Zari kwa Diamond hakumuacha mtu salama

Muktasari:
- Uhusiano wa Diamond na Zari kutoka Uganda ulidumu kwa takribani miaka minne na kujaliwa watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016) ambao wanaishi Afrika Kusini na mama yao pamoja na kaka zao watatu.
Dar es Salaam. Kulingana na hali ya sasa tunaweza kusema kuwa Zari 'The Bosslady' Hassan alifanikiwa sana kuwaweka chini ya ulinzi Wema Sepetu, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna katika ile vita ya kupigania mapenzi yake kwa Diamond Platnumz.
Uhusiano wa Diamond na Zari kutoka Uganda ulidumu kwa takribani miaka minne na kujaliwa watoto wawili, Tiffah (2015) na Nillan (2016) ambao wanaishi Afrika Kusini na mama yao pamoja na kaka zao watatu.
Je, ni lini na kwa namna gani Zari The Bosslady mwenye nguvu kubwa ya ushawishi katika mitandao ya kijamii akiwa namba moja Afrika Mashariki alipambana dhidi ya Wema, Hamisa na Tanasha?
Zari & Wema
Mtandao wa Instagram hapo Januari 2016 uligeuka uwanja wa kutupiana maneno makali kati ya timu Zari na Wema ambaye ni Miss Tanzania 2006 ukiwa ni mwendelezo wa visa vilivyoanza tangu 2014 ulipoanza uhusiano wa Zari na Diamond.
Hiyo ni baada ya maneno kutoka kwa kambi ya Wema kwenda kwa Zari, haikuchua muda Mama Tiffah akawasha moto akiponda mtindo wa maisha wa Wema kwa madai anaishi maisha yenye uongo mwingi kuanzia magari anayomiliki, nyumba na hata mahusiano.

Naye Wema alijibu kwa kumtaka Zari aweke hadharani majibu ya vipimo vya DNA kama ana uhakika kuwa Tiffah ni mtoto wa Diamond kitu ambacho Zari alionyesha kukipuuzia kwa madai kuwa Wema ana maumivu ya kuachwa na Diamond.
Kwenye moja ya mahojiano yake mwaka huo, Wema alidai licha ya kuzama kwenye penzi jipya na Idris Sultan, bado Zari alizidi kumwandama hadi kufikia hatua ya kumzuia (block) kwenye ukurasa wake wa Instagram ili kuepusha maneno.
Hata hivyo, mwaka mmoja nyuma, Wema alionekana akijiachia Afrika Kusini na aliyekuwa mume wa Zari na baba watoto wake watatu, Marehemu Ivan Ssemwanga. Jambo hilo lilitafsiriwa kama amelipiza kisasi kwa Zari mara baada ya kuuteka moyo wa Diamond.
Zari & Hamisa
Mwanamitindo Hamisa ambaye kwa sasa ameolewa na Aziz Ki, alikuwa ni rafiki wa Diamond na Zari kwa wakati mmoja, hata katika sherehe ya 40 ya kuzaliwa kwa Tiffah, Hamisa ni miongoni mwa waliomtunza Zari fedha nyingi.
Hata hivyo, urafiki huo uliingia doa kufuatia Hamisa kubeba ujauzito na hapo ndipo zikaanza tetesi kuwa Diamond ndiye mhusika ingawa mwenyewe alitupilia mbali hilo lakini haikuzuia kuibuka kwa timu zao ambazo ziliraruana mitandaoni.
Ndani ya muda mfupi vita kati ya Zari na Hamisa ilikuwa kali sana hadi Agosti 2017 ambapo Diamond alikiri kuwa mtoto huyo wa pili wa Hamisa ni wake, huku akimuomba radhi Mama Tiffah kwa madai kuwa ni shetani alimpitia!

Hata hivyo, hilo halikumuacha salama Diamond, kwani Februari 2018, Zari alitangaza hadharani kuachana na Diamond kwa kueleza amemvunjia utu wake, pia atawafundisha watoto wake wa kiume kuwaheshimu wanawake.
Licha ya kuachana, Zari alizidi kutupa vijembe vya kutosha kwa Hamisa na timu yake kuonyeshwa kuchukizwa na alichokifanya, lakini kwa upande mwingine Hamisa alionyesha kutojali sana na baadaye alieleza kuwa hana hatia yoyote.
"Wakati nakutana na Diamond nilijua kuna Zari na nilimuuliza, akasema mimi ni Muislamu nina uwezo wa kuoa hata wanawake wawili. Na mimi nipo tayari hata kama ningekuwa nimeolewa halafu mume wangu anataka kuoa mke wa pili ningemruhusu," alisema Hamisa.
Zari & Tanasha
Kuanzia Desemba 2018 zilianza tetesi kuwa Diamond ana uhusiano na mtangazaji wa NRG Radio Kenya ambaye ni Tanasha, basi penzi lao likamea na kushamiri hadi kujaliwa mtoto wa kiume na kumpa jina la Naseeb Junior (2019).
Wakati penzi la Tanasha na Diamond limeanza kupamba moto hasa kwenye mitandao ya kijamii, Tanasha aliandika Instagram; "Ndugu wenye chuki nina mengi sana ya kufanya mchukie, endeleeni kuwa wavumilivu".
Kwa haraka wengi walihisi ujumbe wa Tanasha ameutuma kwa Zari ambaye miezi michache nyuma alitoka kuachana na Diamond, na ndipo akaulizwa iwapo anamfahamu Zari, alijibu hamfahamu na kutaka watu waache kuchochea vita visivyo na maana.

"Hapana simjui, lakini nadhani ni mama wa watoto wawili, najua ni mama mrembo anayefanya kazi na anayejituma sana na watu inabidi waache kufananisha na kuchochea drama ambazo hazina maana na badala yake wawape wanawake nguvu," alijibu Tanasha.
Hata hivyo, Zari aliibuka na kumsikitikia Tanasha kwa kupewa ujauzito na Diamond ambaye alimtaja kama baba wa watoto watatu asiyewajibika. Hiyo ilikuwa Juni 2019 Zari akiwa Kenya kwa mwaliko wa Akothee.
"Kuna mtu anasema Tanasha ni mjamzito, commets zinakuja kila mara, ni vizuri kuwa mjamzito, ni kitu kizuri, lakini ni kitu kingine ukiwa ni ujauzito wa baba wa watoto watatu asiyewajibika, kwa hiyo inanifanya nihoji vipaumbele vyake," alisema na kuongeza:
"Kwa hiyo hongera nina matumaini (Tanasha) una fedha ya kutosha benki kwa ajili ya kumtunza mtoto huyu kwa sababu (Diamond) yupo hivyo alivyo," alisema Zari akizungumza kupitia Insta Live.
Na wakati imeripotiwa kuachana kwa Tanasha na Diamond hapo Machi 2020, Zari hakukaa kimya, aliibuka na kusema, "Haijalishi ni mara ngapi nyoka anajivua gamba lake, ataendelea kuwa nyoka pia!"
Ila baadaye wawili hao walionekana kumaliza tofauti zao, hiyo ni baada ya Tanasha kuhudhuria Zari All White Party iliyofanyika jijini Kampala hapo Desemba 2023, walipiga picha nyingi wakiwa pamoja na hadi sasa hakujawahi kusikika ugomvi kati yao.