Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Heche: Sitishwi na mashambulizi dhidi yangu

Muktasari:

  • Heche ametoa msimamo huo kwa wajumbe wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Mkoa wa Mara waliofika nyumbani kwake wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Dar ers Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema hatishiki na mashambulizi yanayoelekezwa dhidi yake, akijifananisha na mchezaji hatari uwanjani anayekabwa zaidi.

Ingawa hakuyataja mashambulizi ya aina gani, lakini kauli hiyo inakuja siku kadhaa baada ya baadhi ya makada na viongozi wa Chadema kujitokeza hadharani wakimtuhumu Heche kula fedha za michango, wakitaka achukuliwe hatua za kinidhamu.

Kutokana na tuhuma hizo, uongozi wa Chadema Kanda za Kaskazini na Kati uliwasimamisha uongozi viongozi sita na kada mmoja, huku ukiwataka kujieleza na kuwasilisha ushahidi ndani ya siku 14 kuhusu madai hayo dhidi ya Heche.

Aidha, Chadema ilisema itaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na wanachama watakaokiuka kanuni za chama, ikiwamo kupeleka malalamiko kwenye vyombo vya habari badala ya kutumia vikao halali vya chama.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche akizungumza na uongozi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Mkoa wa Mara, waliofika nyumbani kwake Tarime kumfariji baada ya kifo cha dereva wake Suez Maradufu.

Akizungumza jana Jumatano Julai 15, 2026 na Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Mkoa wa Mara waliofika nyumbani kwake wilayani Tarime, Heche amesema mchezaji mwenye mpira ndiye anayekabwa.

“Ukiona mpira unachezwa yule mwenye mpira ndiye anayekabwa, kwa hiyo hata haya unayoyaona wanaita mashambulizi dhidi yangu ni kwa sababu mpira upo hapa.

“Kwa hiyo wala msiwe na wasiwasi, sina muda huo wa kujibizana. Ufalme wa CCM ulishaondoka, umehamia Chadema ‘free Tundu Lissu’  Katiba Mpya, haya mengine mengine siyasikilizi,” amesema Heche.

Heche ambaye ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini mkoani humo, amesisitiza yeye si mtu wa kutishwa wala kurudishwa nyuma kwa maneno aliyoyaita ya khanga.

“Mimi si mtu wa kutishwa mimi, yaani unaweza kunirudisha nyuma kwa maneno ya mtaani ya khanga? Sitishwi na maneno nasonga mbele,” amesisitiza Heche.

Jana, Jumatano Mwanasheria wa Chadema, Dk Nshala Rugemeleza amesema chama hicho kinaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na wanachama wanaokiuka kanuni za chama hicho ikiwemo kupeleka malalamiko kwenye vyombo vya habari badala ya kutumia vikao halali.

Dk Rugemeleza amesema viongozi au makada wanaofanya hivyo hawana tofauti na wasaliti dhidi ya chama hicho.

“Wanaokubali kuingia katika mfumo watachukuliwa hatua, waache waseme maneno yao machafu lakini hatua za kinidhamu chama zitafanywa na zinafanywa dhidi yao. Chama hakitawasahau usaliti na uasi wao na tutachukua hatua zinazostahiki.

“Watu waovu hatuwezi kuwasamehe, kwa sababu wanakisaliti chama, wanastahili adhabu ya kutoka hatuwezi kukaa na wasaliti watakaoshughulikiwa kwa mujibu wa chama chetu kwa wakati unaostahili;  watapata adhabu yao, hawatasamehewa wote wanaojijua watambue Chadema ‘bye bye,” amesema Dk Rugemeleza.

Miongoni mwa waliosimamishwa uongozi ni aliyekuwa Katibu wa Jimbo la Bumbuli, Abubakari Mashambo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, Amuli Shindo, Joseph Mwakidasi na Mathias Cosmas waliokuwa wenyeviti wa Chadema wilaya za Mkinga, Kilindi na Muheza, mkoani Tanga.

Mbali na hao, yumo pia kada mpya wa chama hicho, Joseph Selasini aliyepewa barua na tawi lake la Maharo wilayani Rombo, akitakiwa kujieleza kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya chama hicho.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Selasini anatuhumiwa kutoa matamko na shutuma dhidi ya Heche bila kufuata utaratibu wa chama wa kuwasilisha malalamiko kupitia vyombo vya ndani kwa mujibu wa Katiba na kanuni za Chadema.