Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tishio la mbwakoko -1

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa utafiti asilimia 20 pekee ya mbwa nchini Tanzania wanafungwa au wamejengewa vibanda ili wasizurure, ilhali asilimia 80 wanazurura hovyo mitaani bila udhibiti wowote.

Dar es Salaam. Ni saa moja asubuhi, Loyce John msichana wa miaka 12 anatoka nyumbani kuelekea shuleni kupitia barabara nyembamba ya vumbi.

Barabara hii ipo katika Mtaa wa Kisimani, Kata ya Kibamba wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam. 

Kando mwa barabara kuna vibanda vichache vya biashara, nyumba na sehemu ni vichaka.

Ghafla inasikika milio ya mbwa nyuma, aligeuka kwa haraka, macho yake yakakutana na kundi la mbwa watano waliodhoofika, wakimkodolea macho.

Akiwa mwenye hofu aliongeza mwendo, mbwa nao wakamfuata. Moyo ukidunda kwa kasi asijue la kufanya, bahati walitokea vijana watatu waliokuwa wakielekea kwenye majukumu yao ya kazi waliowafukuza mbwa hao.

Loyce akiwa anatetemeka, anasema alijua ndiyo mwisho wa maisha yake, sababu ikiwa tatizo linaloshika kasi la mbwa kuzurura mitaani.

Tatizo hili haliko katika mtaa wa kina Loyce pekee, limeshuhudiwa katika mitaa kadhaa nchini mijini na vijijini zaidi asubuhi na jioni watoto wanapokwenda shuleni na kurudi nyumbani.

Katika matukio ya watu kung’atwa na mbwa, zaidi ya nusu yanawahusu watoto chini ya miaka 15 wanaoathirika zaidi wakiwa waishio vijijini.

Watoto hushambuliwa zaidi kutokana na hali zao hivyo kushindwa kupambana na wanyama hao.

Ufuatiliaji uliofanya na Mwananchi katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Geita unadhihirisha hali hiyo.


Kuhusu utafiti

Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Maganga Sambo anasema asilimia 20 tu ya mbwa nchini Tanzania wanafungwa mnyororo au wamejengewa vibanda ili wasizurure, ilhali asilimia 80 wanazurura hovyo mitaani bila udhibiti wowote.

“Kati ya mbwa hawa, asilimia 95 wanamilikiwa, lakini asilimia tano tu hawana wamiliki. Sababu ya mbwa wanaomilikiwa kuzurura ni ukosefu wa matunzo bora, kama chakula cha kutosha, hivyo wanalazimika kujitafutia riziki mitaani. Ndiyo maana mbwa hawa huzurura mchana na kurudi nyumbani usiku,” anasema.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, Mei 21, 2024 akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Yustina Rahhi alisema Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na mbwa 302,879 kati ya milioni 2.77 waliopo nchini.

Alisema taarifa ya sampuli ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2020, ilikadiriwa kuwa na mbwa milioni 2.77 nchini.

Mnyeti alisema kupitia taarifa hiyo mikoa iliyoongoza kwa mbwa wengi mbali ya Geita ni Mwanza yenye mbwa 287,270 na Tabora 243,768.


Wasemavyo wananchi

Mkazi wa Mtaa wa Ibanda, jijini Mwanza, Dickson Marekani amesema: "Kuna baadhi ya familia zinazomiliki mbwa hazina uwezo wa kuwatunza, ndiyo maana wengi wanazagaa mtaani hivyo kuhatarisha maisha ya watoto na wananchi kwa ujumla."

Mama lishe jijini Mwanza, Magreth Joseph anasema amekuwa akipata shida kuzuia mbwa wanaosogea kulamba vyombo katika mgahawa wake, jambo linalomweka katika hatari ya kukosa wateja.

"Mara nyingi mbwa wamekuwa wakitangatanga wakati tunapika wanalamba vyombo, hii yote ni kutokana na wanaowafuga hawawapi chakula. Wakati mwingine unakuta wana magonjwa, sipendi kuwaona katika mazingira yetu kwani tunashindwa namna ya kuwazuia,” amesema.


Kuhusu sheria

Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza ambaye pia ni daktari wa mifugo, Nelson Lugaimukamu amesema ufugaji wa mbwa ni utamaduni wa tangu enzi katika jamii za Kiafrika, dhamira yake ikiwa kuimarisha ulinzi.

Amesema: "Hatuna sheria inayozuia mbwa wanaozurura mtaani ila kuna Sheria ya Ustawi wa Wanyama ambayo inazungumzia mnyama atunzweje na apateje mahitaji yake ya kila siku."

Ofisa Mifugo mkoani Mwanza, Candidah Kyamani akizungumzia hatua za udhibiti wa mbwa walio mitaani na adhabu kwa wamiliki wa mifugo hiyo wanaowaacha wazurure mitaani Kyamani amesema:

“Kwa kawaida mbwa walio wengi wanamilikiwa isipokuwa wamiliki wanaposhindwa kuwapatia huduma zao za msingi (malazi na chakula) ndipo wanapotoka kwenda mitaani kutafuta chakula.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 amesema wamiliki wa mbwa na paka wanatakiwa kuwatunza wanyama hao kwa kuwapatia chakula, malazi na kuhakikisha wanafungiwa katika nyumba imara kwa ajili ya kuwazuia kuzurura, kwani wanaweza kuleta madhara kwa binadamu na hata mifugo mingine.

"Iwapo mbwa atapatikana katika mazingira ambayo hatakiwi kuwapo (anazurura) na mmiliki akafahamika, mmiliki atatakiwa kulipa faini fedha au kifungo kulingana na matakwa ya sheria ndogo zinazotumika katika mamlaka za serikali za mitaa za kusimamia udhibiti wa wanyama wafugwao,” amesema.

Daktari wa Mifugo Mkoa wa Geita, David Mitungi anasema halmashauri zimeweka sheria ndogondogo ambazo wamiliki ambao mbwa wao wanazurura hovyo mtaani wanakumbana na faini ya kati ya Sh50,000 hadi Sh300,000.

Ofisa Mifugo Kyamani amesema mbwa wanaozurura na wamiliki hawajulikani huondolewa (kuuawa) kwa utaratibu maalumu.

Katika hilo, Kaimu Ofisa Mifugo na Uvuvi, Wilaya ya Sengerema, ambaye pia ni daktari wa mifugo, Jacob Kamamila anasema kwa kushirikiana na wataalamu waliwapumzisha (kuwaua) mbwa wanaozurura mtaani, akieleza tangu Januari 2025 wamefanya kazi hiyo katika kata za Nyatukala, Nyampulukano, Mission na Sima. Waliopumzishwa anasema wamefikia 126.

Hali hii inayoshuhudiwa mitaani ni matokeo ya kukiukwa Sheria ya Ustawi wa Wanyama Na. 19 ya 2008, Sehemu ya III, Kifungu cha 16(1) kinachowawajibisha wamiliki kuwatunza wanyama wao, ikiwa ni pamoja na kuwapa chanjo. Kifungu cha 57(1) kinatoa adhabu kwa wanaokiuka sheria hii.

Kwa mujibu wa vifungu hivyo vya sheria, mfugaji wa mbwa anatakiwa kuhakikisha anamfunga, anamjengea banda bora la kumfungia wakati wote wa mchana na awe na mnyororo madhubuti.

Endapo mbwa anasafirishwa kutoka eneo moja kwenda lingine, lazima awe amefungwa kwa mnyororo madhubuti, wapatiwe chakula cha kutosha na wakingwe dhidi ya vimelea vya magonjwa.

Mbwa wanapaswa kupatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa kila mwaka, kuwekwa bango linalotoa tahadhari kwa wananchi kuwa kuna mbwa mkali kwenye eneo husika.

Kutoa taarifa kwa mganga wa mifugo wa kata, pindi mbwa anapoonyesha mabadiliko ya tabia ili kupata huduma stahiki na kuchukua tahadhari, kutoa taarifa kwa mganga wa mifugo wa kata pindi mbwa anapokufa, kuuzwa au kumilikiwa na mfugaji mwingine.

Kila mfugaji wa mbwa anaponunua au kuingiza mbwa mgeni inampasa kumsajili kwa mganga wa mifugo wa kata.

Sheria inatoa mamlaka kwa serikali za mitaa kuchukua hatua za kudhibiti wanyama wanaozurura, wakiwamo mbwa na kuchukua hatua za haraka kudhibiti magonjwa yanayoambukiza, ikiwa ni pamoja na kuteketeza wanyama waliothibitika kuwa na magonjwa hatari.

Sheria nyingine inayokiukwa ni ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya Mwaka 2003.


Madhara yanayojitokeza

Mbwa kuachwa kuzurura mtaani pia kunavunja haki itolewayo na Ibara ya 17 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kila raia kwenda kokote na kuishi katika sehemu yoyote.

Kwa mujibu wa Paulina Nchimbi, mkazi wa Gogoni, Kata ya Kibamba wilayani Ubungo, Dar es Salaam anashindwa kuhudhuria misa za asubuhi kanisani kwa miguu kutoka na uwepo wa mbwa wanaozurura mtaani.

Paulina ambaye ni mzee aliyekuwa akitembea kwenda kanisani ikiwa ni njia ya kufanya mazoezi anasema ana hofu ya kung’atwa na wanyama hao, ambao huambukiza ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, watu 900 hufariki dunia kila mwaka nchini kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa, huku takwimu zikionyesha mwaka 2024, takribani watu 35,000 waling’atwa na mnyama huyo.

Takwimu hizo zilitolewa Februari 6, 2025 na Mkurugenzi wa huduma za afya, ustawi wa jamii na lishe kutoka Tamisemi, Dk Rashid Mfaume wakati wa uzinduzi wa mpango wa pamoja kati ya Serikali na wadau kuangalia namna ya kudhibiti kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030.

Itaendelea kesho kwa kuangalia kuhusu huduma za chanjo kwa mbwa na binadamu waliong’atwa na mnyama huyo, pia mapendekezo ya wadau juu ya udhibiti wa mbwa wanaozurura mitaani.

Imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation