Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi ataka wanaowania ubunge, udiwani CCM watambuane

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na wananchi wa Nyamongo mkoani Mara, aliposimama kuwasalimia wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetaka wagombea wake kutambuana na kukiri hadharani kwamba yeyote atakayepitishwa ataungwa mkono hata na mshindani wake.

Serengeti. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, amewataka wabunge wenye nia ya kugombea tena, wawatambue watakaoshindana nao katika mchakato wa ndani wa chama hicho na wakiri hadharani kushirikiana iwapo yeyote atapitishwa.

Amesema kitendo hicho, kitathibitisha uhalisia kuwa uchaguzi si ugomvi, bali ni suala la Watanzania wanamtaka nani awaongoze kwa wakati huo na pengine baadaye wakamchagua mwingine.

Dk Nchimbi ameeleza tamanio lake hilo, baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kumtaja hadharani mshindani wake, Nikolaus Chichake, na kukiri kuwa hata ikitokea amepitishwa na chama hicho, atamshika mkono na kumtembeza katika kata zote za jimbo hilo.

Kauli hiyo ni mwendelezo wa nasaha za Dk Nchimbi kuhusu wanachama wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla kukwepa ugomvi na chuki kwa sababu ya uchaguzi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo, Jumamosi Aprili 26, 2025, aliposimama katika msafara wake kuwasalimia wananchi wa Nyamongo, wilayani Tarime katika Mkoa wa Mara, ikiwa ni sehemu ya matukio katika hitimisho la ziara yake ya siku sita.

Amesema angetamani katika eneo lolote atakalotembelea, mbunge wa eneo husika amtaje mtu anayedhania ni mshindani wake katika uchaguzi ujao na athibitishe kukubali kushindana naye na aahidi kumshika mkono iwapo atamshinda.

"Leo kwa mara ya kwanza Waitara kawafundisha wana CCM Tanzania nzima. Uchaguzi si ugomvi, ni suala la Watanzania wanamtaka nani sasa hivi wewe pengine watakuona baadaye," amesema.

Katika salamu zake hizo, amejibu baadhi ya changamoto zilizoelezwa na Waitara, ikiwemo ya maji, akisema CCM itahakikisha Serikali inatoa kipaumbele kumaliza kero hiyo.

Pia, amepongeza hatua zinazochukuliwa na halmashauri ya Tarime kutenga Sh2 bilioni kwa ajili ya mradi wa maji unaohudumia vijiji sita na sasa wanafanya mchakato kwa ajili ya vijiji vingine.

Kuhusu kuharakishwa kwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), amewahakikishia wananchi hao wa Nyamongo, atamwelekeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kufanikisha hilo.

Katika salamu zake hizo, Dk Nchimbi alifikishiwa changamoto ya wachimbaji wadogo kutopatiwa leseni na amejibu tayari ameshawasiliana na waziri husika (Anthony Mavunde) na ameahidi kwenda kulitekeleza hilo Mei 3, 2025.

"Nataka nipewe taarifa na Waitara iwapo Mavunde hatakuja Nyamongo hiyo Mei 3. Labda awe ametumwa na viongozi wakuu wa nchi," amesema.