Prime
KESI YA MAUAJI INAYOWAKABILI ASKARI POLISI MTWARA: Mahakama yakataa hati ya uthibitisho uchunguzi wa video

Washitakiwa wa mauaji ya Mfanyabiashara wa madini ambao ni Maofisa wa Polisi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara. Picha na Maktaba.
Mtwara. Mahakama imekataa kupokea hati ya uthibitisho wa uhalisia wa picha za video kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa hati hiyo imeandaliwa chini ya kifungu cha Sheria kisichohusika.
Jaji Edwin Kakolaki anayesikiliza kesi hiyo, amesema Kifungu Cha 202 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Ushahidi kilichotumika kuandaa hati hiyo inalenga kuthibitisha uhalisia wa picha za video hizo hakihusiki kwa kuwa kifungu hicho hakishughuliki na picha za video.
Hivyo, amesema kwa sababu hiyo hati hiyo haiwezi kuthibitisha video hizo na ameutupilia mbali.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilikataa hoja nyingine za pingamizi la kupokea hati hiyo zilizoibuliwa na upande wa utetezi kupitia kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu.
Upande wa mashtaka uliiomba mahakama ipokea hati ya uthibitisho wa picha za video alizozifanyia uchunguzi wa uhalisia wake, shahidi wake wa nane, askari kutoka makao makuu ndogo ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, Nobert Leonard Massawe.
Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga pamoja na mambo mengine ukidai haijakidhi matakwa ya kisheria kwa kutokuwa na tamko na kwamba haikuwa kamilifi kwa kutokuambatanishwa na nyaraka nyingine zilizotajwa kuwa zimeambatanishwa nayo.
Mawakili wa Serikali wakipinga hoja hizo, wakidai hati hiyo iko kwa mujibu wa sheria, kwani imetokana na matakwa ya kifungu cha 202 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kwamba hahitaji kuwa na tamko.
Katika ushahidi wake, shahidi huyo wa nane ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha za mnato na picha za video, kutoka kitengo cha uchunguzi wa kisayansi (Forensic Bureau) ameieleza mahakama kuwa Novemba 22, 2022 alipokea barua iliyomtaka kufanya uchunguzi wa picha za video.
Ameeleza barua hiyo ilitoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Mtwara ikiwa imeambatana na bahasha iliyokuwa na flash disk ikimtaka kuchunguza video hizo kubaini kama ni halisi na kwamba baada ya uchunguzi wake alibaini kuwa zilikuwa ni halisi.
Hivyo baada ya uchunguzi huo liandika ripoti ya matokeo ya uchunguzi, na akajaza hati ya uthibitisho wa uchunguzi huo kuwa ni picha halisi akavifunga pamoja na flash disk hiyo akavirejesha ofisi ya RCO Mtwara.
Akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kassim Nassri, shahidi huyo ameiomba mahakama hiyo ipokee hati hiyo ya uthibitisho wa uchunguzi wa picha hizo ndipo upande wa utetezi ukaibua pingamizi hilo.
Wakili Magafu alipinga akidai nyaraka hiyo haina sifa kisheria za kuitwa hati ya uthibitisho na kwamba ni sawa na barua ya kawaida.
Akidai kuwa nyaraka hiyo kwa mujibu wa sheria ya inapaswa kuwa na tamko, ili kuonesha kuwa kile kitu shahidi huyo alichokitoa kwenye kompyuta ni halisi hakikubadilishwa, kuchezewa au kuhaririwa.
Amedai matakwa hayo yanaendana na Sheria ya Viapo Sura ya 34 kama ilivyorejewa mwaka 2019 kifungu cha 10.
"Mheshimiwa hiki kinachoitwa hati ya uthibitisho haina tamko hivyo kwa kutokuwa na tamko. Hii ni sawa tu na barua, hivyo haistahili kuitwa hati kwa sababu hiyo tunaomba isipokewe," alisema wakili Magafu.
Wakili Magafu amedai kuwa sababu ya pili kupinga hati hiyo ni kwamba haijakamilika.
Amedai hati hiyo inaonyesha imeambatanishwa na ripoti ya uchunguzi ambayo tayari imeshakataliwa na kwamba kukubali kuipokea, upande wa mashtaka wanataka wairejesha ile ripoti kwa mlango wa nyuma.
Wakili Magafu amedai ingawa hati hiyo inajieleza imeambatanishwa na nyaraka nyingine mbali na hiyo ripoti ya uchunguzi, hata hizo nyaraka hazijaambatanishwa na kusisitiza hilo linaifanya isiwe kamili
Akijibu hoja hizo Wakili wa Serikali Mwandamizi Ignas Mwinuka amedai shahidi wao aliyeiandaa ambaye ni mtaalamu amesema kuwa hiyo ni hati na kwamba iko kwa mujibu wa sheria na shahidi amefuata matakwa ya sheria.
"Hii fomu imetolewa chini ya kifungu cha 202(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA(. Huyu shahidi wetu hakujitungia hii fomu balia ameifuata hiki kifungu", amedai Wakili Mwinuka.
Kuhusu kutokuwa na viambatanisho, vilivyotajwa ndani ya hati hiyo, amedai Wakili Magafu amekwenda kinyume na misingi ya kisheria kuhusiana na upokeaji vielelezo kwa kusoma maudhui yaliyomo wakati ikiwa bado haijapokewa akidai kuwa kielelezo mpaka kipokewe ndipo kisomwe yaliyomo.
"Shahidi wetu bado yuko kizimbani na kila kielelezo kina namna yake ya kupokewa. Kutokuwa na viambatanisho ni hoja ambayo haiko katika suala la upokewaji vilelelezo", amesema Wakili Mwinuka na kusisitiza:
"Kwa hiyo Wakili (Magafu) hakuwa sahihi kusema kuwa hii ni sawa na barua tu kwenye fomu ambayo inatawaliwa na sheria. Kwa misingi hiyo tunaomba hoja yao ikataliwe"
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu Pascal Marungu amedai kama walivyoeleza (akirejea alichoeleza Wakili Mwinuka) hiyo fomu inatokana na kifungu cha 202 cha CPA na kifungu hicho hakina hitaji la tamko.
Pia amedai fomu hiyo haitakiwi kusomeka pamoja na sheria ya viapo na kwamba kwenye viapo ndiko kunatakiwa tamko.
"Kwa sababu kilichoko mbele yetu kinachotakiwa kutolewa si kiapo hakuna haja ya tamko wala haihusiani.Nyaraka yetu inayotakiwa kutolewa hapa imekidhi matakwa ya sheria kifungu cha 202 CPA.", amesisitiza Wakili Marungu.
Hata hivyo, Wakili Magafu amepinga akidai kifungu cha 202 CPA hakitumiki, kwani kifungu cha kwanza kinazungumzia ukuzaji wa picha au maandishi na hakihusiani na uhalisia wa vifaa vya kielektroniki.
Amesisitiza kuwa masharti ya kifungu cha 202 CPA hutumiwa na wataalamu wa maandishi, ili kulinganisha maandishi yaani hutumika katika kutambua mwandiko wa mkono.
Huku akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi mojawapo amesisitiza hati kama hiyo lazima iwe na tamko.
"Kwa hiyo hii hati ilitakiwa iwe chini ya kifungu cha 18 Sheria ya Miamala ya Kielektroniki na si chini ya kifungu cha 202 maana hicho kinauhusiana na kitu kingine", amesisitiza Wakili Magafu na kuongeza:
"Pia nimesema hii nyaraka haikukamilika maana viambatanisho vilivyotajwa havikuambatanishwa. Kielelezo hakitokewi nusunusu mfano kama ni kitabu huwezi kuondoa page nyingine halafu uzitafutie siku ya kuzileta."
Alihitimisha kuwa kwa ujumla hoja za upande wa mashtaka hazina mashiko na hazipaswi kukubaliwa.
Awali, upande wa mashtaka ulikwama kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wa video hizo baada ya kuwekewa pingamizi na upande wa utetezi.
Wakili Magafu alipinga kupokewa kwa ripoti hiyo pamoja na mambo mengine akidai upande wa mashtaka haukujenga msingi wa upokeaji ripoti hiyo kuwa kielelezo kwa kuwa hakumuongoza shahidi kueleza namna inavyohusiana na kesi hiyo.
Baada ya Mahakama kurejea upande wa mashtaka ulikubaliana na pingamizi hilo.
Mheshimiwa Jaji baada ya kupitia kumbukumbu za Mahakama tunakubaliana na pingamizi", amesema wakili Nassri na kuongeza:
"Hivyo tunaomba kuondoa ombi letu ili tuendelee na examination in chief (mahojiano ya msingi kati ya mwendesha mashtaka na shahidi ambapo humuuliza shahidi maswali ya kumuongoza kutoa ushahidi wake)
Kesi hiyo itaendelea kesho kwa ushahidi wa shahidi huyo wa nane kumalizia sehemu ya ushahidi wake uliobakia.