Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalam wa Tehama wajadili 'miji maridadi'

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe akizungumza katika mkutano wa wataalam wa Tehama ulioandaliwa na Shirika la Mawasiliano duniani(ITU), leo Jumatano Septemba 13, 2023 jijini Arusha. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), wataalam na wabunifu hao wanazungumzia mpango huo wa maboresho ujulikanayo kama 'miji maridadi,' ambao utaboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Arusha. Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kutoka nchi mbalimbali duniani, wameanza mkutano wao mkoani hapa wakijadili namna ya kuboresha huduma katika miji na majiji.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), pamoja na kuboresha huduma katika miji, mkutano huo wa siku 14, utaangazia namna matumizi ya teknolojia yanavyoweza kukuza uchumi wa kidijitali.

Akizungumza katika mkutano huo, leo Jumatano Septemba 13, 2023; Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew, amesema matumizi ya Tehama yatasaidia na kuongeza ufanisi wa huduma za Serikali.

Na kwamba, ufanisi huo, unaifanya serikali kuweza kutimiza azma ya kuwa na miji maridadi na hivyo kupunguza changamoto kwa wananchi.

Naibu Waziri huyo amesema, miaka 38 iliyopita, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa ITU na kuwa kupata fursa ya kufanyika mkutano huo nchini, utasaidia kubadilishana uzoefu katika masuala ya Tehama.

"Wanapopanga vile viwango na kuona teknolojia ipi itatumika wapi, wanajaribu kuangalia sera na sheria zipi ziwekwe, ili kuweza kumudu aina ya teknolojia inayokuja kuibukia au iliyoibukia ili sasa dunia nzima tunapoongelea suala la viwango, basi tuende pamoja,” amesema na kuongeza;

“Tunahitaji kuwa na miji ya kisasa, ambayo lazima iwepo teknolojia itakayotuwezesha...kikao hiki watoa huduma wameshiriki, Serikali itaendelea kujifunza, kujipanga na kuweka sera ambazo zitaweza kuendana na mabadiliko ya teknolojia, na hili Rais ameshatoa maelekezo, tunaanza kupitia sera zetu,” amesisitiza Naibu huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, amesema wao wanadhamana ya kusimamia sekta ya mawasiliano, na kwamba watahakikisha teknolojia za kidijitali zinazowezesha ukuaji wa miji ya kisasa inaingia na kutumika nchini kwa ukamilifu.

“Kwanza tunafurahi mkutano huu muhimu umefanyika Tanzania, sisi kama TCRA, tunaweka mazingira sahihi na wezeshi yatakayosaidia teknolojia hizi kukuza miji ya kisasa. Kama mlivyomsikia Naibu Waziri, mpango huu unaanzia jiji la Dodoma, kuhakikisha miji yetu inaongozwa na teknolojia za kisasa za kidijitali, tumejidhatiti,” amesema Dk Bakari.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, amesema miji maridadi ni ile inayotumia Tehama katika kutoa huduma kwa wananchi wake.

“Katika hili tunaona ukiwa na miji maridadi huduma zinakuwa rahisi. Mfano Dodoma tumedhamiria liwe jiji maridadi, sasa mji maridadi faida zake ni pamoja na kuhudumiwa wananchi kwa kiwango cha juu, kutoa huduma bora na kwa wakati,” amesema Profesa huyo