Prime
Mashahidi wa Serikali waugua, kesi mauaji ya muuza madini yaahirishwa

Mshtakiwa wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara ya madini, Mussa Hamis inayowakabili maafisa saba wa Polisi mkoani Mtwara, ASP Nicholas Kisinza akiwasikiliza mawakili wao, Majura Magafu (kushoto) na Emmanuel Msengezi, ndani ya ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.
Muktasari:
- Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imeshindwa kuendelea na usikilizaji wa kesi ya mauaji ya muuza madini wa Nachingwea Lindi, anayedaiwa kuuawa na maofisa wa Polisi mkoani Mtwara baada ya mashahidi wa Jamhuri kuugua na kushindwa kufika mahakamani. Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Alhamisi.
Mtwara. Mashahidi wawili wa Serikali waliokuwa wameandaliwa kutoa ushahidi wao katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, wameugua wote hivyo kukwamisha mwendelezo wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 inayosikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa leo Jumatano Novemba 22, 2023 ambapo a upande wa mashtaka ulikuwa uwasilishe ushahidi.
Hata hivyo, baada ya kuitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu ameieleza Mahakama mashahidi wao waliokuwa wamewaandaa wamepata matatizo ya kiafya, akaomba iahirishwe hadi tarehe nyingine.
"Mheshimiwa shauri hili linakuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka," amesema Marandu na kuendelea:
"Ilikuwa mashahidi wawili watoe ushahidi kwa leo, wa kwanza amepata changamoto ya afya tangu jana na wa pili vilevile amepata changamoto ya kiafya usiku wa kuamkia leo,”amesema.
Wakili Marandu amehitimisha kwa kwa kusema “Kwa muktadha huo mheshimiwa Jaji tunaomba Mahakama yako tukufu, kama itapendezwa ipokee ombi letu la kuomba ahirisho kwa leo na itupangie siku nyingine.
Akijibu hoja hiyo ya upande wa mashtaka ya ahirisho, Wakili Robert Dadaya, kwa niaba ya kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu, amesema kwa umoja wao hawana pingamizi kwa maombi ya upande wa Jamhuri.
"Kutokana na sababu zilizotolewa, tunalazimika kuahirisha shauri hili hadi kesho saa 3:00 asubuhi. Upande wa mashtaka mhakikishe mnaleta mashahidi wenu ili tuweze kuendelea. Washtakiwa mtaendelea kuwa chini ya uangalizi wa mahabusu," amesema Jaji Kakolaki.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, aliyekuwa Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.
Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Wilaya (DCIO) Mtwara ASP Nicholaus Stanslaus Kisinza, Mkaguzi Msaidizi, Marco Mbuta Chigingozi, Mkaguzi John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara; Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.
Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa Hamis katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Mussa kwa kumziba mdomo na pua kwa kutumia tambala, baada ya kumchoma sindano ya dawa ya usingizi.
Kulingana na ushahidi huo, walifikia uamuzi huo ili asiendelee kuwadai pesa na mali zake walizokuwa wamezichukua walipokwenda kumfanyia upekuzi nyumbani kwake wakimtuhumu kuiba pikipiki na mali hizo. Upande wa mashtaka unatarajia kuwaita mashahidi 72 (idadi iliyotajwa, ingawa wanaweza kupunguza wengine kadri itakavyoonekana inafaa), lakini mpaka sasa waliokwishatoa ushahidi ni saba.