Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hekaheka saa 72 barabara Dar- Kusini ilivyokatika na kurejeshwa

Muktasari:

  • Mawasiliano ya barabara ya Dar kwenda mikoa ya Kusini yaliyokatika na kuleta adha kwa watumiaji yamerejea kwa kutengenezwa njia ya dharura na sasa magari yanapita.

Lindi. Zaidi ya saa 72 zimetumika kurejesha mawasiliano ya barabara ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini iliyokatika Aprili 6, 2025 kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Kufuatia mvua hizo, mawasiliano yalikatika huku baadhi ya madaraja kubomoka likiwamo la Somanga-Mtama na la Mto Matandu ambalo awali liliharibiwa na mvua zilizoambatana na Kimbunga Hidaya, Mei 5, 2024.

Daraja la Somanga-Mtama lilikatika saa 12 asubuhi Aprili 7, 2025 huku Daraja la Mto Matandu lilikatika na kufunga mawasiliano kwa mikoa ya Lindi-Mtwara.

Kukatika kwa mawasiliano hayo kwa muda huo kumesababisha adha kwa watumiaji wa barabara hiyo ambapo awali walilazimika kungoja hatua ya Serikali kuanza kurejesha taratibu.

Akizungumza leo Alhamisi Aprili 10, 2025 alipotembelea na kujionea maendeleo ya urejeshwaji wa barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema kwa hatua iliyofikia sasa magari yanapita.

Amesema mvua zilizonyesha zimeleta madhara na wataalamu na mafundi wamepambana kurejesha mawasiliano kwa haraka ili kuondoa adha kwa wananchi wanaoitumia barabara hiyo.

Amesema tayari mawe yamewekwa katika maeneo yote korofi na ujenzi unaendelea.

“Hatua ya kwanza waliyoifanya wataalamu ni pamoja na kuleta mawe makubwa zaidi ya gari 100 kutoka Dar es Salaam, yakawekwa juu ili kuruhusu msururu wa magari yaliyokwama yapite,” amesema Ulega.

Amefafanua kuwa mafundi pia wamejenga barabara ya muda iliyowekewa karavati za chuma zinazopitisha maji chini, itakayotumika mpaka msimu wa mvua utakapomalizika.

“Aidha zaidi ya Sh100 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza madaraja 11 na makaravati 18 kuanzia hapa Somanga, maeneo yote haya yana makandarasi wanaoendelea na ujenzi kwa  hatua mbalimbali,” amesema waziri huyo.

Waziri Ulega amesema fedha hizo zilizotolewa zitajenga daraja la Somanga lenye urefu wa mita 60 sawa na zaidi ya nusu ya kiwanja cha mpira.

"Mkandarasi anayejenga hapa Somanga, daraja lina jumla ya nguzo 43 na ameshazamisha chini nguzo 26 zimebaki 17. Hali hii ya mvua imetukuta wakati makandarasi wanaendelea na ujenzi," amesema Waziri Ulega.

Hata hivyo, amekiri kuwa barabara hiyo wakati inajengwa haikutarajiwa kubeba mizigo mizito.

"Tutakata vipande vilivyoharibika na kuanza kutengeneza upya hadi barabara hii ikae sawa," amesema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Mohamed Besta amesema kwa sasa sehemu zote mbili zinapitika, “kwa maana gari za kwenda na kurudi.”

"Lakini pia na makandarasi wa kazi za dharura wanaendelea kumwaga zege, maendeleo ni mazuri,” amesema Besta.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema mkoa huo umepata mafuriko kwa kuwa ndio unaopokea maji kwenda baharini.

"Mkoa huu unapokea maji mengi kutoka mikoa mingine hata kama hauna mvua ndio maana kumetokea changamoto hii," amesema.


Ulega akabidhiwa rungu

Katika hatua nyingine Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amemtaka Waziri Ulega, kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji wazembe ndani ya wizara hiyo.

Kauli ya Makalla inakuja alipokuwa kwenye ziara hiyo akiungana na Ulega na viongozi wengine wa Tanroads na mkoa wa Lindi hii leo.

Makalla amemtaka Ulega kuwa mkali huku akila sahani moja na watendaji wanaoleta uzembe.

Amepongeza juhudi za Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo ya kuhakikisha wanarejesha mawasiliano kwa haraka.

“Tumekesha kwa siku tatu kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa. Nimeridhishwa na kazi inayofanyika, na Waziri Ulega unaelekea vizuri. Hakikisha kazi inaendelea kwa kasi ili wananchi wetu waendelee na maisha, hata msimu mwingine wa mvua ukija, barabara zetu ziwe imara,” amesisitiza Makalla.

Athumani Zarahani, dereva wa lori aliyekuwa akitokea mkoani Lindi kuelekea Dar es Salaam baada ya kupita Somanga, amesema hakutarajia kama angeweza kupita kutokana na taarifa alizopata awali kuwa pamekatika.

"Nimefurahishwa japokuwa tunapita kwa kusubiriana ni heri kuliko kutopita kabisa. Naomba Serikali iharakishe ujenzi wa daraja, huku tunasafirisha bidhaa nyingi," amesema alipozungumza na Mwananchi.