Prime
KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI ASKARI POLISI MTWARA: Serikali yakubali pingamizi la mawakili wa utetezi

Maofisa wa Jeshi la Polisi Mtwara wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, wakiwa katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.
Mtwara. Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, umekubaliana na pingamizi la mawakili wa utetezi na kuondoa maombi yake ya upokewaji wa kielelezo.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo, upande wa mashtaka umemuita shahidi wake wa nane, Nobert Leonard Massawe, ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha za mnato na picha jongefu (video) kutoka makao makuu ndogo ya Jeshi la Polis Dar es Salaam.
Wakati akitoa ushahidi wake akiongozwa na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kassim Nassri, shahidi huyo ameiomba Mahakama ipokee taarifa ya uchunguzi wa picha za video alizofanyia uchunguzi ziwe kielelezo cha upande wa mashtaka.
Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu aliibua pingamizi aliiomba mahakama hiyo isiipokee ripoti hiyo, akidai upande wa mashtaka haujaweka msingi unaoiwezesha Mahakama kupokea kielelezo hicho.
"Shahidi amesema alipokea flash disk kutoka Mtwara, hajaieleza Mahakama ilikuwa inahusianaje na tukio husika. Shahidi hajaieleza Mahakama picha zilichukuliwa wapi ili kuona kama inahusiana na kesi hii," amesema Wakili Magafu.
Baada ya hoja hizo za pingamizi, upande wa mashtaka uliomba wapewe muda wa dakika 30 ili watafakari kupitia ushahidi wa mashahidi wake waliotangulia, ili kuona namna gani kielelezo hicho kinauhusiana na kesi hiyo.
Baada ya Mahakama kurejea, upande wa mashtaka umeeleza wamekubaliana na pingamizi hilo, hivyo kuondoa ombi lao la Mahakama kupokea ripoti hiyo kuwa kielelezo.
"Jaji baada ya kupitia kumbukumbu za Mahakama, tunakubaliana na pingamizi hivyo tunaomba kuondoa ombi letu ili kuendelea na examination in chief (mahojiano ya msingi kati ya mwendesha mashtaka na shahidi) ambapo humuuliza shahidi maswali ya kumuongoza kutoa ushahidi wake.
Jaji Kakolaki amekubaliana na hoja ya upande wa mashtaka.
"Kwa sababu upande wa mashtaka umekubaliana na hoja la pingamizi, Mahakama hii inalikubali pingamizi na ombi la kuondoa mahakamani kielelezo chao linakubaliwa," amesema Jaji Kakolaki.
Baada ya uamuzi huo, Wakili Nassri ameendelea kumuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake kuhusiana na uchunguzi wa video hizo.
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp.) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.
Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai fedha na mali zake walizozichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwao wakimtuhumu kwa wizi wa fedha na pikipiki.