Kesi ya polisi wanaodaiwa kumuua muuza madini: Wakili afiwa na baba mzazi, Jaji atoa maagizo kwa msajili

Muktasari:
- Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya mauaji inayowakabili askari polisi saba mjini Mtwara, baada ya Wakili Fredrick Ododa anayemwakilisha mshtakiwa wa pili, kufiwa na baba yake mzazi huku Jaji anayesikiliza kesi hiyo akimweleza msajili amtafutie mshtakiwa huyo wakili mwingine Ili kesi iendelee kusikilizwa Jumatatu.
Mtwara. Wakili Fredrick Ododa anayemwakilisha mshtakiwa wa pili katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, amefiwa na baba yake na kusababisha kesi kutokuendelea kusikilizwa leo Alhamisi, Novemba 23,2023.
Kutokana na sababu hiyo, Jaji Edwin Kakolaki amelazimika kuahirisha kesi mpaka Jumatatu, Novemba 27, 2023 huku akimuelekeza msajili wa mahakama hiyo kumtafutia wakili mwingine mshtakiwa ambaye wakili wake amefiwa na baba yake.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi (A/Insp) Marco Mbuta Chigingozi, Mkaguzi (Insp.) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, A/Insp Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.
Wanadaiwa kumuua kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi, ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizozichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwao wakimtuhumu kwa wizi wa fedha na pikipiki.
Kutokana tatizo la wakili huyo, Ododa anayemwakilisha mshtakiwa wa pili, ASP Onyango, Mahakama imeshindwa kuendelea na usikilizwaji, hivyo kuiahirisha mpaka Jumatatu, Novemba 27, mwaka huu.
Awali, mawakili wa pande zote walikuwa katika majadiliano na Jaji Kakolaki yaliyochukua saa kadhaa, mpaka mchana ilipoitwa na kisha kuahirishwa baada upande wa utetezi kuwasilisha taarifa hiyo ya wakili mwenzao kufikiwa na kuomba ahirisho.
Baada ya mawakili wa pande zote kuingia ndani na kisha Jaji Kakolaki, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Maternus Marandu akaieleza mahakama kuwa mwakilishi wa kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Robert Dadaya ana ombi ambalo anataka kuliwasilisha.
"Mheshimiwa Jaji shauri lilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa, lakini kabla ya kuingia hapa mahakamani asubuhi nimeongea na Wakili Dadaya akasema kuna maombi atayaleta hapa, mahakama hii ikipendezwa imruhusu awasilishe maombi hayo," ameeleza.
Jaji Kakolaki alikubaliana na hoja hiyo, ndipo Wakili Dadaya aliyemwakilisha kiongozi wa jopo lao, Wakili Majura Magafu alieleza kuwa wakili mwenzao Ododa amefiwa na baba yake mzazi.
“Mheshimiwa jaji kwa mazingira hayo tunaomba mahakama yako ikipendezwa iahirishe shauri hili mpaka siku nyingine ili mshtakiwa wa pili apate uwakilishi kwa maana ya wakili mwingine," ameelza wakili Dadaya.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Marandu amesema hawana pingamizi na ndipo Jaji Kakolaki aliahirisha kesi hiyo huku akitoa maelekezo hayo kwa msajili.
"Kutokana na ukweli kwamba mshtakiwa wa pili anapaswa kuwa na uwakilishi wakati shauri linaendelea, kwa misingi ya haki tunapaswa kuahirisha shauri hili ili apate wakili atakayemwakilisha mpaka wakili wake atakapoungana naye baadaye.
"Kwa kipindi hiki msajili anaelekezwa kumtafutia wakili mwingine mshtakiwa, hivyo shauri hili linaahirishwa mpaka Novemba 27, 2023 na washtakiwa mtaendelea kuwa mahabusu," amema jaji huyo.
Leo ni mara ya pili kesi hivyo kukwama kuendelea kusikilizwa, baada ya jana Jumatano kuahirishwa kutokana na mashahidi wote wawili wa upande wa mashtaka kushindwa kufika mahakamani kutokana na kuugua.
Jana asubuhi, baada ya kesi kuitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, Wakili Marandu aliieleza mahakama kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji upande wa mashtaka lakini mashahidi wao waliokuwa wamewaandaa wamepata matatizo ya kiafya.
"Tulikuwa na mashahidi wawili, wa kwanza amepata changamoto ya afya tangu jana na wa pili vilevile amepata changamoto ya kiafya usiku wa kuamkia leo (jana)," alisema Wakili Marandu.