Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua za masika zaacha maumivu mikoa mitatu

Dar/mikoani. Mvua za masika zimeendelea kuleta maumivu kwa watumiaji wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini, huku baadhi ya maeneo yakishindwa kufikika kutokana na uharibifu.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kuilaumu Serikali, wakidai licha ya majanga hayo kujirudia kila mwaka, hakuna mpango endelevu wa kudhibiti madhara hayo.

Hali hii inajitokeza ikiwa ni wiki ya pili tangu mvua za Masika zianze kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, huku zikiacha madhara mbalimbali, ikiwemo kusombwa kwa madaraja.


Dar yatenganishwa na kusini

Kutokana na mvua hizo, safari ya kwenda na kurudi Dar es Salaam kutoka mikoa ya kusini zimekwama kwa saa kadhaa, baada ya kusombwa kwa daraja la Sombanga-Mtama linaloiunganisha mikoa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), imeruhusu mabasi yasafiri kwa njia ya dharura kati ya Dar es Salaam - Lindi - Mtwara - Masasi - Tunduru kupitia njia ya Songea, Makambako na Iringa tangu juzi

Pamoja na hatua hiyo, leo Jumanne April 8, 2025, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mawasiliano ya barabara hiyo kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini yamefunguka baada ya matengenezo ya dharura.

Kwa hatua ya sasa, amesema magari yatakayopita ni yale madogo na ya abiria, lakini baadaye ukarabati utafanyika ili yale makubwa ya mizigo yaweze kuruhusiwa.

"Kuanzia sasa barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini imefunguka rasmi lakini magari yanayopita ni madogo na yale ya abiria," amesema.

Baadhi ya wananchi wamesema pamoja na kufunguka kwa barabara hiyo, ni vema Serikali iangalie upya matengenezo ya dharura inayoyafanya ili matatizo yasijirudie.

Wakazi wa Mwanza wakiwa pembezoni mwa Daraja la Mkuyuni jijini Mwanza lililojaa maji kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini humo. Picha na Mgongo Kaitira

"Hii barabara ina madaraja mengi, kwa hiyo Serikali ijitahidi katika kujenga madaraja bora ili yasilete madhara tena," amesema Rajabu Omary.

Katika mikoa hiyo,  mbali na Daraja la Somanga-Mtama lililokatika Aprili 6, lingine la Mto Matandu lilikatika Aprili 7  na kusababisha adha kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji.

Kama ilivyo katika mikoa hiyo, mkoani Mwanza nako, Daraja la Mkuyuni jijini humo limevunjika na kukwamisha wananchi kuingia katikati ya Jiji hilo, baada ya mvua iliyonyesha kuanzia 9:30 usiku wa kuamkia leo Aprili 8, 2025.

Akizungumzia kadhia hiyo, Mkazi wa Mkuyuni, Charles Lulinga amesema mafuriko hayo yamesababishwa na ufinyu wa mitaro katika daraja hilo, ambalo upanuzi wake ulianza Januari mwaka huu, lakini bado haukuwa umekamilika.

Amesema ni muda mrefu magari ya mkandarasi yameshuhudiwa katika eneo hilo, bila kuona maendeleo yoyote ya ujenzi wa daraja.

“Ni kweli mkandarasi tunamuona hapa anajenga lakini hatuoni mabadiliko yoyote hadi muda huu mvua zimeanza kunyesha tena… Serikali iingilie kati hili suala hili daraja limeshatuchosha,” amesema Lulinga.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Pamba jijini Mwanza, Victoria Fredrick amesema kutokana na daraja hilo kufurika amechelewa kwenye mitihani ya kujipima shuleni.

“Imeniathiri kwa sababu hatujaenda shule hadi muda huu (saa 3:20) asubuhi na tulikuwa na mitihani, kwa hiyo tunaomba Rais wetu  atusaidie waliinue, ili tusiwe tunapata changamoto kuvuka kila mvua inaponyesha,” amesema.

Mwendesha pikipiki maarufu kama bodaboda akipita juu ya daraja lililofurika la maji la Mkuyuni jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira



Amesema wapo watu wanaotozaSh500 kuwabeba watu mgongoni kuwavusha, lakini wanafunzi wanashindwa kumudu gharama hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema wamefanikiwa kuwadhibiti waliokuwa wakilazimisha kuvuka juu ya daraja hilo lililofurika maji, jambo ambalo linahatarisha maisha yao.

Pia, amewataka wenye magari kutumia barabara mbadala kufika mjini, hususan ya Sahwa na Usagara kupitia Kisesa hadi katikati ya jiji hilo, ili kuepuka kupoteza muda kwenye foleni iliyosababishwa na mafuriko hayo.

“Tuko hapa tangu saa 11 alfajiri baada ya mvua kupungua na tulipopewa taarifa kuwa kuna foleni hapa. Bado hatujapata taarifa ya maafa yoyote kwa raia au mali, ila tunachohimiza ni kwamba wananchi wasilazimishe kuvuka wanapoona maji yamekata barabara,” amesema kamanda Mutafungwa.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza, Pascal Ambrose amethibitisha daraja hilo kufurika, huku akiomba radhi kwa wananchi kutokana na changamoto hiyo.

“Wenzetu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) katika kujenga mradi wao wa SGR walijenga tuta kubwa, kwa hiyo linakusanya maji na kuyapitisha sehemu moja. Kwa hiyo yale maji yote yanalazimika kupitishwa katika daraja hilo la Mkuyuni, ambalo uwezo wake ni mdogo kwenda Ziwa Victoria,” amesema.

Kwa kutambua changamoto hiyo, amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa daraja hilo ulioanza Desemba 2024, kwa gharama ya Sh5.5 bilioni, likitarajiwa kukamilika Novemba 2025.

“Huo mradi unahusisha upanuzi wa daraja na ujenzi wa barabara kwa urefu wa mita 500 kila upande. Kwenye ujenzi lazima kuna adha zinajitokeza tunawaomba samahani, lakini hapo tutakapokuwa tumekamilisha ujenzi wa hilo daraja, tutasahau yote haya,” amesema.

Mwakilishi wa Kampuni ya Jasco inayotekeleza ujenzi huo, Nestory James amesema ujenzi wake umesuasua kutokana na mchoro wa awali kuonekana kutofaa, hivyo wamelazimika kuuboresha mchoro huo.

“Awali, usanifu ulionekana kuwa lijengwe daraja la kawaida lakini kutokana na changamoto ya maji kuwa kubwa tumelazimika kuchora mchoro mwingine na tayari umekamilika wiki hii ujenzi utaendelea,” amesema.

Amesema mradi huo utakapokamilika utawezesha kingo za mto na daraja hilo kuinuliwa, jambo litakaloondoa kabisa changamoto ya mafuriko kwenye eneo hilo na kutoa fursa kwa wananchi kupita bila kikwazo chochote wakati wa masika.

Morogoro nako si shwari

Wakati huohuo, Hali ya baadhi ya barabara si shwari katika Mkoa wa Morogoro kutokana na mvua hizo, kuna maeneo yasiyopitika kutokana na mashimo makubwa yaliyojitengeneza barabarani.

Mmoja wa wananchi anayetumia chombo cha moto, Maurus Dihindila amesema mvua hizo zimeongezea uharibifu, kwa kuwa barabara hizo zilishakuwa mbovu tangu awali.

"Hizo barabara tangu mwaka jana zinapitika kwa shida na kuna nyingine huwezi kupita na gari wala bodaboda, mvua za mwaka jana zilivyoisha tukajua Tarura watakarabati lakini hadi mwaka huu hakuna kilichofanyika,” amesema.

"Barabara zilizoharibika ni nyingi karibia kata zote zina changamoto, lakini yapo maeneo kwenye mitaa mingine hayafikiki kwa usafiri wa gari. Barabara zimechimbika, zimeweka matuta na mifereji katikati na hatujui lini zitakarabatiwa maana mvua nazo ndio zimechanganya,” amesema.

Rahma Athumani mkazi wa kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro, amesema kilio chake ni Barabara ya Mazimbu eneo la Kwa Bwana Jela ambako lami ilisombwa na mvua za mwaka jana na hadi sasa hakuna matengenezo.

Akizungumzia hilo, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amekiri kuwepo uharibifu wa miundombinu ya barabara uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

“Kwa sababu hiyo, tumeona halmashauri tuwe na katapila letu wenyewe kwa ajili ya kuchonga barabara za kwenye mitaa, na tayari tumenunua greda kwa Sh1.3 bilioni na lipo hapa manispaa," amesema.

Amesema wanasubiri mvua zipungue au kuisha ili kazi ya kuchonga barabara ianze na hivyo amewataka wananchi wawe wavumilivu.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira (Mwanza), Nasra Abdallah (Dar), Hamida Shariff (Moro) na Bahati Matesa (Lindi).