Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi kuchunguza tuhuma askari kuhusishwa kupotea kwa mdude

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limetangaza kuchunguza tuhuma za kuhusika kwa askari katika tukio la kupotea kwa mwanaharakati na kada wa Chadema, Mdude Nyagali huko mkoani Mbeya.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetangaza kuchunguza tuhuma za kuhusika kwa askari katika tukio la kupotea kwa mwanaharakati na kada wa Chadema, Mdude Nyagali huko mkoani Mbeya.

Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia Mei 2, 2025 saa 8:00 Mdude akiwa amelala nyumbani kwake Mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi, jijini Mbeya, watu wasiojulikana walimvamia kwa kuvunja mlango, wakaingia ndani na kisha kumjeruhi kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kutokomea naye.

Hata hivyo baada ya tukio hilo kuzua sintofahamu Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilikanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa askari wake wanahusika katika tukio hilo.

“Taarifa hizo siyo za kweli na zinalenga kupotosha umma kuhusu uhalisia wa tukio hilo ambalo bado linaendelea kuchunguzwa’”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, alitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Mei 2, 2025.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi Dodoma leo Jumapili Mei 4, 2025 tuhuma za kuhusika kwa askari katika tukio hilo zimetolewa na mwananchi mmoja ambaye jina lake linaendelea kufuatiliwa.

Mwananchi huyu amewatuhumu askari wawili kupitia mitandao ya kijamii kuwa walimfuata kumtaka afanye nao kazi ya kijajusi pamoja na kumuahidi kumpatia fedha.

Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai limeunda kikosi kazi ambacho tayari kimeshafika mkoani Mbeya kwa ajili ya uchunguzi juu ya suala hilo.

"Wakati uchunguzi juu ya suala hilo ukiendelea, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi, yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kubaini ukweli juu ya suala hili atoe ushirikiano kwa kutoa taarifa hizo.”

Aidha, tukio hilo limeibua mapya ikiwemo kitendo cha viongozi na wafuasi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya kuanzisha jitihada za kumtafuta katika maeneo ya porini,  kisha kuandamana hadi ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoani humo wakitaka kupata taarifa zaidi.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana, Jumamosi, Mei 3, 2025, Kamanda Kuzaga alisema uchunguzi unaendelea, akibainisha kuwa kikosi kazi maalumu, kikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, kinafanyia kazi tukio hilo.

“Tunaendelea na uchunguzi. Naomba wananchi watulie na washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kupatikana kwa Mdude Nyagali na kuwabaini waliomteka,” alisema Kamanda Kuzaga.