Moto wateketeza kituo cha watoto yatima Algeria, 11 wafariki dunia
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Shirika la Ulinzi wa Raia la Algeria, moto huo ulizuka leo Alhamisi Julai 16,2026 saa 3:30 usiku kwa saa za nchini humo ndani ya Taasisi ya Msaada kwa Watoto (Childhood Relief Institution), inayotoa huduma za makazi, matibabu na msaada wa kijamii kwa watoto yatima, waliotelekezwa na wenye mahitaji maalumu.
Watu 11 wamefariki dunia na wengine 19 kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika kituo cha kulelea watoto kilichopo Mohammadia, mashariki mwa mji mkuu wa Algeria, Algiers.
Kwa mujibu wa Shirika la Ulinzi wa Raia la Algeria, moto huo ulizuka usiku wa kuamkia leo Alhamisi Julai 16,2026 ndani ya Taasisi ya Msaada kwa Watoto (Childhood Relief Institution), inayotoa huduma za makazi, matibabu na msaada wa kijamii kwa watoto yatima, waliotelekezwa na wenye mahitaji maalumu.
Taarifa ya shirika hilo imeeleza kuwa wahudumu wa dharura waliwahudumia watu 10 walioungua kwa viwango tofauti vya majeraha, huku wawili wakipata matatizo makubwa ya kupumua kutokana na kuvuta moshi.
Aidha, watu saba walipatiwa huduma baada ya kupata mshtuko wakati wakazi watano wenye mahitaji maalumu walihamishwa na kupelekwa eneo salama.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mamia ya wakazi wakifuatilia operesheni ya uokoaji, huku picha zilizotolewa na Shirika la Ulinzi wa Raia zikionyesha askari wa zimamoto wakipambana na moshi mzito uliotanda kwenye korido za jengo hilo wakati wakiendelea kuwaokoa watoto na wafanyakazi.
Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, ametuma salamu za pole kupitia mitandao ya kijamii, akieleza kusikitishwa na taarifa za vifo hivyo na kujeruhiwa kwa wengine katika tukio hilo.
Waziri Mkuu wa Algeria, Sifi Ghrieb ametembelea Hospitali ya Chuo Kikuu ya Mustapha Pacha mjini Algiers kuwajulia hali majeruhi na kufuatilia utoaji wa matibabu.
Vyombo vya habari vya Algeria vimeripoti kuwa operesheni za kuzima moto na utafutaji zimekamilika, huku vyombo vya usalama na mamlaka za uchunguzi vikianza kuchunguza chanzo cha moto huo.