Prime
KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI POLISI: Kesi yasimama kwa muda baada ya utetezi kupinga kielelezo

Mshtakiwa wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara ya madini, Mussa Hamis inayowakabili maafisa saba wa Polisi mkoani Mtwara, ASP Nicholas Kisinza akiwasikiliza mawakili wao, Majura Magafu (kushoto) na Emmanuel Msengezi, ndani ya ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.
Muktasari:
- Mahakama imeahirishwa kwa muda kesi ya askari Polisi Mtwara wanaokabiliwa na shtaka la mauaji ya mfanyabiashara wa madini, baada ya mawakili wa utetezi kuibua pingamizi dhidi ya kielelezo cha upande wa mashtaka.
Mtwara. Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara imesimama kwa muda, ili kutoa fursa kwa upande wa mashtaka kutafakari hoja za pingamizi la upande wa utetezi dhidi ya kielelezo wanachotaka kuwasilisha.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo na upande wa utetezi umemuita shahidi wake wa nane, Nobert Leonard Massawe ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha za mnato na picha jongefu (video) kutoka makao makuu ndogo ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Wakati akitoa ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kassim Nassri, shahidi huyo ameiomba mahakama ipokee taarifa ya uchunguzi wa picha za video alizofanyia uchunguzi ziwe kielelezo cha upande wa mashtaka.
Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu ameibua pingamizi aliiomba mahakama hiyo isiipokee ripoti hiyo, akidai kuwa upande wa mashtaka haujaweka msingi unaoiwezesha Mahakama kupokea kielelezo hicho.
Wakili Magafu kwa niaba ya mawakili wa utetezi, ameieleza Mahakama kuwa moja ya vigezo vya kielelezo kupokewa na Mahakama ni uhusiano wa kielelezo hicho na kesi husika.
"Shahidi amesema alipokea flash disk kutoka Mtwara, hajaieleza Mahakama ilikuwa inahusianaje na tukio husika. Shahidi hajaieleza Mahakama picha zilichukuliwa wapi, ili kuona kama inahusiana na kesi hii," amesema Wakili Magafu na kuongeza:
"Kwa hiyo kwa kuwa wameshindwa kujenga msingi na kuonyesha kuwa ina uhusiano gani wana namna mbili ama kuiondoa au kujibu hoja, lakini sisi tunasema haina uhusiano wowote na kesi hii."
Baada ya hizo za pingamizi, upande wa mashtaka umeomba wapewe muda wa dakika 20 ili watafakari kwa kupitia ushahidi wa mashahidi wake waliotangulia, ili kuona namna gani kielelezo hicho kinahusiana na kesi hiyo.
Mheshimiwa Jaji tunaomba ahirisho la dakika 20 ili tupitie ushahidi wa mashahidi wetu ili tuona uhusiano ili kama tunajibu tujibu kwa ukamilifu au kama tunakubali pingamizi," amesema Wakili Nassri.
Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka, baada ya ya upande wa utetezi kueleza kuwa hawana pingamizi kuhusu upande wa mashtaka kupewa muda.
Hivyo, Jaji Kakolaki ameahirisha kesi hiyo kwa dakika 30 kabla ya kuendelea ambapo upande wa mashtaka ama watajibu hoja za pingamizi hilo au watakubaliana nalo na kuondoa nia yao ya kuwasilisha ripoti hiyo ipokewe kama kielelezo.
Kesi hiyo ya jinai namba 15/2023 inayosikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza; Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi; Mkaguzi (Insp.) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; A/Insp. Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.
Endelea kufuatilia.