Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI ASKARI POLISI MTWARA: Mawakili wa utetezi waiwekea Serikali pingamizi lingine

Maofisa wa Jeshi la Polisi Mtwara wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, wakiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

Muktasari:

  • Ni mapingamizi juu ya mapingamizi, kesi ya mauaji inayowakabili askari Polisi mkoani Mtwara baada ya upande wa utetezi kuibua pingamizi lingine dhidi ya kielelezo cha upande wa mashtaka.

Mtwara. Baada ya Serikali kukubali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, mawakili wa utetezi wameibua pingamizi lingine dhidi ya kielelezo kingine.

Mawakili hao wameibua mapingamizi mawili dhidi ya upande wa mashtaka leo Jumatatu, Novemba 27, 2023 wakipinga Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara isipokee nyaraka mbili kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka umeomba Mahakama ipokea nyaraka zinazohusiana na uchunguzi wa picha za video alioufanya shahidi huyo wa nane, askari kutoka makao makuu ndogo ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, Nobert Leonard Massawe.

Kesi hiyo ya jinai namba 15/2023 inayosikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kassim Nassri, shahidi huyo wa nane ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha za mnato na picha za video kutoka kitengo cha uchunguzi wa kisayansi (Forensic Bureau) ameieleza mahakama kuwa Novemba 22, 2022 alipokea barua iliyomtaka kufanya uchunguzi wa picha za video.

Amedai barua hiyo ilitoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara ikiwa imeambatana na bahasha iliyokuwa na flash disk ikimtaka kuchunguza video hizo kubaini kama ni halisi na baada ya uchunguzi alibaini zilikuwa halisi.

Hivyo, aliandika ripoti ya matokeo ya uchunguzi na akajaza hati ya uthibitisho wa uchunguzi huo kuwa ni halisi akavifunga pamoja na flash disk hiyo akavirejesha ofisi ya RCO Mtwara.

Akiongozwa na Wakili wa Nassri, shahidi huyo ameomba Mahakama iipokee ripoti hiyo ya uchunguzi.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu ameweka pingamizi akidai upande wa mashtaka haukujenga msingi wa upokeaji wa ripoti hiyo kuwa kielelezo kwa kuwa hakumuongoza shahidi kueleza namna inavyohusiana na kesi hiyo.

Kutokana na pingamizi hilo, upande wa mashtaka uliomba ahirisho ili wapate muda kupitia ushahidi wao kuona namna ya kujibu, baada ya Mahakama kurejea dakika 40 ulikubaliana na pingamizi hilo.

Baada ya kukwaa kisiki katika kuwasilisha mahakamani nyaraka hiyo, wameiomba mahakama hiyo ipokee hati hiyo ya uthibitisho wa uchunguzi wa picha hizo.

Lakini nayo imewekewa pingamizi na upande wa utetezi.

Wakili Magafu amedai wanapinga nyaraka hiyo kupokewa kwa kuwa haina sifa kisheria za kuitwa hati ya uthibitisho na kwamba ni sawa na barua ya kawaida.

Amedai nyaraka hiyo kwa mujibu wa sheria  inapaswa kuwa na tamko akidai kuwa kama kiapo,  ili kuonyesha kile kitu alichokitoa kwenye kompyuta ni halisi hakikubadilishwa, kuchezewa au kuhaririwa.

Amedai matakwa hayo yanaendana na sheria ya viapo sura ya 34 kama ilivyorejewa mwaka 2019 kifungu cha 10.

"Mheshimiwa hiki kinachoitwa hati ya uthibitisho haina tamko, hivyo kwa kutokuwa na tamko hii ni sawa na barua, hivyo haistahili kuitwa hati kwa sababu hiyo tunaomba isipokewe," amesema Wakili Magafu.

Wakili Magafu amedai kuwa sababu ya pili kupinga hati hiyo kuwa haijakamilika kwa kuwa inaonyesha imeambatanishwa na ripoti ya uchunguzi ambayo tayari imeshakataliwa na kwamba kukubali kuipokea hati hiyo,  upande wa mashtaka wanataka wairejesha ripoti ile kwa mlango wa nyuma.

Amedai ingawa hati hiyo inajieleza kuwa imeambatanishwa na nyaraka nyingine, hata nyaraka hizo hazijaambatanishwa na kusisitiza hilo linaifanya isiwe kamili.

"Kwa hayo machache, tunaomba hii ambayo wao wanaiita hati isipokewe, maana si  ni sawa na barua tu," amesisitiza Wakili Magafu.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Ignas Mwinuka amedai shahidi wao aliyeiandaa ambaye ni mtaalamu amesema ni cheti na iko kwa mujibu wa sheria na shahidi amefuata matakwa ya sheria.

"Hii fomu imetolewa chini ya kifungu cha 202(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA). Huyu shahidi wetu hakujitungia hii fomu bali ameifuata hiki kifungu," amedai Wakili Mwinuka.

Kuhusu kutokuwa na  viambatanisho, vilivyotajwa ndani ya hati hiyo, amedai Wakili Magafu amekwenda kinyume na misingi ya kisheria kuhusiana na upokeaji vielelezo kwa kwenda kusoma maudhui wakati ikiwa bado haijapokewa, akidai kielelezo mpaka kipokewe ndipo kisomwe yaliyomo.

"Shahidi wetu bado yuko kizimbani na kila kielelezo kina namna yake ya kupokewa. Kutokuwa na viambatanisho ni hoja ambayo haiko katika suala la upokewaji vilelelezo," amesema Wakili Mwinuka na kusisitiza:

"Kwa hiyo wakili (Magafu) hakuwa sahihi kusema hii ni sawa na barua tu kwenye fomu ambayo inatawaliwa na sheria. Kwa misingi hiyo tunaomba hoja yao ikataliwe," amesema.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu Pascal Marungu amedai walivyosema fomu hiyo inatokana na kifungu cha 202 cha CPA hakina hitaji la tamko.

Pia amedai kuwa fomu hiyo haitakiwi kusomeka pamoja na sheria ya viapo na kwamba kwenye viapo ndiko  kunatakiwa tamko.

"Kwa sababu kilichoko mbele yetu kinachotakiwa kutolewa si kiapo, hakuna haja ya tamko wala haihusiani. Nyaraka yetu inayotakiwa kutolewa hapa imekidhi matakwa ya sheria kifungu cha 202 CPA,"amesisitiza Wakili Marungu.

Hata hivyo, Wakili Magafu amepinga kifungu cha 202 CPA hakitumiki, kwani kifungu cha kwanza kinazungumzia ukuzaji wa picha au maandishi na hakihusiani na uhalisia wa vifaa vya kielektroniki.

Wakili Magafu amesisitiza masharti ya kifungu cha 202 CPA hutumiwa na wataalamu wa maandishi, ili kulinganisha maandishi yaani hutumika katika kutambua mwandiko wa mkono.

Huku akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi mojawapo amesisitiza hati kama hiyo lazima iwe na tamko.

"Kwa hiyo hii hati ilitakiwa iwe chini ya kifungu cha 18 sheria ya miamala ya kielektroniki na si chini ya kifungu cha 202 maana hicho kinauhusiana na kitu kingine," amesisitiza Wakili Magafu na kuongeza:

"Pia nimesema hii nyaraka haikukamilika maana viambatanisho vilivyotajwa havikuambatanishwa. Kielelezo hakitokewi nusunusu, mfano kama ni kitabu huwezi kuondoa ukurasa mwingine halafu uzitafutie siku ya kuzileta.

Amehitimisha kuwa kwa ujumla hoja za upande wa mashtaka hazina mashiko na hazipaswi kukubaliwa.

Jaji Kakolaki baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo kwa muda kwa ajili ya kuandika uamuzi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara, ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi  (Insp.) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara;  A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Wanakabiliwa na shtaka la mauaji wakidaiwa kumuua Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.