Prime
Makalla alivyojitenga na uvumi wa ubunge Morogoro

Muktasari:
- Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amefanya ziara ya siku tano mkoani Morogoro ambapo alitumia ziara hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo la kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2025.
Morogoro. Ziara ya siku tano ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, mkoani Morogoro, imemtosha kujitenga na uvumi kuwa atagombea ubunge katika Jimbo la Mvomero.
Hii ni kutokana na kile alichoeleza hana nia ya kugombea ubunge, badala yake mawazo yake yamejikita katika kumsaidia mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi ya uenezi wa CCM.
Makalla aliyewahi kuwa Mbunge wa Mvomero 2010/15 alikata mzizi wa fitina huo baada ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Jonas Van Zeeland kuweka bayana kwamba hatachukua fomu ya kutetea nafasi hiyo endapo mwenezi huyo atajitosa kwenye kinyang'iro hicho.
Zeeland alieleza hayo katika mkutano wa hadhara wa Makalla uliofanyika Mei 7 wilayani Mvomero, akibainisha kuwa amefikia uamuzi huo, kutokana na ukarimu na roho ya upendo aliyonayo Makalla, kwa kuwa alimuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka 2020, licha ya Kamati Kuu ya CCM kukata jina lake.
Katika mchakato wa kura za maoni za CCM mwaka 2020, Makalla aliongoza kwa kura 321, Sadiq Murad 231 na Zeeland 112, hata hivyo kamati kuu haikurejesha jina la Makalla badala yake ilimteua Zeeland kupeperusha bendera ya chama hicho kwa nafasi ya ubunge.
Katika maelezo yake, Zeeland amesema: "Katika kura za maoni za CCM Makalla alikuwa mtu wa kwanza, Sadiq Murad wa pili, kisha mimi wa tatu, baada ya matokeo yao nilimpigia simu Makalla na kumweleza nia yangu ya kumuunga mkono kwenye kampeni, sikujua kama nitateuliwa na kamati kuu."
"Nataka niwaambie wananchi wa Mvomero kama kuna mtu amenifundisha siasa uvumilivu, hakuna mwingine ni Makalla, hakuwa na kinyongo. Wakati wa kampeni za kusaka kura za CCM alikuja kuniunga mkono ana moyo ya kipekee hana kinyongo, Mungu akiniweka hai sitochukua fomu, Makalla akichukua," amesema Zeeland.
Ukiachana na hayo, katika ziara hiyo iliyoanzia jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kuliibuka mambo mbalimbali ikiwemo Makalla kumjibu Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kuhusu CCM kuketi na Chadema.
Mambo mengine ni CCM kuwakingia kifua wanaohama Chadema kikisema ni haki yao ya msingi, pia Makalla aliwapokea na kuwakaribisha makada wa Chadema, sambamba na kutoa hakikisho la kukoma kwa kero za maji na barabara za wilaya za Malinyi na Ulanga mkoani humo.
Makalla alitumia ziara hiyo kuwajenga kisaikolojia WanaCCM na wananchi kutambua kwamba uchaguzi upo kama kawaida na wasitishike na maneno yatakayosemwa na viongozi wa Chadema watakaofanya ziara hivi karibuni mkoani humo.
Walichokisema WanaMvomero
“Naona wote wawili Makalla na Zeeland uwezekano wa kuchukua fomu ya kugombea ubunge upo mkubwa maneno ya majukwaani sio ya kuyatilia umakini hasa kipindi hiki," amesema Juma Majid.
Mkazi wa kijiji cha Manyinga, Sophia Angerus amesema Zeeland ameonyesha heshima kubwa kwa Makalla kutokana na kitendo cha kuungwa mkono katika uchaguzi uliopita mwaka 2020 ambao mwenezi huyo aliongoza.

“Kazi ninayoona ni mchuano mkali kati ya Jonas Van Zeeland na Murad Sadiq ubunge mwaka huu na kujiondoa kwake Makalla naona huenda kwa sababu ya nafasi aliyonayo sasa ndani ya CCM na wamewekeana heshima kubwa sana kisiasa,” amesema Sophia.
Ally Salim amesema cheo cha uenezi alichonacho Makalla ni nafasi kubwa ndani ya CCM, hivyo uamuzi wa kutogombea ni sahihi ili kulinda heshima yake katika duru za siasa.
“Makalla yupo sahihi kwa sababu cheo chake ni kikubwa kuliko ubunge na habari zilizojificha kuwa yupo kijana ambaye hafahamiki kisiasa ndio anaandaliwa kugombea ubunge kushindana Zeeland," amesema Salim.
Kwa mujibu Salim, kitendo cha Zeeland kutoa kauli ile ni kama kumuomba Makalla asigombee nafasi hiyo ili atetee nafasi yake.
Awakaribisha makada wa Chadema
Katika ziara hiyo, Makalla kila aliposimama jukwaani alitumia dakika kadhaa kuwakaribisha makada wa Chadema wanaokihama chama hicho kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kutoridhishwa na mwenendo wa uongozi chini ya Tundu Lissu.
Miongoni mwa waliokaribishwa ni pamoja na waliowahi kuwa wajumbe wa sekretarieti ambao ni John Mrema, Salum Mwalimu na Benson Kigaila, Julius Mwita na Catherine Ruge waliotangaza kujivua uanachama wa Chadema.
Katika hatua nyingine, Makalla aliwakingia kifua makada wanaohama Chadema akisema hajawafika bei wala kuhongwa kama ambavyo Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) anavyowatuhumu.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya za Ulanga na Malinyi, Makalla ameitaka Chadema kutotafuta mchawi kuhusu wanaokihama chama hicho, kwa sababu wamechochwa na yanayoendelea hasa msimamo wa No reforms, no election unaokwenda kuzima ndoto za wanaotaka ubunge na udiwani.
Makalla ametumia ziara yake kuwaomba wananchi kuwa makini na maneno ya viongozi wa Chadema watakaofanya ziara mkoani humo kwa siku za karibuni, akiwataka kuwapuuza hasa ajenda yao ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
Wapokea ushauri wa Jaji Warioba
Katika ziara hiyo, Makalla amesema CCM imeupokea ushauri wa Jaji Joseph Warioba aliyeshauri kuweka meza ya mazungumzo kati ya Serikali, Chama cha Mapinduzi na Chadema ili kumalize tofauti zao kabla ya uchaguzi.
Makalla alisema wameupokea ushauri huo na wanaheshimu Warioba lakini hakiwezi kuutumia kwa sasa kwa kuwa CCM hakina mgogoro na Chadema na wanashirikiana katika mambo mbalimbali.
Ushauri huo ulitokana na kile alichokisema Jaji Warioba kuwa endapo hilo halitafanyika nchi itaingia katika uchaguzi ikiwa katika mgawanyiko kuanzia viongozi na wananchi, huku akisema dawa peke yake ipo katika meza ya mazungumzo na si mapambano ya lugha zinazoligawa Taifa zilizopo sasa.
Aahidi neema kero za maji, barabara
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa majimbo ya Morogoro Kusini na Mashariki, Malinyi na Ulanga, Makalla amewaahidi kuwa atazifikisha kero zao za maji na barabara kwa viongozi wakuu akiwemo Rais Samia.

"Kuona ni kuamini, nimekuja nimeona hasa changamoto za barabara niwaambie Waziri wa Ujenzi (Abdallah Ulega) atakuja huku, lakini nitazifikisha kero zenu kwenye mamlaka husika," amesema Makalla.