Visa vya Ebola DRC vyafikia 2,011 wahudumu wagoma
Muktasari:
- Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al Jazeera wahudumu hao waligoma tangu Jumatano katika Hospitali Kuu ya Bunia, mkoani Ituri, kwa kuzuia shughuli za kawaida hospitalini huku wakidai hawajapata malipo yoyote tangu mlipuko wa Ebola ulipoanza, licha ya kuendelea kuhudumia wagonjwa.
Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeendelea kushika kasi baada ya idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kufikia 2,011 huku vifo vikifikia 754, wakati wahudumu wa afya katika eneo lililoathirika zaidi wakianza mgomo wakidai kutolipwa mishahara na kuboreshewa mazingira ya kazi.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al Jazeera wahudumu hao waligoma tangu Jumatano katika Hospitali Kuu ya Bunia, mkoani Ituri, kwa kuzuia shughuli za kawaida hospitalini huku wakidai hawajapata malipo yoyote tangu mlipuko wa Ebola ulipoanza, licha ya kuendelea kuhudumia wagonjwa.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya wahudumu wengine wa afya katika Hospitali Kuu ya Rwampara kusitisha kazi.
Walishiriki katika mgomo huo ni pamoja na wataalamu wa magonjwa ya mlipuko na wafanyakazi wanaosimamia mazishi ya waathirika wa Ebola, wakieleza kuwa hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeuelezea mlipuko huu ni wa tatu kwa ukubwa na unaokua kwa kasi zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya ugonjwa wa Ebola.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa idadi halisi ya vifo inaweza kuwa mara mbili hadi nne zaidi ya takwimu rasmi kutokana na uwezekano wa wagonjwa na vifo vingine kutoripotiwa.
Mlipuko wa sasa ulianza Mei 15 mwaka huu na unasababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo hadi sasa havina chanjo wala tiba iliyothibitishwa.
Hata hivyo, matumaini mapya yanaanza kuonekana baada ya WHO kutangaza kuanza kwa jaribio la kwanza la kitabibu la dawa inayolenga kuzuia maambukizi kwa watu waliokutana na wagonjwa wa virusi vya Bundibugyo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema majaribio hayo yalianza Jumanne na yanalenga kubaini kama dawa hiyo inaweza kuwakinga watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa baada ya kuathiriwa na virusi hivyo.
"Ikiwa dawa hiyo itaonyesha ufanisi kwa watu walio katika hatari kubwa baada ya kuathiriwa na virusi vya Bundibugyo, inaweza kuwa hatua muhimu katika kuzuia maambukizi ya aina hii ya Ebola," amesema Tedros kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.
Mlipuko wa sasa unaendelea kuibua hofu kwa jumuiya ya kimataifa, huku wataalamu wakisisitiza kuwa mafanikio ya juhudi za kuudhibiti yatategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa wahudumu wa afya, ufuatiliaji wa wagonjwa na kuimarishwa kwa huduma za matibabu katika maeneo yaliyoathirika.