Prime
Mambo matano ziara Dk Nchimbi Mara

Muktasari:
- Mambo hayo yote yamejidhihirisha kupitia hotuba na salamu za Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi alizozitoa kwa nyakati tofauti, akiwa kwenye Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mara alikofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25 kuanzia, Aprili 22 hadi 26, mwaka huu.
Dar es Salaam. Siku sita za ziara ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi mkoani Mara, zimetosha kwa chama hicho kujitenga na kauli hatari dhidi ya upinzani, kuziweka mtegoni wizara tatu na kuwafichua watiania kimyakimya wa nafasi za ubunge kupitia chama hicho.
Hayo yote yamejidhihirisha kupitia hotuba na salamu za Dk Nchimbi alizozitoa kwa nyakati tofauti, akiwa kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mara alikofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25 kuanzia, Aprili 22 hadi jana Jumamosi 26, 2025.
Katika ziara hiyo, mtendaji mkuu huyo wa CCM, alipiga marufuku chama hicho kutumia wimbo wenye maudhui yanayosababisha chuki dhidi ya upinzani, huku akikitaka kuwa mfano wa lugha zinazoleta mshikamano wa Taifa.
Sambamba na hilo, Dk Nchimbi ambaye ndiye mgombea mwenza mteule wa urais wa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa Oktoba 2025, alitoa maelekezo kwa wizara na mawaziri mbalimbali ndani ya ziara hiyo, yakiwemo yanayopaswa kutekelezwa kabla Bunge halijavunjwa.
Kama hiyo haitoshi, ziara hiyo pia ilihusisha maelekezo mahususi kwa wabunge wanaotaka kuwania tena nafasi hizo, kuwataja hadharani watu wanaoona watakuwa washindani wao katika mchakato wa ndani ya chama hicho na waahidi kushirikiana iwapo yeyote kati yao atapitishwa.
Ukiacha hilo, Dk Nchimbi ametumia moja ya salamu zake kwa wananchi ziarani humo, kuwapa jukumu wajumbe watakaopiga kura za maoni kuwapitisha wagombea mbalimbali, wasikilize maoni ya wananchi.
Hoja na maelekezo hayo ya mtendaji mkuu huyo wa CCM, yanatazamwa na wataalamu wa siasa kuwa, msingi wake ni hulka na uzoefu alionao kiongozi huyo ndani ya chama hicho.
Kuhusu karipio dhidi ya kauli za chuki kutoka CCM kwenda upinzani mwanazuoni wa historia, Philemon Mtoi, amesema, "mtazamo wake (Dk Nchimbi) unaweza usipendwe na wahafidhina lakini kwangu mimi ni mzuri sana katika kujenga Taifa la watu wamoja na wanaopendana."
Kauli chafu dhidi ya upinzani
Alipokuwa Shirati wilayani Rorya akizungumza na wananchi, Dk Nchimbi ameonyesha kukerwa na nyimbo na kauli mbaya kutoka ndani ya chama hicho dhidi ya upinzani, akisema CCM inapaswa kuwa mfano wa lugha zinazowaunganisha Watanzania.
Kwa sababu chama hicho ndicho kilicholiasisi Taifa, amesema wanachama wake hawapaswi kuwa chanzo cha uchochezi, vurugu na namna yoyote itakayochochea umwagaji damu nchini.
Ameijenga hoja hiyo akirejea sehemu ya wimbo unaosikika katika kipande cha video kilichosambaa mtandaoni kikionyesha wafuasi wa CCM wakiimba wimbo fulani dhidi ya vyama vya upinzani.
Maneno ndani ya wimbo huo yanasikika, ...pinzani ukifa... mimi siwezi kulia... nitawatupa mtoni, wawe chakula cha mamba."
Baada ya Dk Nchimbi kuwasikilizisha kipande hicho cha video wananchi wa Shirati mkoani Mara, hapo hapo alipiga marufuku kisitumike popote dhidi ya vyama vya upinzani.
"Hayajengi upendo miongoni mwa Watanzania, lazima zitafutwe nyimbo zinazohamasisha upendo bila kusababisha chuki kwa wengine. Wimbo wa namna hii, mimi kama Katibu Mkuu wa CCM napiga marufuku kutumika dhidi ya upinzani," amesema.
Akizungumzia hilo, Mwanazuoni wa Historia, Philemon Mtoi amesema kila hoja ya mwanasiasa huyo msingi wake ni hulka na uzoefu wake ndani ya CCM.
Philemon amesema mwanasiasa huyo sio mhafidhina bali ni mtu aliyejijenga katika itikadi za uliberali na hata alipo sasa kumetokana na mapito aliyopitia akiwa ndani ya CCM.
"Ni kiongozi mwenye misimamo isiyotikisika. Ni mtu anayesoma alama za nyakati anayetamani kuona siasa za hoja pasipo kuumizana," amesema.
Mwanazuoni huyo amesema tangu Dk Nchimbi alipokuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akihamasisha umoja na mshikamano wa kitaifa na aliyetamani kuona tofauti za vyama haziwatenganishi Watanzania.
"Mtazamo wake unaweza usipendwe na wahafidhina na ya chama lakini kwangu mimi ni mtazamo mzuri sana katika kujenga taifa la watu wamoja na wanaopendana," ameeleza.
Hata hivyo, amesema iwapo hoja zake zingekuja na msukumo wa nguvu kuanzia kwenye vikao vya juu vya CCM, kungeshuhudiwa mabadiliko na utengamano wa kisiasa wa hali ya juu nchini.
"Kwa siasa za nchi nyingi za Afrika, hasa zile zenye vyama vikongwe vya ukombozi, chama hupenda kuwa na nguvu dhidi ya Serikali na msingi huo umejengwa katika dhana kwamba mkataba, au ilani imeandaliwa na chama na lazima wafuatilie utekelezaji wake.
"Japokuwa kwa Tanzania hatujawahi kuona chama kikimuwajibisha mwenyekiti wa chama taifa pale anapokosea," amesema Philemon.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, amesema ni matamanio yake kuona kauli hiyo inaendana na uwajibishaji wa wanaofanya makosa hayo.
Amesema iwapo watawajibishwa, itaonekana dhahiri kuwa CCM imedhamiria kukomesha kauli na nyimbo mbaya.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Msigani Dar es Salaam, Reinhad Chikando amesema kauli ya Dk Nchimbi ni muhimu na inalenga kudhihirisha kuwa chama hicho ni kiongozi wa vingine.
Wagombea watambuane
Akiwa katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, Dk Nchimbi amewataka wabunge wenye nia ya kugombea tena, wanawatambua watakaoshindana nao katika mchakato wa ndani wa chama hicho na wakiri hadharani kushirikiana iwapo yeyote atapitishwa.
Amesema kitendo hicho, kitathibitisha uhalisia kuwa uchaguzi si ugomvi, bali ni suala la Watanzania wanamtaka nani awaongoze kwa wakati huo na pengine baadaye wakamchagua mwingine.
Dk Nchimbi alieleza tamanio lake hilo, baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kumtaja hadharani mshindani wake, Nikolaus Chichake na kukiri kuwa hata ikitokea amepitishwa na chama hicho, atamshika mkono na kumtembeza katika kata zote za jimbo hilo.
"Leo kwa mara ya kwanza Waitara kawafundisha wana CCM Tanzania nzima. Uchaguzi sio ugomvi ni suala la Watanzania wanamtaka nani sasa hivi wewe pengine watakuona baadaye," amesema.
Kuhusu hilo, Chikando amesema itasaidia kuvunja vinyongo baada ya mchakato wa kura za maoni ambao aghalabu huisha kwa manung'uniko.
"Mtu akimtaja hadharani mshindani wake na akaahidi kumuunga mkono iwapo atapitishwa, inapunguza vita ya kiuchaguzi, kwa sababu kushindana kimyakimya kunazaa chuki na uadui," ameeleza.
Jukumu kwa wajumbe
Dk Nchimbi pia, aliwataka wajumbe watakaopiga kura za maoni, wachague wagombea kwa kuwasikiliza wananchi wanamtaka nani apitishwe ili wampigie kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.
Sababu ya kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, ni kiu ya chama hicho katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu, kupata wagombea watakaokubalika na wananchi na sio wanaopitishwa kwa nguvu ya fedha zao, huku akiwasisitiza wajumbe wafanikishe hilo.
Amesema chama hicho kinatambua kuwepo kwa wabunge wake waliopitishwa na kushinda uchaguzi, lakini wamehudumu kwa miaka mitano bila kurudi majimboni walipo wananchi waliowachagua.
Katika kufanikisha kiu ya CCM kupata wagombea watakaokubalika na wananchi, amesema kumefanywa maboresho ya kikanuni kuongeza idadi ya wajumbe watakaopiga kura za maoni.
Idadi iliyopo sasa, amesema inaondoa kasumba waliyokuwa nayo baadhi ya wagombea, kuhesabu wajumbe na kuwapa fedha ili wawachague.
"Kulikuwa na watu ndani ya miaka mitano hawafanyi kazi wanaishia kuhesabu kwamba wajumbe wangapi awape fedha wampitishe, sasa hivi tumewaongezea wajumbe kama kuwapa fedha, kwa sasa utawapa wangapi," amesema.
Hata hivyo, Dk Nchimbi amesema pamoja maoni ya mjumbe binafsi, siku ya kura za maoni wananchi wasiogope kuwaambia wanataka nani akapigiwe kura ili apitishwe kwa sababu ndiye hitaji lao.
"Waambieni bila woga kwamba tuleteeni mtu fulani tutampa kura zote," amesema.
Kuhusu hilo, Philemon amesema hiyo ndio hoja ya msingi ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na amekuwa akizungumza wakati wote.
"Rais Samia anaonyesha hataki kupata wabunge ambao hawana msaada kwake, anataka wenye uwezo wa kumsaidia katika shughuli za Serikali," amesema.
Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, katika uchaguzi wa mwaka huu huenda wakashuhudiwa wabunge wengi wa CCM ni wale wenye elimu nzuri na watii kwa Serikali.
"Dunia imebadilika na wao wameamua kuja na mchakato ambao utawapa wanachotaka," amesema.
Kuhusu hilo, Dk Masabo amesema pamoja na mabadiliko ya kikanuni yaliyofanywa na chama hicho, muhimu kutengeneze utaratibu wa kuimarisha mamlaka itakayochuja wagombea.
"Hiyo mamlaka inapaswa kuwa na wajumbe wanaokubalika na kuaminika kutoka miongoni mwa wana CCM. Hawa ndio wanaweza kuleta wagombea watakaomudu ushindani," amesema.
Mtego kwa mawaziri
Katika ziara hiyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amejikuta akipokea maelekezo matatu kwa nyakati tofauti.
Alielekezwa na Dk Nchimbi kuhakikisha anatoa fedha kabla Bunge halijavunjwa kumlipa mkandarasi anayetengeneza jenereta katika Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Julius Nyerere ili akamilishe kazi haraka.
Pia, waziri huyo alielekezwa ndani ya siku 14 kuhakikisha anatoa fedha kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika Wilaya ya Bunda.
Maelekezo kama hayo, aliyatoa pia kuhusu kutolewa kwa fedha za kukamilisha malipo ya mkandarasi wa Uwanja wa Ndege Musoma ili ukamilike haraka kama ilivyopangwa.
Dk Nchimbi pia, alimwelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana kushirikiana na Mkoa wa Mara kuona namna watakavyoharakisha tathmini kwa ajili ya wananchi waliopisha eneo hilo la ushoroba.
Kwa upande wa Wizara ya Maji, inayoongozwa na Waziri Jumaa Aweso alielekeza itoe kipaumbele kwa kufanikisha kukamilika kwa mradi wa maji Rorya-Tarime.
Dk Nchimbi amesema mradi huo ni mojawapo ya miradi ya maji mikubwa nchini ambayo inalenga kutatua tatizo kwa muda mrefu ujao, hivyo akahimiza uwekewe msukumo ili wananchi wanaolengwa waanze kupata huduma hiyo.