CCM yalaani shambulio la Padri Kitima, Polisi yaagizwa

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimelaani shambulio dhidi ya na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima kikisema ni tukio la kihalifu.
Chama hicho kimekwenda mbali na kutoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wote wa shambulio dhidi ya kiongozi huyo wa dini wanatiwa nguvuni.
Kwa sasa, Padri Kitima amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam baada ya kushambuliwa na kitu butu kichwani usiku wa jana Jumatano, Aprili 30, 2025. Shambulio hilo lilitokea eneo la Kurasini Temeke, Dar es Salaam, ziliko ofisi za TEC Makao Makuu.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wanamshikilia Rauli Mahabi, mkazi wa Kurasini Dar es Salaam akituhumiwa kuhusika na tukio hilo lililotokea saa 4:15 usiku, alipokwenda maliwatoni pembeni ya kantini alipokuwa akipata kinywaji kuanzia saa 1 jioni.
Kamanda Muliro amesema Padri Kitima alishambuliwa kichwani na kitu butu na watu wawili. Uchunguzi wa kina unaendelea ili hatua kali na za haraka zichukuliwe kwa wahusika.
Leo Alhamisi, Mei 1, 2025, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira ametumia ukurasa wake wa X kulaani tukio hilo.
“Kama M/Mwenyekiti CCM (Bara), nimepokea kwa masikitiko taarifa ya tukio la kihalifu dhidi ya Pr. Dkt. Kitima katika ofisi za Baraza la Maaskofu. Natoa pole zangu na kulaani kitendo hiki. Polisi wafanye uchunguzi wa kina, kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria.