Dk Rioba: Nafasi ya Tehama kukuza uchumi kidijitali kujadiliwa Zanzibar

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Tanzania (TBC), Ayub Rioba (kulia) alipotembele katika ofisi za Mwananchi Communication (MCL) Tabata leo Ijumaa Oktoba 6, 2023.
Muktasari:
- Mkutano mkuu wa mwaka wa 30 wa Umoja wa Mashirika ya Utangazaji ya Umma Kusini mwa Afrika (Saba), utafanyika kwa siku mbili Zanzibar, na kujadili kwa kina pia nafasi ya Tehama na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali Afrika ili kuleta maendeleo endelevu.
Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Mashirika ya Utangazaji ya Umma Kusini mwa Afrika (Saba), utakaoangazia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) katika kukuza uchumi wa kidigitali barani Afrika.
Mkutano huo ambao ni 30, hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi wanachama, na kwa mwaka huu utafanyika Mjini Unguja kuanzia Oktoba 10 hadi 12, ambapo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wake, ukihusisha wadau wa habari zaidi ya 200 kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 6, 2023 alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Ltd (MCL) zilizopo Tabata Relini, ambapo alipokelewa na mwenyeji wake, Bakari Machumu, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL.
Dk Rioba amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo utajadili kwa kina nafasi ya Tehama na mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali Afrika ili kuleta maendeleo endelevu kwa kuonyesha maboresho makubwa yaliyofanyika hivi karibuni katika teknolojia ya habari.
“Lengo jingine ni kubadilisha habari, kuongeza wigo wa uelewa katika masuala ya Tehama ili kupeana mbinu za kuboresha teknolojia ya habari na utangazaji yatakayoendana na mabadiliko ya kiteknolojia ya sasa,” amesema Dk Rioba.
Dk Rioba aliyewahi kuwa mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), amesema katika kipindi cha miaka saba iliyopita taasisi hiyo ya Saba imekuwa na dhima ya kuzungumzia Tehama kwa upande matokeo hasi na chanya katika uendeshaji wa vyombo vya habari vya utangazaji.
Amesema katika mkutano huo wataangalia namna ambavyo vyombo vya habari vya zamani, vitaweza kujiendesha kiuchumi katika muktadha ambao hivi sasa vyombo vya habari vya mtandaoni vimeshika kasi.
“Miaka michache iliyopita nikiwa SMJC nilifanya utafiti uliobaini kuwa asilimia 27 ya Watanzania wana uwezo wa kuifikia intarneti, lakini takwimu za sasa hivi ni zaidi ya nusu wanaifikia.
“Kwa hiyo hakuna namna tutakayokwepa kuangalia jinsi ya kuwa imara zaidi, lazima vyombo vyetu vya habari vitafakari namna ya kujiimarisha kiuchumi kuliko kutegemea vyanzo vya asili vya mapato vya matangazo ya biashara.
Dk Rioba amesema pia wameualika Umoja wa Vyombo vya Utangazaji vya Umma Afrika (AUB), akisema vyombo vya habari vya magazeti vimealikwa ili kujengeana uwezo na uzoefu katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Dk Rioba, pamoja na mambo mengine mkutano huo utachangia ongezeko la pato la Taifa linalotokana na utalii, akisema wameichagua Zanzibar kuwa mojawapo ya maeneo muhimu ya utalii hapa nchini.
“Wageni hawa watakaokuja watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Zanzibar na kujionea uzuri na upekee wa eneo sehemu hii ya nchi yetu. Hadi sasa watu 100 wamethibitisha kushiriki, baadhi yao wameshawasili,” amesema Dk Rioba.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu ameipongeza TBC kwa kuhakikisha mkutano wa Saba unafanyika Tanzania kwa mara nyingine, akisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia yaliyosababisha mtindo wa wananchi kupata taarifa kubadilika.
“Napongeza mkutano huu unachukua dhima ya kidijitali, kama MCL tunashukuru kwa kututembelea, tunaahidi kushikiri katika kuelezea kwa kuangalia mjadala na kuupeleka kwa wananchi.
“Lakini tutoe mchango wa uzoefu kwamba tunakokwenda tunabadilika kwenye kumtambua vizuri mteja na kumhudumia kwa kutumia njia tofauti kama ni redio, magazeti au televisheni, lakini wa kidijitali pia wanataka maudhui yale yale,” amesema Machumu.