Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango wa elimu bila malipo ulivyoibua changamoto kwa jamii za wafugaji Arusha

Muktasari:

  • Wizara hiyo pia ina jukumu la kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu.

Dira ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, ustadi, umahiri, uwezo na mtazamo chanya ili kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Wizara hiyo pia ina jukumu la kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa letu.

Katika utekelezaji wa dira na dhima hii kumekuwepo sera, miongozo na jitihada za kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda. Pia, imejipanga kuhakikisha kuwa vikwazo vya wanafunzi kupata elimu vinaondolewa.

Hivyo, katika utekelezaji wa mikakati yake, Wizara hii mwaka 2016 ilitangaza mpango wa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

Mpango huu umekuwa na mafanikio katika shule za mijini, lakini katika shule za pembezoni za wanakoishi jamii ya Wamasai, Wahadzabe na Wabarbeig mpango huu umekabiliwa na dosari kadhaa ikiwamo kukosekana kwa chakula cha mchana shuleni.

Watoto wengi katika jamii hizi ambao chakula kwao ilikuwa ni motisha, sasa hawapati chakula na baadhi ya wanafunzi wameanza kurejea katika shughuli zao za asili kuchunga mifugo, kurina asali na kuokota matunda kwa ajili ya chakula chao.

Awali katika kuhamasisha watoto wa jamii hizi wapende elimu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP), lilianzisha mpango wa kutoa chakula cha mchana shuleni.

Mpango huu uligusa shule nyingi za pembezoni katika wilaya za Monduli na Karatu mkoani Arusha na hivyo kufanikiwa kuwavutia mamia ya wanafunzi, kuachana na utoro na kuboresha afya zao.

Hata hivyo, WFP walisitisha mpango wa kutoa chakula cha mchana shuleni kuanzia mwaka 2014 katika shule nyingi, lakini lilifanikisha kushirikisha jamii kuendelea na mpango huo.

Wakati mpango huo ukiendelea kwa wananchi kutoa michango, mwaka 2016 Serikali ilitangaza sera ya elimu bure ambayo ilifuta kero ya michango shuleni.

Katika utekelezaji wa mpango wa elimu bure, Serikali ilitangaza kutoa Sh18.77 bilioni kila mwezi ili kugharamia uendeshaji wa shule za Serikali za msingi na sekondari.

Kwa kiasi kikubwa katika shule hasa za mijini mpango wa elimu bure umekuwa na mafanikio kutokana na ongezeko la wanafunzi kwa zaidi ya asilimia 43 na sasa Serikali italazimika kujenga jumla ya madarasa 41,646 katika kipindi cha miaka mitano.

Hali hiyo inatokana na kuwepo kwa ongezeko la wastani wa watoto 333,169 kila mwaka kwa miaka mitano ijayo.

Changamoto za elimu bila malipo

Licha ya mpango huo kuongeza udahili wa wanafunzi maeneo ya mjini, umekuwa na kasoro kadhaa ikiwepo uhaba wa miundombinu, madarasa, walimu, vifaa vya kufundishia na ukosefu wa chakula shuleni hoja ambayo ndio inaathiri wanafunzi wa jamii za pembezoni.

Martin Kaaya, mwalimu wa Shule ya Msingi Kilimatinde, anasema shule hiyo tangu mwaka 2010 ilikuwa katika mpango wa WFP, lakini baadaye ulisitishwa.

“WFP walikuwa wanatoa chakula cha mchana, hadi mpango huo ulipositishwa mwaka 2014 na baada ya hapo wazazi na Serikali waliendeleza mradi huo kwa kuchanga,”anasema.

Anasema mwaka 2015 walikwenda vizuri kwa sababu wazazi walichangia chakula na pia walipata chakula cha msaada kwa ajili ya kupambana na njaa kilichotolewa na Serikali.

Mwalimu Zainabu Msangi wa Shule ya Msingi Losingiran anasema maisha duni ya jamii za wafugaji yamekuwa changamoto katika suala la elimu bure.

“Tunaishukuru Serikali kwa mpango huu wa elimu bure, tunapata fedha za kuendesha shughuli mbalimbali za shule, lakini kuhusu uchangiaji chakula imekuwa ni tatizo,”anasema.

Mwalimu Msangi anaomba serikali kuwa na mpango maalum wa kusaidia chakula hasa kwa shule ya pembezoni na bado mwamko wa elimu upo chini na pia kuna umaskini.

“Hata kama tukiwa na vifaa vingi vya kufundishia na walimu wazuri, lakini kama mtoto anayefundishwa afya yake sio nzuri sidhani kama tutafanikiwa,”anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yamaweega, iliyopo wilaya ya Karatu, Qyubati Chagula anasema wazazi kutothamini elimu ni moja ya matatizo makubwa ambayo yanawakabili.

“Sisi katika shule yetu tumepata mfadhili wa kutupa chakula, lakini shule za jirani wamekwama hivyo Serikali ikisaidia itaondoa tatizo hili,” anasema.

NGOs, Wabunge waisihi Serikali

Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti, Maendeleo na Huduma za Jamii za Pembezoni (CORDs), Lilian Lootoitai na ofisa wa masuala ya vijana na jinsia wa mtandao wa mashirika ya wafugaji nchini, PINGOS Forum, Nailejileji Tipap wanashauri Serikali kutazama upya mpango wa elimu bure.

Looloital anasema kimsingi kwa jamii za pembezoni mpango wa elimu bure umegeuka kuwa ni tatizo, kwani umeongeza utoro na kuathiri maendeleo ya wanafunzi.

“Lazima Serikali ipitie upya mpango huu, inawezekana maeneo ya mjini unafanya vizuri lakini vijijini imekuwa ni shida,”anasema.

Anasema shirika hilo tayari limekutana na walimu wakuu na wajumbe wa kamati za shule katika wilaya za Mkoa wa Arusha na kubaini changamoto za elimu bure ni nyingi.

Kwa upande wake Tipap anasema mpango wa elimu bure ulipaswa kufanyiwa utafiti maeneo mbalimbali nchini kabla ya kutangazwa.

“Mpango ulikuwa ni mzuri lakini, unapaswa kutazama maeneo yenye mahitaji maalumu na ndio sababu tunashauri Serikali kupitia upya mpango huu ili kusaidia shule za pembezoni,” anasema.

Utafiti juu ya changamoto za elimu bure ambao umefanywa na Shirika la Haki elimu, pia umebaini changamoto katika mpango huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, John Kalage licha ya kueleza utafiti wao, wamebaini kuwa sera ya elimu bila malipo imesababisha ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza hasa kwa shule za msingi lakini kuna changamoto.

Anazitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na shule kutopatiwa ruzuku kwa wakati, miundombinu duni, uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kufundishia.

Kalage anasema katika utafiti huo, wametoa mapendekezo kwa Serikali ifanye jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba wadau wote wanauelewa vizuri mpango wa elimu bila malipo ili kurahisisha utekelezaji wake.

Amesema kuwa wadau wote wanapaswa kuzielewa nyaraka zote na miongozo kuhusiana na sera ya elimu bila malipo ili kila mdau atambue wajibu wake na jinsi anavyopaswa kushiriki katika utekelezaji wa elimu bure.

Katika utafiti mwingie uliofanywa na Shirika la Twaweza Agosti 2016, uliojulikana kama ‘Hali Halisi: Maoni ya Wananchi juu ya elimu bila malipo ya ada’

Utafiti huu pia ulibaini, mafanikio pia changamoto ambazo ni upungufu wa vitabu, walimu na ukosefu wa chakula shuleni kuwa ni tatizo kwa shule za serikali.

Wabunge Monduli na Karatu

Wabunge katika majimbo ya Monduli na Karatu, Julius Kalanga (Monduli) na Cecilia Paresso( Viti Maalum- Karatu) wanashauri kufanyika tathimini wa mpango wa elimu bila malipo.

Kalanga anasema japo kuwa mpango huo ni mzuri lakini kwa maeneo ya vijijini, umekuwa na upungufu ambao sasa umegeuka kuwa janga.

“Serikali ilitoa kauli kuwa wazazi wasichangishwe michango lakini kimsingi Serikali imeshindwa kutimiza mahitaji yote ya shule ikiwepo kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana,” anasema.

Serikali kugharamia mahitaji muhimu katika shule sio hisani ni wajibu wake, kwani wananchi ndio wanalipa kodi za kuendesha Serikali.

Kwa upande wake, Paresso anasema Serikali itoke hadharani na kueleza imekwama kutekeleza mpango wa elimu bure.

“Ni bora wazazi na kamati za shule wangeruhusiwa kuendelea kuchanga kwa uwazi tu, ili kutatua kero lakini ambacho kipo sasa wanafunzi hasa wa vijijini ndio wanapata shida,” anasema.

“Hakuna chakula cha mchana shuleni, miundombinu bado ni duni, hakuna nyumba za walimu za kutosha,”anasema.

Msimamo wa Serikali

Hata hivyo, licha ya changamoto kadhaa katika mpango wa elimu bila malipo, Serikali inaeleza kujivunia mafanikio ambayo yamepatikana ikiwepo kuongeza udahili wa wanafunzi.

Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Gift Kyando pamoja na wakurugenzi halmashauri za Karatu na Monduli wanaeleza mpango wa elimu bila malipo umekufa na manufaa makubwa.

“Mpango wa elimu bila malipo umekuwa na manufaa na takwimu zipo wazi ingawa nipo nje ya ofisini, lakini mpango huu unakwenda vizuri,”anasema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Steven Ulaya anasema licha ya changamoto za chakula kwa baadhi ya shule, mpango wa elimu bila malipo katika halmashauri yake unakwenda vizuri.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Karatu, Papaking Kaai anasema mpango wa elimu bure kwa kiasi kikubwa umesaidia wilaya hiyo ikiwepo kuongeza udahili wa wanafunzi.

Kaai ambaye pia ni Ofisa Elimu wa Halmashuari ya Karatu anasema ingawa changamoto zipo, lakini zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Huu ndio mpango wa elimu bila malipo ambao unakabiliwa na changamoto kadhaa licha ya kuwa na mafanikio hatua ambayo imeibua hoja za kufanyika tathimini ya mpango huu, ili kuzipatia suluhu changamoto.