, Kurasini jijini Dar es Salaam huku ukitolewa wito wa uchunguzi wa haraka.

Wakati TEC ikisema hayo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo amesema Serikali imepokea rai ya baraza hilo na mamlaka husika zinaendelea kuwatafuta ili kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika na shambulio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, kiongozi huyo wa kiroho alishambuliwa kichwani na watu wawili kwa kitu butu, alipokwenda maliwatoni, akitokea kwenye mghahawa wa TEC, alikokuwa amekaa kwa saa kadhaa.

Jeshi hilo linamshiklia mkazi wa Kurasini, Rauli Mahabi kuhusiana na tukio hilo lililotokea Aprili 30, 2025 huku Padri Kitima akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa ameagiza uchunguzi na hatua kwa watakaohusika, pia ametaka akamatwe mtu aliyeandika ujumbe kuwa ‘siku za Kitima zinahesabika’ katika ukuraza wake wa X (zamani twitter).


Alichosema Askofu Nzigilwa

Akitoa salimu katika misa ya kumsimika Askofu Musomba na uzinduzi wa Jimbo la Bagamoyo, Askofu Nzigilwa amesema si lengo la baraza hilo kueleza namna tukio lilivyotokea, bali wanajiuliza waliohusika walilenga kumshambulia Padri Kitima, Baraza la Maaskofu au Taifa.

“Tunatafakari na kujiuliza ni nini hasa kinachoshambuliwa kwa tukio kama lile. Je, anashambuliwa mtu, taasisi au taifa,” amehoji na kufafanua kuwa maeneo matatu yameshambuliwa na kujeruhiwa.

 “Shambulio lile halikuwa la watu waliotaka kumpora mali au fedha, bali lilikuwa ni shambulio la watu waliotaka kumpora uhai wake, uhuru na haki yake ya kuishi, kusema na kutenda kadiri ya dhamiri, imani na wito wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu,” amesema Askofu Nzingilwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda.

Ameongeza kuwa shambulio alilofanyiwa Padri Kitima ni dhidi ya heshima na sifa ya Taifa na kwamba waliofanya hivyo wanaivunja heshima ya Tanzania inayojulikana kuwa kisiwa cha amani na umoja.

“Shambulio hilo limewapa watu nafasi ya kutukejeli na hata kuwasema vibaya viongozi na vyombo vyetu vya usalama. Tunaomba basi, mamlaka na vyombo vinavyohusika walifanyie kazi jambo hili kukomesha maovu haya ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika nchi yetu,” amesema.

Kuhusu hali ya Padri Kitima, amesema anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Askofu huyo ameshukuru hatua ya Waziri Bashungwa kulichukulia suala hilo kwa ukubwa na kuwa Watanzania wanataka kuona wahusika wanachukuliwa hatua.

“Tunawaomba waamini na wote wenye mapenzi mema tumwinulie Mungu mioyo yetu kwa sala na maombi, tumwombe Mwenyezi Mungu atujaalie haki, amani, uhuru, upendo na umoja vistawi tena katika nchi yetu na Mungu mwenye uwezo wote atuondolee vyote vinavyotuzuru,” amesema.

Ametaka wote wanaopanga, kufadhili na kutekeleza maovu hayo, wajaaliwe neema ya toba ya kweli ili waepukane na adhabu ya milele.

“Tunaomba mamlaka na vyombo vinavyohusika walifanyie kazi jambo hili kukomesha maovu haya ambayo yamekuja yakijirudia mara kwa mara katika nchi yetu,” ameeleza.


Kauli ya Serikali

Katika hafla hiyo, Dk Mpango ambaye amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeshaagiza mamlaka zinazohusika kuchukua hatua dhidi ya wahusika wa tukio hilo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia mara baada ya Misa ya Kumsimika Askofu wa Jimbo Jipya Katoliki la Bagamoyo Mhashamu Askofu Stephano Lameck Musomba pamoja na Sherehe ya Uzinduzi wa Jimbo hilo iliyofanyika katika  Uwanja wa St. Mary Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani leo  Mei 04, 2025.


Pamoja na kulaani na kukemea tukio hilo na mengine, amesema Serikali imepokea kwa unyenyekevu rai iliyotolewa na kanisa kupitia Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Nzigilwa.

"Napenda niwahakikishe Watanzania, wapenda haki, amani na usalama, kwamba tayari Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, imeviagiza vyombo vya dola kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria waliohusika,” amesema.

“Nawaomba sana wahashamu maaskofu, wakleri na wote walioumizwa na tukio hili baya, kujikabidhi kwa Mungu pale tunapoumizwa na udhalimu, kama tunavyosoma katika Waraka wa Kwanza wa Petro (1 Pet. 2:19 ).

...maana huu ndiyo wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu pale ateswapo isivyo haki”.

Aidha, nawasihi sana Watanzania tuendelee kupendana na kusimama pamoja kulaani matendo hayo mabaya, yasiyoakisi Tanzania yetu inayosifika kama kisiwa cha amani,” amesema.

Sambamba na hilo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika mambo mbalimbali, ili kuleta amani ya taifa.

Vilevile amewasihi wananchi wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.

Katika hatua nyingine, Dk Mpango amesema Rais Samia ametoa Sh20 milioni kwa Askofu Musomba, kwa ajili ya kusaidia gharama za mafuta ya gari katika mizunguko yake ya kichungaji.


Uongozi si kutumia nguvu

Awali, katika mahubiri aliyoyatoa Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Lazarus Msimbe, amesema ni muhimu kukumbuka uongozi wa kweli si kutumia nguvu au kulazimisha watu wafuate mawazo yako hata kama ni mabaya.

Badala yake, amesema uongozi ni kuwaongoza watu kupitia matendo ya maadili na kwamba kiongozi huongoza kwa mfano na kukuza mazingira ya uaminifu, heshima na ushirikiano.

“Viongozi wanapoonyesha uadilifu wanakuwa mfano kwa wengine kumfuata, hivyo wajitahidi kukuza mitindo yao ya uongozi kwenye jamii badala ya kutumia mamlaka,” amesema.

Askofu huyo amesema ni muhimu kusimamia ukweli daima kwani ndio huwafanya watu kuwa huru, akitolea mfano, mitume na makuhani waliomsikiliza Yesu Kristo na kumfuata.

Kuhusu maadhimisho hayo, amesema viongozi hao wameridhia kulisha kondoo sio kwa mkate na ekaristi pekee, bali kimwili kwa kuwasaidia wasiojiweza, wagonjwa na wazee kwa heshima na kuwaimarisha wanyonge kwa utetezi na kuwatia moyo waliokata tamaa.

“Kile tunachoadhimisha lazima kionekane katika maisha yetu, kama katika ekalisti tunashiriki mwili na damu ya Kristo lazima tuende kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu,” amesema.

Askofu Msimbe amehitimisha mahubiri yake kwa maneno ya Mtakatifu Augustino akisema maisha ya kila siku watu wahakikishe waliokata tamaa wanatiwa moyo, walio dhaifu wasaidiwe, wapinzani wa injili waelekezwe, wajinga wafundwe, wachochezi waangaliwe kwa makini na kunyamazishwa.

“Wenye majivuno wafundishwe unyenyekevu, wanaogombana wapatanishwe, masikini wasaidiwe wanaonyanyaswa wakombolewe, watu wema wapongezwe, watu wabaya waonywe na watu wema wapendwe,” amesema.


Alichokisema Askofu Musoba

Kwa upande wake, Askofu Musomba baada ya kusimikwa amesema kazi kubwa iliyobaki ni kushirikiana na kushikamana kwa upendo kujenga jimbo hilo jipya na kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake.

"Tuongozwe na maneno matatu, uwazi, uwajibikaji na wajibu, tusije kukimbia kivuli chetu hasa pale tunapokosolewa bali tuwe tayari kukosolewa na kujirekebisha mara kwa mara," amesema.

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa'ichi amewaomba wananchi wa Bagamoyo kujenga umoja kama jimbo bila kutazama maeneo waliyotoka, bali watambue wao ni kanisa moja takatifu Katoliki la mitume.

“Katika kujitambua hivyo muwe makini kulipenda jimbo lenu na kulishughulikia, zama hizi hatuna tena wajomba Ulaya, wajomba wa uinjilishaji kwetu ni sisi wenyewe, kwa hiyo naomba mshikamane mjenge jimbo lenu na sisi tuliowazaa tutawapa mshikamano wa dhati muimarike na kuwa kanisa linaloheshimika," amesema.

Amesema katika umri wake wa uaskofu ameshuhudia kuzaliwa kwa majimbo, ikiwemo Jimbo la Kondoa lililozaliwa likiwa na Parokia 10, tofauti na Bagamoyo ambalo limezaliwa likiwa na Parokia 27 na Parokia teule tatu.