Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nape aeleza uwezekano Watanzania kupiga kura kwa intaneti

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kwa sasa nchini kuna watumiaji milioni 34 wa intaneti na kuna miundombinu mingi inawekezwa hivyo inawezekana kupanua demokrasia kwa kutumia teknolojia hiyo.

Dar es Salaam. Serikali imeeleza uwezekano wa Watanzania kupiga kura katika chaguzi zijazo kwa kutumia intaneti kutokana na ongezeko la watumiaji wa mtandao wa intaneti pamoja na kasi ya ukuaji wa huduma hiyo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 28 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika kongamano la Jukwaa la Uhuru wa Mitandao barani Afrika, (FIFAfrica23), lililoandaliwa na Taasisi ya Ushirikiano wa Sera ya Kimataifa ya Tehama Afrika Mashariki na Kusini (CIPESA) na kufanyika jijini Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo lililoshirikisha wadau kutoka nchi 40 zikiwemo Ufaransa, Marekani na Uingereza, Nape amesema kwa sasa kuna watumiaji milioni 34 wa intaneti na kuna miundombinu mingi inawekezwa hivyo inawezekana kupanua demokrasia kwa njia hiyo.

"Ikiwezekana chaguzi zijazo ziwe chaguzi zinazotumia teknolojia. Kwa nini isifike mahali kuwe na uwezo wa mtu kupiga kura mtandaoni popote alipo badala ya kwenda kupanga foleni," amesema Nape.

Amesema uamuzi ukifikiwa kujipanga sio shida ukilinganisha na matumizi na miundombinu ya huduma hiyo.

"Kila kitu kinawezekana kufanyika mtandaoni kama mtu unaweza kununua vitu, kuomba kazi kupitia mtandao kwanini ushindwe kufanya maamuzi ya kupiga kura. Hii inawezekana pia kupanua demokrasia yetu ili ushiriki wa watu ukawa mwingi kwa kuwaruhusu watu, na zipo nchi zimefanya hivyo zikafanikiwa," amesema Nape.

Hata hivyo, ameonya teknolojia hiyo ya intaneti pamoja na uhuru wa mtandao uliopo kusifanye maadili ya Kitanzania yakasahaulika.

"Sisi kama nchi ni waumini wa uhuru wa mtandao na ni haki ya kikatiba, hivyo ni muhimu sana kuendelea kulinda maadili, tamaduni na watoto wetu wa kiafrika. Tumeona madhara yaliyotokea kwenye nchi za wenzetu," amesema.

Amesema ni vyema kuulinda utamaduni wa Kitanzania na kiafrika kwa ujumla ili jamii iendelee kubake salama.

Kwa upande wake Neema Lugangila Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) amesema, kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa 2025, intaneti inapaswa kuimarishwa Watanzania waone yanayoendelea.