Rais Trump akalia kuti kavu, mchakato wa kumng’oa madarakani waanza

Muktasari:
- Jumatano iliyopita Spika wa Bunge la Marekani, alitangaza mchakato wa kumuondoa madarakani kiongozi huyo.
Washington, Marekani. Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi ametangaza kuanzisha mchakato wa kumng’oa madarakani Rais Donald Trump.
Tamko la Spika Nancy ambalo amelitoa jana ni hatua ya kwanza katika mchakato ambao unaweza kumuondoa Rais huyo madarakani.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la AFP, hatua ya Spika Nancy inafuatia madai kuwa Julai 25 Trump alizungumza kwa simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kutaka msaada wa kumuangamiza mpinzani wake katika kampeni yake ijayo ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020.
Aidha, katika mazungumzo hayo Trump inadaiwa alimshinikiza Rais huyo wa Ukraine kutafuta njia za kuchafua sifa ya makamu wa Rais wa zamani, Joe Biden na mtoto wake, Hunter.
Tayari makamu huyo wa Rais ameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo kupitia tiketi ya Chama cha Democratic hivyo kuzidisha joto la uchaguzi huo kwa kutoa upinzani kwa Rais Trump ambaye atakuwa akitetea nafasi yake baada ya kumaliza kipindi cha kwanza cha uongozi wake.
Lakini jana Spika Nancy alisema “inasikitisha sana kufikiria kwamba Rais wetu anaweza kufanya kosa la kufunguliwa mashtaka. Ni ngumu unajua? Ni ngumu kusema tumefika katika hali hiyo,” alisisitiza Spika Pelosi akitoa taarifa hiyo kwa njia ya televisheni.
Kupitia tangazo lake Spika Nacy alisema uchunguzi maalumu utafanywa ili kubaini ukweli kisha kura zitapigwa na wabunge kupata fursa ya kuamua.
Spika Pelosi aliongeza kuwa kamati nyingine sita zinazofanya uchunguzi wa masuala mengine dhidi ya Trump zitaendelea na kazi yao chini ya uchunguzi wa sasa.
Rais Trump yuko katika wakati mgumu kutokana na hoja hiyo kuungwa mkono na wafuasia wa Chama cha Democrats juu ya uchunguzi huo ambao unaweza kumuondoa madarakani.
Ikiwa uchunguzi huo utaendelea, Bunge la Congress litapigia kura mashtaka yoyote yatakayobainika na kwa kuwa chama cha Democrats ndio kina wawakilishi wengi katika muhimili huo lo kinaweza kupitisha umuzi mgumu dhidi ya Rais Trump.
Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa iwapo mchakato huo ukiendelea huenda usipitishwe na Baraza la Seneti ambalo lina wajumbe wengi kutoka Chama cha Republicans na kwa mujibu wa sheria inahitajika theluthi tatu ya kura za wabunge hivyo ni rahisi kwao kuzuia mpango.
Mchakato wa kumng’oa Rais Trump umechochewa na ripoti za jasusi aliyefichua malalamiko kuhusu simu ambazo kiongozi huyo alimpigia mwenzake wa Ukrain Rais Volodymyr Zelensky.
Hata hivyo, Trump amekanusha vikali madai hayo na kudai kuwa mazungumzo yalikuwa ya kirafiki huku akizitaja juhudi za kumtuhumu kama hila chafu dhidi yake.
Rais Trump akiri kuzungumza na viongozi hao lakini akasema alikuwa tu akijaribu kuitaka Ulaya iingilie kati kutoa msaada kwa kuitishia kusitisha msaada wa kijeshi.
Trump pia alikubali kwamba kwa muda mfupi alizuia fedha za msaada kwa Ukraine kiasi cha dola milioni 400 ingawa si kwa lengo la kumshinikiza Zelenskiy aanzishe uchunguzi ambao utaharibu sifa ya Biden. Pesa hizo za misaada hatimaye zilitolewa wiki iliyopita.